Ijumaa, tarehe 13 Oktoba, 2023
Leo ni Ijumaa tarehe 27 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1445 Hijria sawa na tarehe 13 Oktoba 2023.
Tarehe 27 Rabiul Awwal miaka 1082 iliyopita alizaliwa mshairi na mwandishi mashuhuri wa Kiarabu, Abul Alaa al Maarry katika mji wa Maarrat al-Nu'man karibu na mji wa Halab (Aleppo) nchini Syria.
Abul Alaa alifariki dunia mwaka 449 Hijria katika mji huo huo ulioko umbali wa kilomita 33 kusini mwa Idlib. Alielekea Baghdad kwa ajili ya kukamilisha elimu ya juu.
Licha ya kuwa kipofu tangu utotoni, lakini Abul Alaa alitokea kuwa mshairi mashuhuri na hodari wa zama zake. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri la "Risalatul Ghufran" na "al Aamali."
Siku kama ya leo miaka 141 iliyopita alifariki dunia mwandishi na mwanafalsafa wa Kifaransa, Joseph Arthur de Gobineau mwanaharakati wa Ufaransa ambaye anajulikana zaidi kwa kusaidia kuhalalisha ubaguzi wa rangi kwa kutumia nadharia ya kisayansi.
Gobineau alizaliwa mwaka 1816 huko Paris na baada ya kumaliza masomo yake alijishughulisha na uandishi wa habari. Gobineau aliwahi kuwa katibu na balozi wa Ufaransa nchini Iran na kupata kujifunza lugha za Kifarsi na Kiarabu. Mwandishi huyo wa Kifaransa aliamini kuwa watu weupe hasa wale wenye asili ya Aryan ndio watu bora zaidi na meandika vitabu kadhaa kuhusiana na kutokuwepo usawa kati ya wanadamu.
Nadharia ya kuwa kizazi cha Aryan ndicho kizazi bora zaidi kuliko vizazi vingine vya wanadamu ni moja ya sababu zilizompelekea Adolf Hitler kuanzisha Vita vya Pili vya Dunia na kuua kwa umati watu wasiokuwa wa asili ya Aryan. **
Katika siku kama hii ya leo miaka 59 iliyopita bunge la kimaonyesho la Iran lilipasisha sheria iliyowapa washauri wa kijeshi wa Marekani nchini kinga ya kutofikishwa mahakamani iwapo wangepatikana na hatia ya aina yoyote (Capitulation Accord) .
Kwa mujibu wa sheria hiyo, wahalifu wa Kimarekani wangehukumiwa nchini kwao kama watatenda jinai nchini Iran, na mahakama za Iran hazikuwa na haki ya kushughulikia kesi zao.
Sheria hiyo ilitambuliwa kuwa dharau kwa taifa la Iran na iliyokiuka wazi kujitawala kwa nchi. Kwa msingi huo hayati Imam Ruhullah Khomeini (MA) siku kadhaa baada ya kupasishwa sheria hiyo bungeni alitoa hotuba ya kihistoria akieleza taathira zake na kumshambulia vikali Mfalme Shah na Marekani. Baada ya hotuba hiyo Imam Khomeini alikamatwa na kupelekwa uhamishoni.

Na Siku kama ya leo Miaka 55 iliyopita, Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim, mkuu wa kituo cha kidini cha Najaf aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 92.
Alipambana vikali na kila kundi au watu waliojaribu kuharibu jina la Uislamu. Fatua yake mashuhuri ya kupinga fikra ya ukomunisti dhidi ya mafundisho ya dini ilileta mabadiliko makubwa nchin Iraq. Fatua hiyo pia ilimpelekea kutoa amri ya kupigana jihadi dhidi ya utawala haramu wa Israel.
Ujenzi wa maktaba, shule na vituo vya kidini na kiutamaduni pamoja na uandishi wa vitabu kama vile Mustamsak Urwat al-Wuthqah na Nahjul Faqaha ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vilivyoandikwa na mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu.