Jumapili, 15 Oktoba, 2023
Leo ni Jumapili 29 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1445 Hijria mwafaka na tarehe 15 Oktoba 2023 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 481 iliyopita alizaliwa Abul-Fat'h Jalal al-Din Muhammad Akbar, mfalme aliyekuwa na nguvu kubwa wa silsila ya Teimurian nchini India. Mfalme huyo alikuwa maarufu kwa jina la Akbar Shah na alichukua madaraka akiwa na umri wa miaka 13 baada ya kufariki dunia baba yake, yaani Homayun. Kwa kipindi cha miaka mitano aliongoza nchi akiwa na cheo cha naibu mtawala chini ya usimamizi wa Bairam Khan. Baada ya kushika madaraka kikamilifu alianza kupanua wigo wa utawala wake katika maeneo ya Bengal, Kashmir, Sindh, Punjab, Ahmednagar na Kandahar. Mfalme Abul-Fat'h Jalal al-Din Muhammad Akbar alikomboa kisiwa cha Dakan huko kusini mwa India kutoka mikononi mwa Wareno. Akbar Shah alifariki dunia mwaka 1605. ***
Katika siku kama ya leo miaka 179 iliyopita alizaliwa mwanafalsafa wa Kijerumani Friedrich Wilhelm Nietzsche. Baada ya kuhitimu masomo, Nietzsche alianza kufunza katika Chuo Kikuu cha Basel. Mwanafalsafa huyo alikuwa akipinga dini na misingi ya kimaadili na katika falsafa na mitazamo yake alikuwa akiamini nadharia ya "Superman", kwa maana ya mtu mwenye uwezo kupita kiasi. Nietzsche alikuwa akiamini kwamba, mtu mwenye uwezo kupita kiasi au Superman ni matokeo ya irada na matashi ya mwanadamu na huwa juu ya mema na mabaya yote. Mwanafalsafa huyo ameandika vitabu kadhaa ikiwa ni pamoja na Beyond Good and Evil, The Birth of Tragedy na Thus Spoke Zarathustra. Katika kipindi cha mwishoni mwa uhai wake Friedrich Wilhelm Nietzsche alipoteza mlingano wa kifikra na alifariki dunia mwaka 1900. ***
Miaka 79 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 29 Rabiul-Awwal, kuliasisiwa taasisi ya kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu huko Cairo Misri. Taasisi hiyo ilianzishwa kwa hima na juhudi kubwa za Muhammad Taqi Qomi mwakilishi wa Ayatullah Sayyid Hussein Tabatabai Boroujerdi, Marjaa Taqlidi katika zama hizo na Imamu wa al-Azhar Sheikh Muhammad Shaltut. Watu kama Sayyid Jamal al-Ddin Asadabadi, mashuhuri kama Jamal Afghani, Sheikh Muhammad Abdu, Sheikh Muhammad Hussein Kashif al-Ghitaa na Sheikh Abdul-Majid Salim walijihusisha na kubadilisha mawazo na fikra katika uga huo. Baada ya kuasisiwa taasisi hiyo ya kukurubisha maadhehebu zaa Kiislamu iliyojulikana kama Dar al-Taqrib Baina al-Madhahib al-Islamiyah" jarida la "Risalat al-Islam" nalo likaanza kuchapishwa. Jarida hili lilikuwa likichapisha makala za kielimu zenye thamani kuhusiana na madhehebu mbalimbali. ***
Miaka 32 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Bosnia Herzegovina ilijitangazia uhuru kutoka kwa Yugoslavia. Jamhuri ya Bosnia Herzegovina kijiografia ipo kusini mwa baara Ulaya na inapakana na nchi za Croatia na Yugoslavia. Baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia Bosnia Herzegovina iliunganishwa na nchi ya Yugoslavia. Bosnia Herzegovina kama zilivyokuwa nchi zingine kama Serbia, Croatia, Slovenia na nyinginezo nayo ilipagania uhuru na kufanikiwa kujikomboa katika siku kama aya leo. ***
Na leo tarehe 15 Oktoba ni Siku ya Vipofu Duniani. Suala la usalama wa vipofu na haki zao za kijamii daima lilikuwa likipewa umuhimu maalumu katika jumuiya za kimataifa na kwa msingi huo mwaka 1950 Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) na Baraza la Kimataifa la Vipofu zilikutana na kupasisha sheria ya Fimbo Nyeupe na kuitangaza tarehe 15 Oktoba kuwa ni Siku ya Fimbo Nyeupe au Siku ya Kimataifa ya Usalama wa Vipovu. Miongoni mwa vipengee vya sheria hiyo ni pamoja na haki ya vipofu kutumia suhula zote za hali bora ya kimaisha katika jamii, kuwahamasisha watu wa jamii hiyo kushiriki katika masuala ya serikali na kupewa ajira serikalini, kulinda haki za vipofu wakati wa kuvuka barabara na kadhalika. ***
