Oct 21, 2023 02:23 UTC
  • Jumamosi, 21 Oktoba, 2023

Leo ni Jumamosi 5 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1445 Hijria mwafakka na tarehe 21 Oktoba 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 233 iliyopita, alizaliwa malenga wa Kifaransa Alphonse de Lamartine. De Lamartine alitambulika kuwa msanii na mwanafikra mkubwa nchini Ufaransa. Aliwahi pia kusafiri Mashariki na kuishi katika mji mkuu wa Lebanon, Bairut. Aidha miongoni mwa athari za malenga huyu, ni pamoja na "Safari ya Mashariki" na "Kimya cha Malaika". Alphonse de Lamartine alifariki dunia mwaka 1869. ***

Alphonse de Lamartine. De Lamartine

 

Miaka 190 iliyopita katika siku kama hii ya leo, alizaliwa Alfred Nobel mkemia wa Sweden na mvumbuzi wa dynamite. Nobel alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza sayansi ya kemia na baadaye akafanya utafiti mkubwa katika uwanja huo na kufanikiwa kuvumbua mada za mlipuko yaani (dynamite). Kinyume na alivyotarajia, majeshi ya nchi mbalimbali yalianza kutumia dynamite vitani na hivyo kusababisha mauaji ya raia wengi. Mkemia Nobel ambaye alikuwa na utajiri mkubwa na hakufikiri kuwa dynamite ingeweza kutumiwa vibaya, aliamua kutoa utajiri wake kama tuzo na zawadi. Alfred Nobel alifanya hivyo kwa lengo kwamba, tuzo hiyo itolewe kila mwaka kwa shakhsiya aliyefanya kazi kubwa ya thamani duniani katika masuala ya sayansi, fasihi na amani. Hata hivyo kinyume na matakwa yake, leo hii Tuzo ya Amani ya Nobel imechukua sura ya kisiasa na inatumiwa kama wenzo wa kutangaza na kueneza siasa za nchi za Magharibi duniani. ***

Alfred Nobel

 

Katika siku kama ya leo miaka 178 iliyopita mwafaka na tarahe 5 Rabiuthani mwaka 1267 Hijiria, gazeti la kwanza la lugha ya Kifarsi lililoitwa 'Waqai'e Itifaqiyeh' lilianza kuchapishwa mjini Tehran. Gazeti hilo lilianza kuchapishwa wakati wa kutimia mwaka wa tatu wa ufalme wa Nasiruddin Shah Kajjar, kwa amri ya Kansela Mirza Taqi Khan Amir Kabiri. Gazeti hilo lilikuwa likiandika habari za utawala wa wakati huo wa Iran, dunia na makala za kisayansi zilizokuwa zikitafsiriwa kutoka kwenye magazeti ya Ulaya. Gazeti la 'Waqai'e Itifaqiyeh' lilichapisha hadi toleo nambari 472 na baada ya hapo liliendelea kuchapishwa kwa majina tofauti. ***

 

Siku kama ya leo miaka 120 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ismail Nuri Tabarsi, faqihi, mtaalamu mkubwa wa elimu ya teolojia na hadithi. Ayatullah Sayyid Ismail Nuri Tabarsi alizaliwa katika mji wa Mazandaran mwanzoni mwa karne ya 13 Hijiria Shamsia katika moja ya vijiji vya kaunti ya Nur nchini Iran. Baada ya kuhitimu masomo ya msingi alijiunga na chuo cha kidini na baadaye alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya kuendelea na masomo ya juuu. Akiwa Najaf alipata kusoma masomo ya ngazi ya juu ya fiqhi, usulu fiqhi, teolojia na hadithi kwa maulama wakubwa kama Sheikh Morteza Answari, Mirza Habibullah Rashti na Mirza Mohammad Hassan Shirazi maarufu kwa jina la Mirza Mkubwa. Mbali na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji, pia aliandika vitabu vya thamani kama vile 'Kifaayatul-Muwahhidin' chenye juzu tatu. Ayatullah Sayyid Ismail Nuri Tabarsi pia ameandika vitabu vya 'Wasiilatul-Maad fii Sharhi Najaatul-Ibaad' na 'Usuulul-Fiqhi.' Msomi huyo alifariki dunia mjini Kadhimiya, Iraq na kuzikwa huko. ***

Ayatullah Sayyid Ismail Nuri Tabarsi

 

Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Somalia ilipata uhuru na siku hii inajulikana nchini humo kama Siku ya Taifa. Kijiografia Somalia ipo kaskazini mashariki mwa bara la Afrika katika eneo linalojulikana kama Pembe ya Afrika. Mji mkuu wa Somalia ni Mogadishu na lugha rasmi ya nchi hiyo ni Kisomali na Kiarabu. Asilimia 99 ya wananchi wa Somalia ni Waislamu. Nchi hiyo kwa miaka kadhaa ilikuwa chini ya ukoloni wa Italia na Uingereza mpaka ilipojipatia uhuru mwaka 1960 katika siku kama ya leo.***

 

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, vibarua na wafanyakazi wa sekta ya mafuta nchini Iran walianza kufanya mgomo wa nchi nzima wakati wa kujiri harakati za mapambano ya wananchi dhidi ya utawala dhalimu wa Shah. Kufuatia mgomo huo, usafirishaji mafuta nje ulisimamishwa, jambo ambalo liliukatia utawala wa Shah moja ya vyanzo muhimu vya kipato. Aidha kusimamishwa usafirishaji mafuta ya Iran nje ya nchi, kulipelekea kupanda mno kwa bei ya bidhaa hiyo ulimwenguni. Utawala wa Shah ulitumia vitisho mbalimbali ili kuwafanya wafanyakazi hao warejee kazini, lakini mgomo huo uliendelea hadi utawala huo kibaraka ulipoangushwa. Wananchi wanampinduzi wa Iran licha ya kukabiliwa na matatizo mengi yaliyosababishwa na uhaba wa nishati ya mafuta, lakini walisimama kidete na kuuunga mkono mgomo wa wafanyakazi hao wa sekta ya mafuta. ***

 

Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo Brigedia Jenerali Mundhir Abu Ghazala, kamanda Jeshi la Majini la Palestina aliuawa na maajenti wa shirika la ujasusi la utawala ghasibu wa Kizayuni Mossad. Wazayuni walimuuwa kigaidi kamanda huyo wa jeshi la majini la Palestina kwa kutega bomu ndani ya gari lake huko Athens mji mkuu wa Ugiriki. Brigedia Jenerali Abu Ghazala ni miongoni mwa wahanga wa ugaidi wa kiserikali wa utawala wa kibaguzi wa Kizayuni unaoungwa mkono kwa hali na mali na Marekani. ***

Brigedia Jenerali Mundhir Abu Ghazala,