Leo katika Historia, Jumanne tarehe 24 Oktoba 2023
Leo ni Jumanne tarehe 8 Rabiuthanil 1445 Hijria sawa na tarehe 24 Oktoba 2023.
Miaka 1213 iliyopita katika siku kama hii ya leo, yaani tarehe 8 Rabiu Thani mwaka 232 Hijria Qamaria, Imam Hassan Askari AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina.
Akiwa katika umri wa utotoni, mtoto huyo alilazimishwa na makhalifa wa Bani Abbas akiwa na baba yake Imam Hadi AS, kuondoka mji huo na kuhamia katika mji wa Samarra ambao wakati huo ulikuwa makao makuu ya utawala wao. Japokuwa mtukufu huyo hakuweza kuishi zaidi ya miaka 28 lakini aliacha nyuma maarifa muhimu na adhimu ya Kiislamu.
Imam Hassan Askari AS alikuwa na huruma na upendo mkubwa uliokuwa ukiwavutia watu wengi. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Hassan Askary alichukua jukumu zito la kuwaongoza Waislamu sambamba na kueneza mafunzo sahihi ya dini tukufu ya Kiislamu.
Kama walivyokuwa Maimamu wengine watukufu, Imam Hassan Askari naye aliitumia karibu sehemu yote ya umri wake kulinda na kueneza mafunzo sahihi na a'ali ya dini tukufu ya Kiislamu.

Katika siku kama ya leo miaka 1088 iliyopita, Abu Feras Hamdani mshairi na mwandishi wa Kiarabu alifariki dunia.
Sambamba na kuwa mshairi, Abu Feras alikuwa mpiganaji vita na alikuwa mmoja wa watu wa karibu wa Seif al-Daulah mtawala wa Halab na alikuwa mmoja wa makamanda wa jeshi.
Siku kama ya leo miaka 95 iliyopita sawa na tarehe Pili mwezi Aban mwaka 1307 Hijria Shamsia, Ayatullah Dakta Sayyid Muhammad Husseini Beheshti mwanafikra na mwanamapinduzi wa Iran, alizaliwa huko Isfahan, moja kati ya miji ya katikati mwa Iran.
Ayatullah Beheshti alilelewa katika familia ya kidini na alianza kujifunza masomo ya kidini akiwa kijana mdogo. Akiwa na umri wa miaka 18, alielekea katika mji wa kidini wa Qum nchini Iran na kusoma kwa maulamaa wakubwa wa mji huo akiwemo Imam Khomeini (RA). Wakati huo huo, Dakta Beheshti alitumia kipawa chake kikubwa na kuamua kuendelea pia na masomo ya Chuo Kikuu na kufanikiwa kupata shahada ya udaktari katika falsafa.
Dakta Beheshti aliuawa shahidi akiwa na viongozi na shakhsiya wengine 72 wa Iran katika mkutano mwezi Tiir mwaka 1360 Hijria Shamsia baada kundi la kigaidi la Munafiqin kuripua bomu katika mkutano huo.
Tarehe 24 Oktoba miaka 94 iliyopita ulianza mgogoro mkubwa wa kiuchumi wa Marekani unaojulikana kwa jina la Wall Street.
Kimsingi Wall Street ni mtaa mashuhuri mjini New York ambao kutokana na kuwa na taasisi nyingi kubwa za kifedha na kibenki unatambuliwa kuwa kituo muhimu sana cha kiuchumi cha Marekani. Kituo hicho cha kiuchumi kilikumbwa na mgogoro mkubwa wa kifedha wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia na baada yake.
Oktoba 24 mwaka 1929 janga kubwa la kifedha liligubika makao ya hisa ya Marekani huko Wall Street na kupelekea kukosa kazi zaidi ya wafanyakazi milioni 13 wa Marekani, njaa kali, kufilisika kwa viwanda na mabenki na mamilioni ya watu kupoteza makazi na nyumba zao.

Katika siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, uliundwa Umoja wa Mataifa na kuchukua nafasi ya Jumuiya ya Mataifa.
Wawakilishi wa mataifa yaliyoafikiana katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, yaani Marekani, Urusi, Uingereza na Ufaransa, waliandaa mazingira ya kuundwa umoja huo; na hatimaye katika mkutano uliofanyika San Francisco, Marekani, wawakilishi kutoka nchi 50 duniani walipitisha sheria za kuundwa umoja huo.
Ijapokuwa umoja huo umefanikiwa katika baadhi ya mambo, lakini kuwepo haki ya veto kwa baadhi ya nchi ambazo ni Marekani, Russia, Uingereza, Ufaransa, na China kunalifanya Baraza la Usalama la umoja huo kufuata kibubusa siasa za nchi zenye haki ya kupiga kura ya turufu, na hasa Marekani.
Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, Iran ilifanikiwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa hati ya Umoja wa Mataifa, mlango wa kujiunga na umoja huo uko wazi kwa mataifa yote yanayopenda amani na ambayo yanakubaliana na sheria na maaamuzi ya taasisi hiyo.
Nchini Iran, Umoja wa Mataifa una jumla ya ofisi 14 za uwakilishi na utendaji. ***
Na miaka 50 iliyopita katika siku kama ya leo, vita vya nne baina ya Waarabu na Israel vilivyojulikana kwa jina la Vita vya Ramadhani vilifikia tamati.
Tarehe 6 Oktoba 1973 Anwar Sadat Rais wa wakati huo wa Misri akiwa na lengo la kufidia kushindwa katika vita vya Waarabu na Israel mwaka 1967, alifanya mashambulio ya kushtukiza katika ngome za Israel katika Mfereji wa Suez.
Muda mchache baada ya mashambulio hayo, wanajeshi wa Syria nao walifanya mashambulio katika miinuko ya Golan ambayo ilikaliwa kwa mabavu na Israel katika vita vya mwaka 1967 na kufanikiwa kuwatimua wanajeshi wote wa utawala huo haramu kutoka katika maeneo waliokuwa wakiyadhibiti.
