Oct 24, 2023 23:22 UTC
  • Jumatano, Oktoba 25, mwaka 2023

Leo ni Jumatano tarehe 9 Mfunguo Siba Rabiuthani 1445 Hijria sawa na Oktoba 25 mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 312 iliyopita, mwanakijiji mmoja aligundua alama za awali za mabaki ya miji miwili ya kihistoria ya Pompeii na Herculaneum nchini Italia.

Mji wa Pompeii ulijengwa na kaumu ya Oscan mwanzoni mwa karne ya 6 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih (as) na ulikuwa na bandari maarufu na yenye ustawi mkubwa hadi karne ya kwanza baada ya kuzaliwa Nabii Issa (as).

Mji huo na ule wa Herculaneum ilizikwa na kufunikwa kikamilifu na volcano ya Mlima Vesuvius mwaka 79 Miladia.

Siku kama ya leo, miaka 212 iliyopita, alizaliwa Évariste Galois, mtaalamu wa hesabati wa nchini Ufaransa, karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, Paris.

Kufikia umri wa miaka 12, Galois hakufunzwa na mtu yeyote isipokuwa mama yake na alianza kusoma vitabu vya jiometri na hivyo kuinukia kielimu. Baada ya hapo alijiunga na chuo, ambapo alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani katika kila somo.

Baadaye Évariste Galois alianza kutalii elimu ya hisabati. Akiwa na umri wa miaka 18 alikamilisha kazi ya uandishi wa kitabu cha hisabati na baada ya hapo akaandika vitabu vitatu vipya katika taaluma hiyo na kujipatia umashuhuri mkubwa.  Galois aliuawa  akiwa na umri wa miaka 21 hapo tarehe 29 mwezi Mei mwaka 1832 baada ya kutiwa jela wakati wa harakati zake za kisiasa nchini Ufaransa.

Weledi wanaamini kuwa, kama Galois hangeuawa mapema, basi angepiga hatua kubwa katika uga wa hisabati duniani. 

Évariste Galois

Siku kama ya leo miaka 142 iliyopita, alizaliwa Pablo Picasso mchoraji mashuhuri wa Kihispania.

Picasso alikuwa mwasisi wa harakati ya Cubist ambayo ilienea kwa kasi kubwa miongoni mwa wachoraji wa Ufaransa. Pablo Picasso alichora picha nyingi na daima alikuwa akifanya juhudi za kuendeleza harakati hiyo.

Mchoro wa 'The Girls of Avignon' wa mchoraji huyo ndio uliokuwa mwanzo wa mtindo wa Cubism na kazi kubwa zaidi ya Picasso katika mtindo huo ni 'Guernica'. Katika mchoro huo Pablo Picasso anaonesha hofu iliyompata kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na ndege za kivita za Ujerumani na Italia dhidi ya mji wa Guernica.

Picasso alifariki dunia Aprili mwaka 1973. 

Pablo Picasso

Siku kama ya leo miaka 141 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Haj Mirza Abdul Rahim Nahavandi, alimu na msomi mkubwa wa sheria za Kiislamu.

Ayatullah Nahavandi alibobea katika elimu ya fiqhi na usulu fiqhi, na kutokana na hali hiyo wasomi wengi wa Iraq na Iran waliweza kustafidi na elimu yake.

Inafaa kufahamisha kwamba, Ayatullah Haj Mirza Abdul Rahim Nahavandi, alizaliwa katika mji wa Nahavand, ulio magharibi mwa Iran na akiwa kijana alielekea mjini Najaf, Iraq na kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo hususan Sheikh Murtadha Answari, ambapo kwa kipindi cha miaka 30 alijikita katika shughuli ya ufundishaji wa sheria za Kiislamu.

Katika siku kama hii ya leo miaka 141 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 58, Ayatullah Sayyid Haidar Hilli.

Abul-Hassan Sayyid Haidar Bin Sulaiman bin Daud Hilli Husseini, ni miongoni mwa malenga na viongozi mashuhuri wa fani hiyo katika zama hizo. Ufasaha na uwezo mkubwa wa kiimani aliokuwa nao, vilimsukuma katika kuwasifu Ahlu Baiti wa Mtume (saw) kupitia mashairi yake.

Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu cha 'ad-Duraru-Yatim' na 'al-Aqdul-Mufaswal.'   

Na katika siku kama ya leo miaka 31 iliyopita aliaga dunia Abul Qassim Halat mshairi, mchekeshaji na mtarjumi wa zama hizi wa Kiirani.

Alianza kutunga mashairi akiwa na umri wa miaka 16 na akaondokea kubobea katika mashairi ya vichekesho. Malengo huyo alikuwa akizifahamu vyema lugha za Kifarsi, Kiingereza, Kifaransa na Kiarabu.

Miongoni mwa athari zake muhimu ni tarjama ya maneno yenye thamani kubwa ya Bwana Mtume (saw) na Imam Ali bin Abi Talib (as). Abul Qassim Halat ameacha athari nyingi zenye thamani kubwa katika uga wa maishairi. 

Abul Qassim Halat