Ijumaa, tarehe 27 Oktoba, 2023
Leo ni Ijumaa tarehe 11 Rabiuthani 1445 Hijria, sawa na 27 Oktoba 2023.
Siku kama ya leo miaka 1225 iliyopita, alifariki dunia Abu Ali Khayyat, mnajimu na mtaalamu wa hesabati wa Kiislamu.
Abu Ali ni mmoja wa shakhsia aliyekuwa na nafasi kubwa wakati wake huku jina lake likiwekwa mstari wa mbele katika kitabu cha majina ya wasomi wakubwa na mashuhuri wa dunia.
Msomi huyo ameandika vitabu vingi maarufu zaidi kikiwa ni kitabu cha 'Mawaalid' na 'Siyarul-A'amaal.' Vitabu vingi vya Abu Ali Khayyat vimetarjumiwa kwa lugha ya Kilatini.

Siku kama ya leo miaka 837 iliyopita, alizawa mjini Mosul, moja ya miji mashuhuri ya Iraq, Ibn Khallikan, kadhi, mwanahistoria na mtaalamu wa fasihi wa Kiislamu.
Akiwa kijana alisoma elimu za awali katika mji alikozaliwa na kisha kufanya safari mbalimbali na kukutana na wanasheria wa Kiislamu na wanahistoria wakubwa sanjari na kustafidi na elimu kutoka kwao.
Kwa muda mrefu Ibn Khallikan alikuwa kadhi mjini Damascus, Syria ya leo huku akiwa mtaalamu pia katika elimu za historia, fasihi ya Kiarabu na mashairi. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwezi wa Rajab mwaka 681 Hijiria baada ya kuugua na kuzikwa chini ya mlima Qasioun ulio Damascus ambako pia wamezikwa wasomi wengi.
Kitabu muhimu zaidi cha Ibn Khallekan ni Wafayatul A'yan.
Siku kama ya leo miaka 118 iliyopita, nchi ya Norway ilivunja muungano wake na Sweden na kujitangazia uhuru.
Kabla ya karne ya 14 Norway ilikuwa nchi yenye ushawishi na moja ya madola vamizi.
Hata hivyo mnamo mwaka 1380 ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Denmark na kuendelea kuwa chini ya udhibiti wa nchi hiyo kwa muda wa karne 4.
Katika siku kama ya leo miaka 113 iliyopita, baada ya Japan kupigana vita na nchi mbili za China na Russia kwa miaka kadhaa na kupata ushindi katika vita hivyo, iliunganisha rasmi ardhi ya Korea na ardhi yake.
Korea iliendelea kuwa chini ya udhibiti wa Japan hadi mwaka 1945 wakati Japan iliposhindwa katika Vita vya Pili vya Dunia.

Katika siku kama ya leo miaka 65 iliyopita katika siku kama ya leo, Jenerali Muhammad Ayub Khan alifanya mapinduzi nchini Pakistan na kushika hatamu za uongozi wa nchi hiyo.
Tukio hilo lilitokea miaka 11 baada ya Pakistan kupata uhuru, ambapo Jenerali Muhammad Ayub Khan aliyekuwa mmoja wa makamanda wa jeshi alichukua hatamu za uongozi baada ya kufanya mapinduzi ambayo hayakuwa na umwagaji damu.
Kufuatia mapinduzi hayo, Iskander Mirza aliyekuwa Rais wa kwanza wa Pakistan akalazimika kuondoka madarakani. Baada ya mapinduzi hayo, Muhammad Ayub Khan ambaye alichukua nyadhifa za Urais na Waziri Mkuu alitangaza serikali ya kijeshi nchini humo.
Hata kama baada ya miaka 7 Ayub Khan aliibuka mshindi katika uchaguzi wa Rais uliofanyika nchini humo mwaka 1965, lakini alianza kukabiliwa na mashinikizo baada ya kuongezeka matatizo ya kiuchumi na kisiasa.
Hatimaye mwaka 1969, Ayub Khan aliachia ngazi na kukabidhi uongozi wa nchi kwa Jenerali Yahya Khan aliyekuwa mkwewe.
Na siku kama ya leo miaka 50 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Zanjani, alimu mkubwa na mtaalamu wa elimu ya fiqhi.
Ayatullah Zanjani alizaliwa mwaka 1308 Hijiria, huku akisomea elimu ya awali na ya juu mjini Zanjan. Baada ya hapo alielekea mjini Qum kwa ajili ya kuendelea na elimu ambapo alipata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Abdul-Karim Haeri Yazdi na Muhammad Hujjat Kuh-Kamari. Baada ya Ayatullah Muhammad Hujjat kufariki dunia, Ayatullah Sayyid Ahmad Zanjani alichukua wadhifa wa kuswalisha swala ya jamaa katika shule ya Fayzia.
Aidha katika muongo wa 1320 Hijiria Shamsia, msomi huyo alikutana na Imam Khomeini (MA) ambapo alishirikiana naye katika vikao vingi vya kielimu. Vitabu kama vime 'Arbain' 'Afwahur-Rijal' 'Furuqul-Ahkaam' na vitabu 20 vingine ni sehemu ya turathi za Ayatullah Sayyid Ahmad Zanjani.