Jumapili, 29 Oktoba, 2023
Leo ni Jumapili tarehe 13 Mfunguo Saba Rabiuthani 1445 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 29 Oktoba 2023 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1226 iliyopita yaani tarehe 13 Rabiuthani mwaka 218 Hijria aliaga dunia Ibn Hisham msomi na mwanahistoria mkubwa wa Kiarabu. Ibn Hisham alizaliwa Basra nchini Iraq na alibobea katika elimu na fasihi na utungaji mashairi. Alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufanya uchunguzi kuhusu maisha ya Nabii Muhammad (saw). Umashuhuri mkubwa wa Ibn Hisham unatokana na kitabu chake cha al Sira al Nabawiyya ambacho ni miongoni mwa marejeo muhimu kuhusu maisha ya Mtume Muhammad (saw). ***
Katika siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, mfumo wa utawala wa serikali ya jamhuri uliasisiwa nchini Uturuki kwa uongozi wa Mustafa Kemal Pasha mashuhuri kwa jina la Ataturk. Kemal Ataturk aliiongoza kidikteta nchi hiyo kwa muda wa miaka 15 na kufanya hujuma za kufuta sheria, nembo pamoja na matukufu ya Kiislamu na wakati huo huo, kueneza utamaduni na nembo za Kimagharibi nchini humo. Hata baada ya kufariki dunia kiongozi huyo aliyekuwa na uadui na Uislamu mnamo mwaka 1938, njama hizo dhidi ya Uislamu nchini Uturuki ziliendelezwa na wafuasi wake. ***
Miaka 97 iliyopita yaani tarehe 7 Aban mwaka 1305 Hijria Shamsia Ayatualha Sayyid Hassan Modarres aliyekuwa miongoni mwa wanazuoni na wanamapambano maarufu nchini Iran alinusurika jaribio la kuuawa. Jaribio hilo lilifanywa na vibaraka wa Shah Reza Pahlavi aliyekuwa maarufu kwa udikteta, ukatili na upinzani mkubwa dhidi ya maulama wa Kiislamu. Uhasama wa utawala wa kifalme wa Pahlavi dhidi ya Ayatullah Modarres ulitokana na mchango mkubwa wa mwanazuoni huyo wa Kiislamu katika kuwaamsha wananchi na kufichua njama za utawala wa Kipahlavi na muungaji mkono wake yaani serikali ya Uingereza. Kwa kipindi fulani Ayatullah Modarres alikuwa mwakilishi wa wananchi wa Tehran katika Bunge. Baada ya kunusurika kifo Ayatullah Modarres alipelekwa uhamishoni kwa amri ya mfalme dikteta Reza Khan na muda mfupi baadaye aliuawa shahidi na vibaraka wa Shah. ***
Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, katika jinai yao nyingine, Wazayuni waliwauwa kwa umati wakazi wa kijiji cha Kafr Qasim huko Palestina. Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni walitangaza utawala wa kijeshi katika kijiji hicho. Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni waliwauwa kwa umati wanawaume, wanawake na watoto madhlumu wa Palestina wasiopungua 49 na kujeruhi makumi ya wengine huko Kafr Qasim. ***
Katika siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, askari jeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walishambulia Peninsula ya Sinai iliyoko Misri. Mashambulio hayo yalianza baada ya Rais wa wakati huo wa Misri, Gamal Abdul Nassir kutaifisha mfereji wa Suez. Siku mbili baada ya mashambulio hayo, Uingereza na Ufaransa zilipeleka majeshi yao pembezoni mwa mfereji huo kwa lengo la kuusaidia utawala ghasibu wa Israel. Mnamo mwaka 1957 majeshi vamizi ya Ufaransa, Uingereza na utawala haramu wa Israel yaliondoka katika ardhi ya Misri kufuatia mashinikizo ya fikra za waliowengi, madola mengi ya Magharibi na upatanishi wa Umoja wa Mataifa. ***