Ijumaa, tarehe Tatu Novemba, 2023
Leo ni Ijumaa tarehe 18 Rabiuthani 1445 Hijiria, sawa na tarehe 3 Novemba 2023.
Katika siku kama ya leo miaka 843 iliyopita alizaliwa Muhaqiq Hilli, Abul Qasim Ja'far bin Hassan, mmoja wa wanazuoni wakubwa na faqihi ya Kiislamu katika mji mashuhuri wa Hillah nchini Iraq.
Muhaqiq Hilli alikuwa msomi aliyekuwa na nafasi ya juu na mtaalamu wa sheria za Kiislamu na alibobea pia katika fasihi na uandishi wa mashairi.
Baada ya kukamilisha masomo ya awali na kukwea daraja za juu za kiroho, alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa zama zake. Kitabu muhimu zaidi cha Muhaqqiq al Hilli ni Sharaiu'l Islam fii Masaailil-Halal Wal-haraam'. Mwanazuoni huyo pia ameandika vitabu vya "Nafi', Ma'arij na Tanbih".
Muhaqqiq al Hilli alifariki dunia mwaka 676 Hijria akiwa na umri wa miaka 74.
Siku kama ya leo miaka 120 iliyopita, nchi ya Panama ilifanikiwa kujipatia uhuru wake kutoka Colombia na siku hii huadhimishwa nchini humo kama siku ya taifa.
Ardhi ya Panama iligunduliwa na kukaliwa kwa mabavu na Wahispania mnamo mwaka 1501 Miladia. Panama ilikaliwa kwa mabavu na Colombia mwaka 1821 Miladia na tangu wakati huo wananchi wa nchi hiyo walianzisha mapambano dhidi ya wavamizi wa Colombia.
Mapambano hayo ya wananchi yalishadidi zaidi baada ya kuwasilishwa mpango wa mfereji wa Panama. Mwaka 1903, Panama ikafanikiwa kujitenga na Colombia na kujitawala.
Siku kama ya leo miaka 115 iliyopita alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 93 Ayatulla Mirza Hussein Husseini, maarufu kwa jina la Mirza Khalil, msomi mkubwa na mwanamapambano.
Ayatulla Mirza Hussein Husseini alizaliwa yapata mwaka 1230 Hijiria katika mji wa Najaf mashariki, nchini Iraq. Msomi huyo mkuwa baada ya kuhitimu masomo ya awali na ya kati kwa baba na kaka yake, alipata pia kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Muhammad Hasan al-Najafi na Sheikh Morteza Ansari na kufikia daraja ya umarjaa wa Kishia. Hadhi ya umarjaa aliipata baada ya kufariki dunia Sayyid Mirza Bozorq Shirazi ambapo Waislamu wa Shia kutoka Iran, Iraq, Lebanon, India na maeneo mengine ya Waislamu walikuwa wakirejea kwake kiasi cha kufikia kumpa jina la Mkuu wa Hauza ya Kielimu ya Najaf.
Kwa muda wote Ayatulla Mirza Hussein Husseini Khalil alijishughulisha na kazi ya kufundisha elimu ya fiqhi ambapo aliweza kulea makumi ya wanafunzi katika uwanja huo. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na 'Kitabun- fil Ijaazah' 'Kitabun fil-Ghasbi' na 'Sharhu Najaatul-Ibaad.'

Miaka 67 iliyopita muwafaka na siku kama hii ya leo, wakati wa kujiri mashambulio ya askari wa utawala dhalimu wa Israel dhidi ya Misri, wanajeshi wa utawala huo waliuvamia mji wa Khan Yunis katika Ukanda wa Gaza huko Palestina na kuwaua kwa umati wakazi wa mji huo.
Baada ya kuukalia kwa mabavu mji huo, askari hao waliwanyonga askari 25 wa Kimisri. Unyama wa askari hao haukuishia hapo, kwani waliishambulia hospitali ya mkoa mjini Khan Yunis na kuwaua kwa umati wauguzi, madaktari na wagonjwa wote waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo.
Watu wapatao 275 waliuawa katika mashambulio hayo.
Na siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, alifariki dunia Jenerali Jean-Bedel Bokassa mtawala wa Afrika ya Kati. Bokassa alichukua madaraka mwaka 1921 kupitia mapinduzi ya kijeshi, baada ya kuiondoa madarakani serikali ya Rais David Dacko kwa uungaji mkono wa Ufaransa. Katika miaka 14 ya utawala wake, kiongozi huyo alitenda jinai na mauaji mbalimbali na kujilimbikizia mali nyingi.