Nov 05, 2023 23:28 UTC
  • Jumatatu tarehe 6 Novemba 2023

Leo ni Jumatatu tarehe 21 Rabiuthani 1445 Hijria sawa na tarehe 6 Novemba 2023.

Miaka 391 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa Gustav wa Pili, mfalme wa Sweden.

Alizaliwa mwaka 1594 na alikalia kiti cha ufalme alipokuwa na umri wa miaka 17.

Umaarufu wake ulitokana na kushinda kwake katika vita vya kidini vya miaka 30 kati ya Waprotestant na Wakatoliki vya mwaka 1618 hadi 1648. 

Gustav wa Pili

Siku kama ya leo miaka 210 iliyopita vita vya kwanza vya Simon Bolivar, shujaa wa uhuru wa mataifa ya Amerika ya Latini vya kukomboa nchi ya Venezuela kutoka kwa wakoloni wa Kihispania vilimalizika kwa ushindi.

Katika vita hivyo askari 6500 wa Simon Bolivar waliwashinda askari elfu 13 wa Uhispania. Hatimaye shujaa huyo wa Amerika ya Latini aliikomboa Venezuela kutoka utawala wa kikoloni wa Uhispania na kisha akashiriki katika mapambano ya kupigania uhuru ya nchi nyingine kadhaa za kusini mwa Amerika.   

Simon Bolivar

Miaka 163 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 6 Novemba 1860 Abraham Lincoln aliyekuwa mpinzani wa utumwa nchini Marekani, alishika madaraka na kuwa rais wa nchi hiyo. Katika kipindi cha uongozi wake vita kadhaa vilitokea nchini Marekani na kupelekea kushindwa waliokuwa wakiunga mkono utumwa.

Abraham Lincoln aliuawa mwaka 1865 na mmoja wa wapinzani wa harakati za kupinga utumwa nchini Marekani. 

Simon Bolivar

Na siku kama ya leo miaka 45 iliyopita wafanyakazi wa redio na televisheni ya Iran walianza mgomo wakipinga utawala wa Shah.

Mgomo huo ulifanyika kwa shabaha ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya utawala wa Shah na kuharakisha mwenendo wa kuipindua serikali yake. Siku hiyo hiyo maafisa wa jeshi la Shah walishambulia taasisi za magazeti na vyombo vya habari na kuwatia nguvuni waandishi kadhaa.

Hatua hiyo ilipelekea kusitishwa uchapishaji wa magazeti yaliyokuwa yakichapishwa kwa wingi nchini.