Nov 10, 2023 04:20 UTC
  • Ijumaa, tarehe 10 Novemba, 2023

Leo ni Ijuumaa tarehe 25 Mfunguo Saba Rabiuthani 1445 Hijria sawa na Novemba 10 mwaka 2023.

Mwaka 288 Hijria katika siku kama ya leo, alifariki dunia Thabit bin Qurrah Swabi, mtaalamu wa hisabati, nyota na tabibu katika kipindi cha utawala wa Bani Abbas.

Alizaliwa mwaka 221 Hijria mjini Harran uliopo eneo la Mesopotamia nchini Iraq. Thabit bin Qurrah Swabi alikuwa akizungumza lugha za Kigiriki, Kisiriyan na Kiarabu. Alisafiri kwenda mjini Baghdad, Iraq kwa lengo la kusoma na kwa usimamizi wa Muhammad bin Mussa aliyekuwa mtaalamu mkubwa Mwislamu wa hisabati na nyota kipindi hicho, Thabit bin Qurrah Swabi akaingia katika uwanja wa elimu hizo. Alibuni nadharia mpya katika uwanja wa hisabati. Aidha katika utaalamu wa nyota yeye ni katika watu wa kwanza kurekebisha chombo cha Ptolemaic.

Thabit bin Qurrah Swabi aliandika vitabu vingi katika uwanja wa tiba, hisabati na nyota, vilivyofasiriwa kutoka lugha ya Kigiriki kwenda Kiarabu. Miongoni mwa vitabu hivyo ni pamoja na kile kiitwacho "Adh Dhakhiratu fii Ilmi al Twib" na "Kitabul Mafrudhaat." 

Thabit bin Qurrah Swabi

Miaka 1077 iliyopita mwaka 368 Hijiria, alizaliwa mjini (Corduba, Qurtuba) Uhispania, faqihi, mtaalamu wa hadithi, fasihi na mwanahistoria Abu Omar Yusuf bin Abdallah mashuhuri kwa jina la Abdul Birr.

Alipata masomo ya msingi kutoka kwa baba yake na walimu wengine wakubwa wa kipindi hicho. Ibnu Abdul Birr aliupa umuhimu mkubwa utafiti, ambapo kwa kipindi cha muda mfupi alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa mjini Andalusia. Kufuatia kukosekana amani na usalama katika mji wa Corduba, Ibn Abdul Birr alilazimika kuhamia mji mwingine wa Daynah ambao kipindi hicho ulikuwa moja ya vituo muhimu vya elimu vya Andalusia, na huko alifanikiwa kuandika vitabu vyake.

Miongoni mwa athari za msomi huyu mashuhuri ni kitabu cha "al Istiiab" ambacho kinahusu maisha ya masahaba wa Mtukufu Mtume Muhammad (saw). 

Miaka 540 iliyopita muwafaka na leo, alizaliwa Martin Luther, mpigania mageuzi ya kidini wa Kijerumani.

Luther alikuwa padri wakati akiwa kijana. Mitazamo ya Martin Luther kuhusiana na dini ya Kikristo ilitofautiana na baadhi ya mitazamo ya Papa na viongozi wa ngazi ya juu wa Kanisa na kuanzia mwaka 1517, Luther alidhihirisha mapambano na upinzani wake dhidi ya dhulma na ukandamizaji wa Kanisa Katoliki.

Martin Luther alipinga waziwazi agizo la Papa wa Kanisa Katoliki na akaifasiri Injili kwa lugha ya Kijerumani. Baada ya hapo aliaanzisha harakati ya kiprotestanti dhidi ya kanisa hilo.

Martin Luther

Siku kama ya leo miaka 224 iliyopita yaani tarehe 10 Novemba mwaka 1899, kulitokea mapinduzi ya kijeshi yaliyofahamika kwa jina la Brumaire nchini Ufaransa.

Brumaire lilikuwa jina la mwezi wa pili katika kalenda ya mapinduzi ya Ufaransa ambao unaenda sambamba na mwezi wa Novemba kwa kalenda ya Milaadia. Siku hiyo Napolione Luis Banaparte ambaye alikuwa katika jitihada a kuteka na kukalia nchi za kaskazini mwa Afrika, alirejea kwa siri nchini Ufaransa kufuatia mwaliko wa kiongozi mmoja wa utawala wa nchi hiyo.

Luis Banaparte alifanikiwa kupindua utawala uliokuwepo nchini Ufaransa kwa kutegemea uungaji mkono wa askari jeshi na Bunge la nchi hiyo na kuanza kuiongoza rasmi Ufaransa. 

Napolione Banaparte

Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita yaani tarehe 10 Novemba 1912, Morocco alianza kukoloniwa na Ufaransa na Uhispania. Kabla ya hapo nchi hiyo inayopatikana kaskazini mwa Afrika ilikuwa ikikaliwa na madola mbalimbali kama vile dola la Othmania, Roma na Italia. Baadaye Uhispania na Ufaransa zilianza kukosana, na muungano wao katika kuikoloni Morocco ukavunjika.

Ufaransa iliendelea kuikoloni nchi hiyo na baada ya muda usio mrefu, wananchi wakaanzisha mapambano dhidi ya Wafaransa. Hatimaye mapambana hayo yalipata ushindi na Morocco ikajipatia uhuru 1956.   

Bendera ya Morocco

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita Dakta Sayyid Hussein Fatimi, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Dakta Muhammad Musaddiq, aliuawa kwa kupigwa risasi na vibaraka wa utawala wa Shah nchini Iran.

Dakta Fatimi kabla ya hapo alikuwa amehukumiwa kunyongwa na mahakama moja ya kijeshi ya kimaonyesho ya utawala wa Shah huku akiwa mgonjwa sana. Baada ya mapinduzi yaliyofanywa na Marekani tarehe 28 Mordad mwaka 1332 Hijria Shamsiya hapa nchini Iran na baada ya kujiuzulu Dakta Musaddiq, Dakta Sayyid Hussein Fatimi alikuwa akisakwa na vibaraka wa utawala wa Shah na alikuwa akiishi mafichoni. Alikamatwa na kunyongwa katika siku kama ya leo.   

Dakta Sayyid Hussein Fatimi akiwa katika mahakama ya kijeshi

Miaka 59 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 10 Novemba 1964, Leonid Brezhnev alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha CPSU katika Urusi ya zamani na hivyo kuchukua rasmi jukumu la kukiongoza chama hicho. Brezhnev aliendelea kushikilia cheo hicho cha ukatibu mkuu hadi kifo chake mwaka 1982. Katika kipindi chake cha uongozi, Umoja wa Kisovieti ulipata nguvu zaidi kijeshi lakini pia ulikumbwa na matatizo mengi ya kiuchumi.

Viongozi wa kikomunisti waliokuja baada yake walisema matatizo aliyoyaacha Leonid Brezhnev ndiyo yaliyosababisha kuporomoka na kuvunjika kabisa Umoja wa Kisovieti mwaka 1991.

Leonid Brezhnev

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio nambari 3379 lililoutambua Uzayuni (Zionism) kuwa ni aina fulani ya ubaguzi wa kizazi.

Azimio hilo lilitoa pigo kubwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na kufichua utambulisho halisi wa utawala huo. Azimio hilo la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliikasirisha sana Israel na waungaji mkono wa utawala huo wa kibaguzi hususan Marekani. Tofauti na mafundisho ya Kiyahudi, fikra za Uzayuni ambazo zilianzishwa mwishoni mwa karne ya 19 zinawatambua wafuasi wa dini hiyo kuwa ni ndio kizazi bora zaidi ya wengine wote duniani.

Kwa mujibu wa fikra hiyo Wazayuni wa Israel wanawatambua watu wa Palestina kuwa ni kizazi duni na hakiri zaidi na kwa sababu hiyo wanawakandamiza, kuwaua na kuwafukuza katika makazi na nchi yao.   

صهیونیسم

Na tarehe 10 Novemba mwaka 1981 wakati wa vita vya Saddam Hussein dhidi ya Iran, Ufaransa na Iraq zilitiliana saini mkataba wa mauzo ya silaha uliokuwa na thamani ya dola bilioni moja. Mkataba huo ulikuwa moja kati ya mikataba kadhaa ya mauzo ya silaha baina ya Ufaransa na utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq wakati wa mashambulizi ya Iraq dhidi ya Iran.

Ufaransa ilikuwa bega kwa bega na utawala wa Saddam Hussein tangu mwanzoni mwa mashambulizi na uvamizi wa Iraq dhidi ya Iran na ilihesabiwa kuwa muuzaji mkubwa wa pili wa silaha kwa utawala wa dikteta Saddam Hussein baada ya Russia. Silaha hizo zilijumuisha ndege za kisasa za kivita, makombora ya aina mbalimbali, vifaru, mizinga na aina nyingine za zana za kivita. Ufaransa pia ilimsaidia Saddam Hussein katika kutengeneza silaha za kemikali.

Vilevile iliupatia utawala wa Iraq mkopo wa dola bilioni 5 wakati wa vita vyake dhidi ya Iran na imekataa kulipa deni la dola bilioni moja kwa Iran.