Nov 16, 2023 00:40 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 16 Novemba, 2023

Leo ni Alkhamisi tarehe Pili Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 16 Novemba 2023.

Siku kama ya leo miaka 1054 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia malenga wa Kiirani, Abu Is'haq Kesa-i Marvazi.

Kipindi cha ujana wake kiliambatana na kumalizika kwa kipindi cha utawala wa Wasamani na mwanzoni mwa zama za utawala wa Waghaznavi. Kwa sababu hiyo malenga huyu Mfarsi alitunga mashairi kadhaa ya kusifu tawala hizo mbili. Fauka ya hayo Marvazi alitunga beti kadhaa za mashairi ya kumsifu Mtume Muhammad na (SAW) na kizazi chake hasahasa Imam Ali bin Abi Twalib (as).

Kesa-i Marvazi mbali na kusifika kwa utunzi wa mashairi, lakini pia alitoa waadhi na hekima kupitia mashairi yake ya Kifarsi. Malenga huyu mkubwa wa Kiirani ameandika ya mashairi. 

Abu Is'haq Kesa-i Marvazi

Miaka 43 iliyopita katika siku kama leo mji wa mpakani wa Susangerd huko kusini magharibi mwa Iran ulishuhudia mapambano kati ya wapiganaji wa Kiislamu na wanajeshi vamizi wa utawala wa zamani wa Iraq.

Oparesheni hiyo ya kujihami ilifanywa na wapiganaji shupavu 200 wa Iran waliojumuisha wanajeshi wa ulinzi, wanamgambo wa kujitolea na idadi ya kadhaa ya wenyeji wa mji huo waliokuwa wakitumia silaha nyepesi dhidi ya jeshi vamizi la Saddam.

Katika operesheni hiyo wapiganaji shupavu wa Iran chini ya uongozi wa shahidi Dakta Mustafa Chamran, walipambana vikali na kufanikiwa kuukomboa mji wa Susangerd.  

Ramani ya eneo la Susangerd

Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, Allama Muhammad Taqi Ja'fari, mwanafalsafa na mwanafikra mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia.

Alizaliwa mwaka 1304 Hijria Shamsia katika mji wa Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran. Kipaji chake kilidhihiri na kuchomoza tangu akiwa katika kipindi cha kuinukia kwake ambapo kabla ya kuanza shule ya msingi tayari alikuwa amejifunza Qur'ani. Akiwa shule alionekana mwenye kipaji mno. Hata hivyo umasikini ulimfanya aache shule na kuanza kufanya kazi.

Pamoja na kufanya kazi aliutumia muda wake wa ziada kusoma masomo ya dini. Allama Muhammad Taqi Ja'fari ameandika vitabu vingi ambapo Tarjuma na Tafsiri ya Nahajul Balagha ndio kitabu muhimu zaidi cha mwanazuoni huyo.

Allama Muhammad Taqi Ja'fari

Na miaka 23 iliyopita sawa na tarehe 25 Aban 1379 Hijria Shamsia, aliaga dunia Hujjatul Islam, Dakta Muhammad Hadi Amini Najafi, mmoja wa maulama na waandishi mahiri wa Kiirani.

Alizaliwa Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran, na katika kipindi cha ujana wake alielekea huko Najaf, Iraq akiwa pamoja na baba yake, Allama Amini, mwandishi wa kitabu mashuhuri cha al-Ghadir. Msomi huyo alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar nchini Misri.

Mwaka 1350 Hijria Shamsia Dakta Muhammad Hadi Amini Najafi alirejea nchini Iran na kuanza kufanya kazi ya uandishi, kufundisha na kufanya uhakiki. 

Dakta Muhammad Hadi Amini Najafi