Nov 16, 2023 23:47 UTC
  • Ijumaa, tarehe 17 Novemba, 2023

Leo ni Ijumaa tarehe 3 Jamadil Awwal 1445 Hijria sawa na Novemba 17 mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 306 iliyopita, Jean le Rond d'Alembert mwanahisabati wa Kifaransa alizaliwa katika mji wa Paris huko Ufaransa.

Baba na mama yake walimtelekeza kando ya kanisa moja mjini Paris akiwa mtoto mchanga. Aliokotwa na kulelewa na mwanamke na mwanaume mmoja waliokuwa wauza vioo. Jean le Rond d'Alembert alisoma kwa bidii na baada ya kuhitimu masomo ya kati alianza kusoma taaluma ya tiba na sheria. Hata hivyo baada ya muda aliondokea kuipenda mno taaluma ya hisabati ambapo alifanya utafiti mkubwa katika uwanja huo. Alipotimiza umri wa miaka 22 d'Alembert alizindua makala kuhusiana na hesabu, makala ambayo yalimpatia umashuhuri mkubwa.

Ameacha athari mbalimbali ambazo zipo katika maktaba za Ufaransa. Jean le Rond d'Alembert alifariki dunia tarehe 29 Oktoba 1783 akiwa na umri wa miaka 66.  

Jean le Rond d'Alembert

Siku kama ya leo miaka 227 iliyopita, Catherine The Great malkia mashuhuri wa Russia aliaga dunia.

Alizaliwa Mei Pili 1729 na akiwa na umri wa miaka 15 aliolewa na Peter III. Hata hivyo Peter III mfalme wa wakati huo wa Russia hakuwa akimpenda mkewe huyo na alikuwa akimvunjia heshima na kumdhalilisha mbele za watu.

Mwaka 1762 wakati Peter III alipokuwa ametoka nje ya mji, Catherine the Great alijitangaza kuwa malkia wa Russia. Peter III ambaye alishtushwa na kupata pigo kwa hatua hiyo alilazimika kujiuzulu pasina ya mapambano na baada ya siku chache akaaga dunia.   

Catherine The Great

Siku kama ya leo miaka 165 iliyopita, Robert Owen mpigania mageuzi ya kisoshalisti wa Wales na mmoja wa waasisi wa Harakati ya Usoshalisti aliaga dunia.

Alianza harakati zake tangu akiwa na umri wa miaka 18 sambamba na kujenga kiwanda cha ufumaji. Katika kiwanda chake hicho kwa mara ya kwanza alianza kuboresha hali ya afya na ustawi wa wafanyakazi barani Ulaya kwa kupunguza masaa ya kazi kutoka masaa 14 kufikia masaa 10.  

Robert Owen

Katika siku kama ya leo miaka 154 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 17 Novemba mwaka 1869, Mfereji wa Suez unaounganisha Bahari ya Mediterania na Bahari Nyekundu ulifunguliwa.

Uchimbaji wa mfereji huo ulisimamiwa na mhandisi wa Kifaransa Ferdinand de Lesseps katika kipindi cha miaka 10 huku ukiwa na urefu wa kilomita 168 na upana wa mita 120 hadi 200.

Karne kadhaa kabla yake, Mfalme Daryush wa Iran na baadhi ya wafalme wa Misri walichukua hatua kadhaa za kuanzisha mfereji baina ya bahari hizo mbili, suala ambalo linaonyesha umuhimu wa Mfereji wa Suez unaopunguza kwa kiasi kikubwa masafa ya kutoka Asia kuelekea Ulaya, safari ambayo zamani ilikuwa ikifanyika kupitia Afrika Kusini.  

Ferdinand de Lesseps

Siku kama ya leo miaka 153 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abu Abdillah Sheikhul-Islam Zanjani, alimu na malenga aliyekuwa na uwezo mkubwa wa Waislamu. 

Alizaliwa mwaka 1224 Hijiria mjini Zanjan, moja ya miji ya Iran na akiwa kijana alielekea mjini Isfahan kwa ajili ya masomo. Akiwa mjini Isfahan alijiunga na chuo cha hauza ambacho kilikuwa moja ya vituo vyenye itibari katika elimu ya kidini wakati huo ambapo alifikia elimu ya juu na kisha kurejea nyumbani baada ya kuhitimu masomo yake. 

Sambamba na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji Ayatullah Mirza Abu Abdillah Sheikhul-Islam Zanjani, aliandika vitabu vingi ambavyo baadhi yake ni 'Hujjatul-Abraar' na 'Hidayatul-Muttaqin'.  

Siku kama ya leo miaka 108 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ismail Swadr, alimu na mujtahidi wa ngazi ya juu mjini Kadhimiya, Iraq. 

Alisoma masomo ya awali ya dini ya Kiislamu kwa kaka yake na kisha akaelekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi katika uwanja huo. Akiwa mjini Najaf alijifunza elimu ya sheria za Kiislamu (fiqhi), elimu ya akhlaq na elimu nyingine tofauti za kidini. 

Baada ya kufariki dunia mwalimu wake mkubwa Ayatullah Mirza Shirazi, Ayatullah Sayyid Ismail Swadr alichukua jukumu la ufundishaji mjini Karbala nchini humo.  

Sayyid Muhammad Baqir Sadr na kakka yake Ismail Sadr

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, ulianzishwa tena uhusiano wa kidiplomasia kati ya Iran na Libya.

Uhusiano huo ulikuwa umekatika kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Hilo lilitokana na hatua ya Kanali Muammar Gaddafi Kiongozi wa wakati huo wa Libya ambaye alikuwa akiutambua utawala wa kifalme wa Kipahlavi hapa nchini kuwa, ulikuwa ukifungamana na ubeberu wa Marekani ambao ulikuwa ukitanguliza mbele maslahi na manufaa ya Magharibi na utawala vamizi wa Israel mbele ya maslahi ya nchi za Kiarabu na Wapalestina.   

Na siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiislamu la Iraq liliasisiwa kutokana na vyama na makundi mbalimbali yaliyokuwa yakiupinga utawala wa dikteta Saddam Hussein.

Lengo la kuasisiwa baraza hilo lilikuwa ni kuwaokoa wananchi wa Iraq na dhulma pamoja na ukandamizaji wa utawala wa Chama cha Baath.

Kufuatia mashambulio ya kijeshi ya Marekani nchini Iraq na kuangushwa utawala dhalimu wa Saddam, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiislamu la Iraq, lilihamishia harakati zake za kisiasa ndani ya ardhi ya Iraq na kuwa na nafasi muhimu katika uwanja huo.