Jumanne, Novemba 21, 2023
Leo ni Jumanne tarehe 7 Jamadil Awwal 1445 Hijria sawa na Novemba 21 mwaka 2023.
Katika siku kama hii ya leo tarehe 7 Jamadil Awwal miaka 1056 iliyopita aliaga dunia qari na mtaalamu maarufu wa Hadithi Ibn Ghalbun. Msomi huyo wa Kiislamu alizaliwa mwaka 309 Hijria katika mji wa Halab (Aleppo) nchini Syria lakini akachaga maskani nchini Misri. Ibn Ghalbun alijifunza qira ya Qur'ani na Hadithi kwa wanazuoni wa zama zake na kuwa mwalimu mahiri katika taaluma hizo. Mtaalamu huyo wa Hadithi wa Kiislamu alikuwa ya mitazamo mipya kuhusiana na elimu ya qiraa ya Qur'ani tukufu ambayo imeelezwa na mwanafunzi wake, Makki bin Abu Twalib katika kitabu cha al Kashf. Vilevile alikuwa hodari na gwiji katika fasihi na mashairi ya lugha ya Kiarabu. Kitabu muhimu zaidi ya Ibn Ghalbun ni al Irshad kinachohusiana na visomo saba vya Qur'ani tukufu.

Miaka 240 iliyopita inayosadifiana na tarehe 21 Novemba mwaka 1783, kwa mara ya kwanza katika historia ya jitihada za mwanadamu za kupaa angani, puto lilitumwa angani. Puto hilo lilikuwa limepandwa na watu wawili mmoja akiwa mwanafizikia wa Ufaransa aliyejulikana kwa jina la Pilatre De Rozier. Tangu alipokuwa masomoni De Rozier alikuwa akifikiria kutengeneza wenzo wa kupaa angani na kwa kutengeneza puto hilo mwanafizikia huyo akawa amefanikiwa kuruka angani.
Miaka 59 iliyopita katika siku kama ya leo tarehe 7 Jamadil Awwal Sayyid Qutb msomi na mwanamapambano wa Misri alinyongwa pamoja na wenzake wawili huko Cairo mji mkuu wa nchi hiyo. Msomi huyo alihifadhi Qur'ani Tukufu katika ujana wake. Sayyid Qutb alifahamiana na Hassan al Bana na kujiunga na harakati ya Ikhwanul Muslimin ya nchi hiyo wakati alipokuwa katika harakati za kisiasa nchini Misri. Sayyid Qutb alitiwa nguvuni na baadaye kunyongwa baada ya kuzuka hitilafu kati ya Gamal Abdel Nasser Rais wa wakati huo wa Misri na Ikhwanul Muslimin. Sayyid Qutb alikuwa akiiamini kwamba "kambi za Mashariki na Magharibi zinapigana na Waislamu na kwamba kambi mbili hizo zimeungana ili kupora maliasili za nchi za Kiislamu". Miongoni mwa vitabu vya msomi na mwanamapamban huyo wa Kiislamu ni kile alichokipa jina la" Uislamu na Amani ya Kimataifa".
Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, Butros Butros Ghali alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa sita wa Umoja wa Mataifa. Butros Ghali alizaliwa mwaka 1922 katika familia ya Kikristo katika mji mkuu wa Misri Cairo. Baada ya kumaliza masomo yake Butros Butros Ghali alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Siasa cha Cairo. Mwanadiplomasia huyo ndiye aliyemshawishi na kumshajiisha Anwar Sadat, Rais wa zamani wa Misri, kutia saini mkataba wa Camp David mwaka 1978 na katika kuutambua rasmi utawala ghasibu wa Israel.
Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita inayosadifiana na 21 Novemba 1995, makubaliano ya amani ya Bosnia yaliyojulikana kwa jina la "Makubaliano ya Amani ya Dayton", yalitiwa saini. Makubaliano hayo ambayo yalifanyika kwa mashinikizo ya viongozi wa Marekani tarehe 21 Novemba 1995, yalitiwa saini na Marais wa wakati huo wa Bosnia Herzegovina, Serbia na Croatia. Mafanikio pekee ya makubaliano hayo kwa upande wa Waislamu, yalikuwa kuhitimishwa mauaji ya kinyama yaliyokuwa yakifanywa na Waserbia. Zaidi ya Waislamu laki moja waliuawa kwa umati katika vita vya Bosnia.
Na siku hii ya leo tarehe 21 Novemba imetangazwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Televisheni. Lengo la Umoja wa Mataifa la kuianisha siku hii lilikuwa kuweko mabadilishano ya vipindi vya runinga hususan vipindi vinavyotayarishwa kwa lengo la kueneza amani, ustawi wa kijamii na kiuchumi na kuimarisha masuala ya kiutamaduni katika jamii.
