Nov 23, 2023 03:05 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 23 Novemba, 2023

Leo ni Alkhamisi tarehe 9 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1445 Hijria mwafaka na tarehe 23 Novemba mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 659 iliyopita sawa na tarehe 9 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 786 Hijria, aliuawa shahidi faqihi na mtaalamu mkubwa wa hadithi Muhammad bin Jamaluddin Makki Amili, mashuhuri kwa jina la "Shahidi wa Kwanza." Alizaliwa mwaka 734 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Jabal Amil nchini Lebanon. Alijifunza elimu mbalimbali kutoka kwa walimu wakubwa wa zama zake kama vile Allama Hilli. Mbali na elimu ya dini, Muhammad bin Jamaluddin pia alikuwa hodari katika taaluma za mashairi na fasihi. Katika miaka 52 ya umri wake uliojaa baraka, Shahidi wa Kwanza aliandika vitabu vingi, ikiwa ni pamoja na "Albaqiyatus-Swalihat" na "al Lumuatu Dimashqiyya." Aliuawa na wapinzani wenye taasubi katika siku kama ya leo.

Katika siku kama ya leo miaka 465 iliyopita alizaliwa katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran Ṣadr al-Din, Muḥammad bin Ibrahim al-Shirazi maarufu kwa jina la Ṣadr al-Muta'allihīn na Mulla Sadra, mwanafalsafa na arif mkubwa. Awali alielekea katika mji wa Qazwin uliokuwa katika zama hizo mji mkuu wa utawala wa Safavi na kuhudhuria darsa na masomo ya walimu wakubwa kama Sheikh Bahai. Alisoma Fikihi, Usul, hadithi na hisabati kwa Sheikh Bahai na kusoma mantiki, falsafa na Irfan kwa Mirdamad. Baada ya Isfahan kufanywa mji mkuu, Mulla Sadra naye alihamia katika mji huo na kuanza kufundisha. Hata hivyo kutokana na mitazamo yake kupingana na maulama kadhaa, Mulla Sadra alilazimika kuuhama mji huo na kuanza kuishi katika kijiji cha karibu na mji wa Qum. Baada ya muda alianza tena kujishughulisha na kazi ya kufundisha na kualifu vitabu. al Mabdau Wal-Maad, Zaadul Musafir na Mutashabbihaat al-Qur'an ni baadhi tu ya vitabu vya Ṣadr al-Muta'allihīn au Mulla Sadra kama anavyojulikana pia.

Mulla Sadra

Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita Jagadish Chandra Bose, msomi mtajika wa Bangladesh alifariki dunia. Jagadish alizaliwa Novemba 30 mwaka 1858 katika moja ya maeneo ambayo ni viungwa vya mji mkuu Dhaka. Miongoni mwa elimu alizokuwa amebobea Jagadish nii fizikia, sayansi ya mimea na akiolojia. Hata hivyo umashuhuri wa Jagadish Chandra Bose unatokana na kuvumbua kwake Radio na tanuri ya miale (Microwave). 

Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha hati ya kuundwa nchi huru ya Palestina. Suala la Palestina lilikuwa miongoni mwa mambo ya mwanzo kabisa kujadiliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo maazimio mengi ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakiathiriwa na nchi kubwa zinazowaunga mkono Wazayuni wa Israel na utawala huo ulitumia moja ya maazimio hayo hapo tarehe 14 Mei 1948 kuanzisha dola haramu la Israel katika ardhi ya Palestina.  

Ardhi ya Palestina ilivyonyakuliwa na Wazayuni kuanzia mwaka 1946-2000

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, alifariki dunia André Malraux mwandishi na msanii maarufu wa Ufaransa. Malraux alizaliwa mwaka 1901 mjini Paris na katika ujana wake alikwenda nchini China na India zilizokuwa chini ya ukoloni wa Ufaransa na kujishughulisha na mapambano dhidi ya ukoloni wa nchi yake huko Mashariki mwa Asia. Wakati akirejea katika safari yake hiyo, aliandika kitabu maarufu kwa jina la ‘Hatma ya Mwanadamu.’ Katika vita vya ndani nchini Uhispania, Malraux alishirikiana na wapigania uhuru wa nchi hiyo. André alikuwa akipinga vita na umwagaji damu na alitetea pia uhuru wa mwanadamu. ‘Vilio vya Ukimya’, ‘Ushawishi wa Magharibi’, ‘Tumaini la Mwanadamu’ na ‘Washindi’ ni miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa na msanii huyo wa Kifaransa.  

André Malraux

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, yaani tarehe 23 Novemba mwaka 1996, ndege ya abiria ya Ethiopia iliyokuwa imetekwa nyara ilianguka katika fukwe za Bahari ya Hindi huko nchini Comoro baada ya kuishiwa na mafuta. Ndege hiyo ya Shirika la Ndege la Ethiopia aina ya Boeing 767 ilikuwa na abiria 175. Abiria 125 walipoteza maisha yao katika ajali hiyo. Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Addis Ababa kuelekea Nairobi.  

Tags