Jumatano, tarehe 20 Disemba, 2023
Leo ni tarehe 6Jumadithani 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 20 Disemba mwaka 2023.
Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita aliaga dunia alimu na mwanazuoni Mulla Fat'hullah Gharawi Isfahani aliyejulikana kwa jina la Sheikhu Shari'a Isfahani. Alizaliwa mwaka 1228 Hijria Shamsia huko Isfahan katikati mwa Iran na kupata elimu ya dini katika mji huo. Baadaye kidogo alielekea katika mji mtakatifu wa Mash'had na mwaka 1257 alikwenda Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kutafuta elimu na kusoma kwa walimu wakubwa na mashuhuri wa zama hizo. Ameandika vitabu kadhaa katika masuala ya sheria na fiqhi ya Kiislamu. Sheikhu Shari'a pia alikuwa mstari wa mbele katika mapambano ya kiutamaduni, kisiasa na kijeshi dhidi ya wakoloni wa Kiingereza na aliongoza harakati za wananchi wa Iraq dhidi ya wakoloni hao.

Siku kama ya leo miaka 88 iliyopita, Sheikh Izzuddin Qassam ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa harakati ya mapambano ya ukombozi wa wananchi wa Palestina dhidi ya uvamizi wa Wazayuni maghasibu na ukoloni wa Uingereza, aliuawa shahidi. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali huko Syria, Sheikh Qassam aliendeleza masomo yake katika Chuo Kikuu cha al Azhar huko Misri. Wananchi wa Palestina walianza mapambana dhidi ya mkoloni Mwingereza mwaka 1930 chini ya uongozi wa Sheikh Izzuddin Qassam. Hata hivyo baada ya kupita miaka kadhaa Wazayuni maghasibu walishirikiana na wakoloni wa Kiingereza na kumuuwa kigaidi kiongozi huyo wa harakati ya mapambano ya Palestina.

Miaka 72 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Oman ilipata uhuru kufuatia makubaliano yaliyosainiwa kati ya nchi hiyo na Uingereza. Oman ina historia kongwe na hadi kabla ya kudhihiri Uislamu, nchi hiyo kuna wakati iliwahi kuwa chini ya mamlaka ya Iran. Nchi hiyo iliwekwa chini ya mamlaka ya Waislamu baada ya kuaga dunia Mtume Muhammad (saw). Karibu karne moja baadaye kundi la Khawarij lilianzisha ghasia na uasi huko Oman na kuitawala nchi hiyo kwa karne kadhaa. Baadaye Oman ikakoloniwa na Ureno na Waingereza.

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, aliaga dunia John Steinbeck mwandishi wa riwaya wa Kimarekani baada ya kuishi kwa miaka 66. Alizaliwa mwaka 1902. Katika ujana wake Steinbeck alijishughulisha na kazi mbalimbali na hatimaye akaichagua taaluma ya uandishi. Mwandishi huyo alionesha kipaji cha hali ya juu alichokuwa nacho katika uwanja wa uandishi. Machungu ya Steinbeck katika maisha yake yalimuandalia uwanja wa kubainisha masaibu na machungu ya watu wasiojiweza katika maandishi na vitabuu vyake. Miongoni mwa vitabu vyake ni Travels with Charley, East of Eden, A Russian Jornal na Burning Bright.
