Dec 27, 2023 02:52 UTC
  • Jumatano, tarehe 27 Disemba, 2023

Jumatano tarehe 13 Jamadithani 1445 Hijria sawa na Disemba 27 mwaka 2023.

Tarehe 13 Jumadithani mwaka 64 Hijria kwa mujibu wa nukuu mashuhuri zaidi ya wanahistoria, alifariki dunia Fatima bint Huzam al Kulabiyya, maarufu kwa laqabu ya Ummul Banin, mke mwema na mcha Mungu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as).

Wanahistoria wamehitilafiana juu ya siku aliyozaliwa na baadhi wanasema alizaliwa mwaka wa 5 baada ya Hijra ya Mtume (saw). Imam Ali bin Abi Twalib alimuoa bibi huyu mwema baada ya kufariki dunia Bibi Fatima Zahra (as).

Ummul Banin anatoka katika kizazi cha mashujaa wakubwa wanaopigiwa mfano baina ya Waarabu. Baada ya kuolewa, mtukufu huyo alimuomba Imam Ali ampe laqabu ambayo atakuwa akiitumia kumwitia badala ya jina lake la Fatima ambalo alichelea kwamba, litakuwa likiwakumbusha wajukuu wa Mtume mama yao, yaani Fatimatu Zahraa (as). Aliwapenda sana Ahlul Bait wa Mtume na historia inahadithia jinsi alivyowatuma wanae wote wanne kwenda kulinda familia ya Mtume hususan Imam Hussain katika ardhi ya Karbala.

Watoto wote wanne wa Hadhrat Ummul Banin, wakitanguliwa na Abul Fadhl al Abbas, waliuawa shahidi wakiwa pamoja na kaka yao, Hussein katika medani ya Karbala. Ummul Banin alifariki dunia katika siku kama ya leo mjini Madina na kuzikwa katika makaburi ya Baqi'. 

Siku kama ya leo miaka 1015 iliyopita alifariki dunia Ibn Haytham, mwanafizikia, mwanahisabati na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu katika mji wa Cairo.

Ibn Haytham alizaliwa mwaka 354 Hijria katika mji wa Basra kusini mwa Iraq. Alibobea katika elimu za fizikia, tiba, falsafa na unajimu. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vya hisabati, nujumu na tiba.

Moja ya vitabu vyake muhimu ni al-Manadhir ambacho kimetafsiriwa katika lugha ya Kiingereza na kinatumika katika elimu ya nujumi. 

Ibn Haytham

Miaka 201 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Louis Pasteur, tabibu na mwanakemia wa Kifaransa. Akiwa shuleni Louis Pasteur alisoma kwa bidii na jitihada kubwa. Baada ya kumaliza masomo yake alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika kemia na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Strasbourg huku akijihusisha uhakiki na utafiti kuhusiana na masuala mbalimbali ya kielimu.   

Louis Pasteur

Katika siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, ulianzishwa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF).

Miongoni mwa yaliyokuwa malengo muhimu ya mfuko huo, ni kuandaa nafasi zaidi za ajira, udhibiti wa thamani ya sarafu za kigeni na kuhakikisha kwamba, kunakuweko ukuaji wenye uwiano katika masoko ya kimataifa.

Makao Makuu ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa yako mjini New York Marekani.   

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, kufuatia kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, mkataba wa kihistoria wa kuigawa Peninsula ya Korea ulitiwa saini mjini Moscow.

Mkataba huo ulitiwa saini na wawakilishi wa nchi tatu za Uingereza, Marekani na Umoja wa Sovieti. Kwa mujibu wa mkataba huo, Peninsula ya Korea ambayo hadi katika zama hizo ilikuwa nchi moja ikagawanywa katika sehemu mbili.

Kwa utaratibu huo, kukatokea nchi mbili za Korea ya Kaskazini na Kusini mgawanyiko ambao ungalipo hadi leo.   

Katika siku kama ya leo miaka 16 iliyopita Bi Benazir Bhutto kiongozi wa Chama cha Wananchi cha Pakistan (PPP) aliuawa kwa kufyatuliwa risasi na mlipuko wa bomu uliofanywa na magaidi huko Rawalpindi kaskazini mashariki mwa Pakistan.

Mbali na Bi Benazir Bhutto, watu wengine karibu 20 wafuasi wa chama cha PPP waliuawa pia katika mlipuko huo.

Bhutto alikuwa Waziri Mkuu wa Pakistan kwa mara ya kwanza mwaka 1988 baada ya kuenguliwa madarakani serikali ya kijeshi iliyokuwa ikiongozwa na Jenerali Muhammad Zia ul Haq.   

Benazir Bhutto

Na katika siku kama ya leo miaka 15 iliyopita, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha hujuma kubwa na ya pande zote dhidi ya Ukanda wa Gaza magharibi mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wakazi wa eneo hilo waliwakasirisha viongozi wa Kizayuni kutokana na kupambana kwao kishujaa dhidi ya uchokozi na mashambulizi ya Wazayuni na pia hatua yao ya kuiunga mkono serikali halali ya Palestina iliyokuwa ikiongozwa na harakati ya Hamas.

Ni kwa sababu hiyo ndio maana Ukanda wa Gaza ukawekwa chini ya mzingiro wa kiuchumi wa utawala haramu wa Israel kwa karibu mwaka moja na nusu kabla ya mashambulizi hayo, mzingiro ambao unaendelea kuwasababishia Wapalestina wa eneo hilo matatizo chungu nzima kama vile ukosefu wa chakula na dawa.   

Mashambulizi ya Israel Ukanda wa Gaza