Feb 09, 2024 02:17 UTC
  • Ijumaa, tarehe 9 Februari, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 28 Rajab 1445 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 09 Februari mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 1385 iliyopita, ilianza safari ya msafara wa Imam Hussein (as) kutoka Madina kwenda mjini Makka.

Hatua hiyo ilijiri baada ya kufariki dunia Muawiyah Bin Abu Sufiyan tarehe 15 ya mwezi wa Rajab na kutwaa madaraka mwanaye, Yazid Bin Muawiyah.

Baada ya Yazid kutwaa madaraka, haraka sana alimtaka mtawala wa mji wa Madina amlazimishe Imamu Hussein (as) kutoa baia (kiapo cha utiifu) kwake na kwamba iwapo angekataa kufanya hivyo basi amuuwe. Kwa kuzingatia kwamba Yazid alikuwa mtu muovu na mtenda madhambi, Imamu Hussein alikataa kutoa kiapo hicho na kwa ajili hiyo akaamua kuondoka Madina yeye na watu wa familia ya Mtume Muhammad (saw) kuelekea mjini Makkah.

Kabla ya kuanza safari hiyo, Imamu Hussein (as) alimuusia kaka yake Muhammad Ibnil-Hanafiyyah akisema: "Ninatoka kwa ajili ya kurekebisha umma wa babu yangu, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw); ninataka kuamrisha mema na kukataza maovu na kufuata njia ya babu yangu, Muhammad, na baba yangu, Ali Ibn Abi Twalib (as)…." 

Baada ya kufika Makka na kufuatia kukithiri barua za watu wa mji wa Kufa Iraq, waliokuwa wamemtaka aelekee huko kwa ajili ya kuwaongoza, Imamu Hussein (as) aliamua kuelekea Kufa ambapo hata hivyo alizuiliwa na jeshi la Yazid eneo la Karbala na kuuawa shahidi yeye na watu wa familia ya Mtume (saw) katika eneo hilo. 

Siku kama ya leo miaka 108 iliyopita alifariki dunia Ayatullahil-Udhma Sayyid Mohammed Kazem Tabatabai Yazdi maarufu kwa jina la Allamah Yazdi, msomi mashuhuri wa elimu ya fiqhi.

Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alijiunga na hauza ya kielimu ya mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Ayatullah Mirza Shirazi ambapo alifikia daraja ya ijtihadi.

Baada ya hapo alijishughulisha na kazi ya ufundishaji huku akihusika pia na kuasisi vituo vya misaada, misikiti na shule za kidini. Ameacha taathira mbalimbali lakini maarufu ni kitabu cha 'Al Urwatul-Wuthqa' na 'Bustane Niyaz' ambacho kinahusiana na dua.   

Sayyid Mohammed Kazem Tabatabai Yazdi

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, yaani tarehe 20 Bahman 1357 Hijiria Shamsia, vibaraka wa gadi ya mfalme Shah wa Iran, walivamia moja ya kambi za kikosi cha Jeshi la Anga mjini Tehran majira ya usiku, baada ya kundi la makamanda wa jeshi hilo kutangaza uungaji mkono wao kwa Mapinduzi ya Kiislamu na utiifu wao kwa Imam Ruhullah Khomeini.

Baada ya kutangazwa habari hiyo, wananchi Waislamu wa Iran kutoka pembe zote za mji wa Tehran walielekea katika kambi ya kikosi cha Jeshi la Anga ili kuwasadia wanajeshi hao ambao walikuwa wakipambana na vibaraka hao wa mfalme Shah.

Licha ya kutokuwa na silaha za maana wananchi hao walifanikiwa kuzima shambulio la vibaraka hao na kwa utaratibu huo, hatua ya mwisho ya kuuangushwa utawala wa Shah nchini Iran ikawa imeanza.  

Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita sawa na tarehe 9 Februari 1984, alifariki dunia Yuri Andropov, mmoja wa viongozi wa Urusi ya zamani.

Andropov ambaye alikuwa mwanasiasa mkubwa wa Urusi ya zamani alizaliwa tarehe 15 Juni 1914 ambapo akiwa kijana alijiunga na harakati za kisiasa na Chama cha Kikomonisti. Mwaka 1953 Yuri Andropov aliteuliwa kuwa balozi wa Urusi ya zamani nchini Hungary ambapo wakati nchi yake ilipoivamia Hungary mwaka 1956, alitwaa uongozi wa operesheni hiyo ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo na kutekeleza ukandamizaji na umwagaji damu dhidi ya wapigania uhuru wa Hungary. Mwaka 1967 Yuri Andropov aliteuliwa kuwa mkuu wa shirika la ujasusi la Urusi ya zamani KGB ambapo aliendelea kuliongoza shirika hilo kwa kipindi cha miaka 15 yaani hadi alipofariki dunia Leonid Brezhnev, Kiongozi wa wakati huo wa Urusi ya zamani hapo mwaka 1982.

Miezi saba tangu kiongozi huyo afariki dunia, Andropov aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa Chama cha Kikomonisti cha Urusi ya zamani, ambacho ni cheo cha juu kabisa nchini humo.

Aliendelea kusimamia uongozi wa chama hicho kwa kipindi cha miaka 15, hadi alipofariki dunia. Katika kipindi chake kuliongezeka mashindano ya uundaji wa silaha za nyuklia. 

Yuri Andropov

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, wapiganaji shupavu wa Iran walianzisha operesheni iliyopewa jina la Walfajr 8 kwa kushambulia ngome za jeshi la utawala wa zamani wa Iraq katika eneo la kusini zaidi la mpaka wa nchi mbili hizi.

Maelfu ya wapiganaji wa Iran walivuka Mto Arvand na kufanikiwa kuuteka mji wa Faw unaopatikana kusini mashariki mwa Iraq, katika siku ya kwanza ya operesheni hiyo. Operesheni hiyo ilikuwa ya ghafla na tata kwa upande wa kijeshi na iliwashangaza weledi wa masuala ya kijeshi na kisiasa ulimwenguni na utawala wa zamani wa Iraq.

Operesheni ya Walfajr-8 ilitekelezwa kwa lengo la kuushinikiza utawala wa Saddam uache kuikalia kwa mabavu ardhi ya Iran na kuilipa fidia Tehran kutokana na hasara na maafa yaliyosababishwa na uvamizi wa Iraq. 

Operesheni ya Walfajr-8

Na siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, baada ya Chama cha Wokovu wa Kiislamu cha Algeria (FIS) kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge, wanajeshi waliokuwa wakitawala nchini humo, walibatilisha matokeo ya uchaguzi huo na kukipiga marufuku chama hicho, hali iliyopelekea kuzuka machafuko makubwa.

Machafuko hayo yalipelekea kuuawa watu wengi nchini Algeria.