Feb 13, 2024 07:19 UTC
  • Jumanne, tarehe 13 Febuari, 2024

Leo ni Jumanne tarehe 3 Shaaban 1445 Hijria sawa na tarehe 13 Februari 2024.

Siku kama ya leo miaka 1441 iliyopita, alizaliwa Imam Hussein (as) mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (saw). 

Kipindi bora cha maisha ya Imam Hussein (as) ni cha miaka sita wakati mtukufu huyo alipokuwa pamoja na Mtume Mtukufu wa Uislamu. 

Imam Hussein (as) alijifunza maadili mema na maarifa juu ya kumjua Mwenyezi Mungu kutoka kwa baba yake Imam Ali (as) na mama yake Bi Fatimatul-Zahra (as), ambao walilelewa na Mtume Mtukufu.

Imam Hussein alishiriki vilivyo katika matukio mbalimbali wakati Uislamu ulipokabiliwa na hatari. 

Daima alilinda turathi za thamani kubwa za Mtume kwa kutoa darsa na mafunzo kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya kiitikadi, kifikra na kisiasa. Imam Hussein (as) alichukua jukumu la kuuongoza umma wa Kiislamu mwaka 50 Hijria, baada ya kuuawa shahidi kaka yake Imam Hassan (as). 

Hatimaye Imam Hussein (as) aliuawa shahidi huko Karbala mwaka 61 Hijria wakati akitetea dini tukufu ya Kiislamu.

Katika siku kama ya leo miaka 1385 iliyopita, msafara wa Imam Hussein (as) mjukuu wa Bwana Mtume (saw) uliwasili katika mji wa Makka.

Imam Hussein ambaye alikuwa amehatarisha maisha yake kwa kuupinga utawala wa Yazid na kukataa kumpa baina na mkono wa utiifu kiongozi huyo, aliondoka Madina na kuelekea Makka. Alipowasili mjini Makka Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib alilakiwa na watu wengi na shakhsia wakubwa wa mji huo na akaamua kuitumia fursa ya uwepo wa Mahujaji kwa ajili ya kufichua ufisadi wa Bani Ummayah hususan Yazid bin Muawiya na kwa muktadha huo akawa amefikisha ujumbe wake katika pembe mbalimbali za maeneo ya Waislamu.

Akiwa  Makka, Imam Hussein alipokea maelfu ya barua kutoka kwa wakazi wa mji wa Kufa Iraq ambao mbali na kutangaza kuupinga utawala wa Yazid walimtaka Imam aelekee katika mji huo. Baada ya kukaa kwa takribani miezi mine mjini Makka na kwa kuzingatia mwaliko wa mara kwa mara wa watu wa Kufa na kutokana na hatari iliyokuwa ikimkabili kutoka kwa makachero wa Yazid, tarehe 8 Dhulhija mwaka 60 Hijria, alielekea katika mji wa Kufa. 

Siku kama ya leo mwaka 1946 wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, ndege za kivita za Uingereza na Marekani zilianza kudondosha zaidi ya tani 3900 za mabomu katika mji wa Dresden nchini Ujerumani.

Mashambulizi hayo yaliua zaidi ya watu 25,000 na kusababisha majonzi na vilio kote duniani.

Miaka 36 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Ayatullah Sheikh Salman Khaqani.

Alizaliwa mwaka 1293 Hijria Shamsia katika moja ya miji ya kusini mwa Iraq ya leo. Baada ya kupitisha kipindi cha utoto, akiwa na umri wa miaka 13 alihajiri na kuelekea Najaf al-Ashraf kwa ajili ya kusoma masomo ya dini. Akiendelea na masomo yake, Sheikh Salman Khaqani hakuacha kujihusisha na harakati za kijamii, kiasiasa na kifasihi. Akiwa na umri wa miaka 43 na baada ya kufariki dunia baba yake aliyekuwa mmoja wa maulama wa Khorramshahr hapa Iran aliuchagua mji huo kuwa makazi yake.

Katika kipindi cha miongo mitatu ya kuishi kwake mjini Khorramshahr, mwanazuoni huyo aliondokea kuwa chimbuko la uongofu wa watu na kufanikiwa kutoa huduma zenye thamani kubwa. Baada ya kuanza vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa Baath wa Iraq, nyumba ya alimu huyo ilikuwa kimbilio la watu.

Sheikh Salman Khaqani

 

Tags