Mar 23, 2024 02:29 UTC
  • Jumamosi, 23 Machi, 2024

Leo ni Jumamosi 12 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1445 Hijreia mwafaka na 23 Machi 2024.

Siku kama ya leo yaani tarehe 12 Ramadhani kwa mujibu wa wapokezi wengi wa kalenda ya Hijria Qamaria, ni siku ambayo Nabii Issa Ibn Maryam, Masih AS aliteremshiwa kitabu kitukufu cha Injili. Neno Injili ni la Kigiriki na lina maana ya bishara. Jina hilo limetajwa mara 12 katika Qur’ani Tukufu na kitabu hicho kinaitambua Injili kuwa ni kitabu cha Mwenyezi Mungu SW chenye sheria na kanuni za mbinginu. Hata hivyo kitabu kinachojulikana hivi sasa kwa jina la Injili si kile kilichoteremshwa kwa Nabii Issa Masih bali ni riwaya na kumbukumbu zilizokusanywa na wanafunzi wake baada ya Yeye kupaa mbinguni. ***

Katika siku kama ya leo miaka 1444 iliyopita yaani tarehe 12 Ramadhani mwaka wa kwanza Hijria, muda mfupi baada ya Mtume Mtukufu Muhammad (SAW) kuhama Makka na kuelekea Madina, aliunga udugu baina ya Muhajirina na Ansar. Muhajirina ni watu ambao walihama na Mtume (SAW) kutoka Makka kwenda Madina, na Ansar ni Waislamu wa Madina waliowakaribisha Muhajirina katika mji huo. Kwenye sherehe hiyo ya kuunga udugu bina ya Waislamu, Mtume (SAW) alimtangaza Ali bin Abi Talib (AS) kuwa ndugu yake hapa duniani na Akhera. 

Tarehe 12 Ramadhani miaka 848 iliyopita, alifariki dunia Ibn Jawzi, faqihi na mtaalamu mkubwa wa hadithi katika karne ya 6 Hijria. Ibn Jawzi alizaliwa mwaka 510 Hijria na kufanya safari nyingi kwa ajili ya masomo. Mbali na kubobea katika masuala ya elimu ya fiq'hi na hadithi, alikuwa mtaalamu katika uwanja wa kutoa mawaidha na hata akaweza kuaminiwa na maulamaa wakubwa wa zama zake. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi na mashuhuri zaidi ni Al Muntadhim na Mawaidhul Muluk. 

Miaka 372 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani sawa tarehe 23 Machi mwaka 1652, yalianza shambulizi la manowari za kijeshi za Uingereza dhidi ya majeshi ya Uholanzi. Amri ya shambulizi hilo ilitolewa na Oliver Cromwell aliyekuwa dikteta wa wakati huo wa Uingereza. Akipata uungaji mkono wa Bunge la Uingereza, Cromwell alimpindua mfalme wa Uingereza na kisha kulivunja bunge la nchi hiyo. Inasemekana kuwa, lengo la kutekeleza shambulio hilo lilikuwa ni kulimaliza nguvu jeshi la Uholanzi ambalo lilikuwa na nguvu kubwa ya majini. 

Oliver Cromwell

Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, ilianzishwa harakati ya Ufashisti nchini Italia kwa uongozi wa Benito Mussolini. Ufashisti kwa ujumla ni utawala wa kidikteta wenye kufuata aidolojia ya kibaguzi na kiutaifa, kuwakandamiza wapinzani, kukandamiza uhuru na kuzipotosha itikadi na fikra za wananchi. Hayo yalijiri baada ya Mussolini kunyakuwa wadhifa wa uwaziri mkuu nchini Italia mwaka 1922 na kuanza utawala wa kidikteta nchini humo. Muda mfupi baadaye Mussolini alishirikiana na Adolph Hitler, na kuandaa mazingira ya kuanzishwa Vita vya Pili vya Dunia. 

Benito Mussolini

Katika siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, liliasisiwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani 'WMO'. Shirika hilo linafungamana na Umoja wa Mataifa na taasisi zote za hali ya hewa ulimwenguni hushirikiana na shirika hilo. Miongoni mwa malengo ya kuanzishwa shirika hilo ni kutoa msaada wa elimu ya hali ya hewa kwa wataalamu wa anga, mabaharia, wakulima na shughuli nyingine za kibinadamu. Ni kwa ajili hiyo ndio maana siku ya leo yaani tarehe 23 Machi ikajulikana kuwa Siku ya Hali ya Hewa Duniani. ***