Jumanne, tarehe Pili Aprili, 2024
Leo ni Jumanne tarehe 22 Ramadhani 1445 Hijria sawa na Aprili Pili mwaka 2024.
Siku kama ya leo miaka 1172 iliyopita, alifariki dunia Ibn Majah, mpokezi wa Hadithi na mfasiri mashuhuri wa Qur’ani wa Kiislamu.
Ibn Majah alizaliwa mwaka 209 Hijria katika mji wa Qazvin nchini Iran. Alielekea katika nchi mbalimbali za Kiislamu ili kujifunza elimu ya Hadithi. Aliandika kitabu chake mashuhuri kwa jina la "Sunan Ibn Majah" baada ya kuhitimu masomo katika elimu ya Hadithi, kitabu ambacho ni moja kati ya vitabu sita vya Hadithi vyenye itibari vya Waislamu wa madhehebu ya Suni.
Vitabu vingine vya Ibn Majah ni Tafsirul Qur'an na Tarikh Qazvin.
Katika siku kama ya leo miaka 219 iliyopita, alizaliwa huko nchini Denmark, Hans Christian Andersen malenga, mwandishi na msimulizi wa visa maarufu vya watoto.
Andersen ambaye alikuwa mtoto wa bwana mmoja maskini na fundi viatu, alihamia Copenhagen mji mkuu wa Denmark na kuanza kucheza michezo ya kuigiza. Baada ya muda, Hans Andersen alianza kutunga visa na kuwa mashuhuri baada ya kuandika kitabu chake cha kwanza cha hadithi alichokipa jina la "Fairy Tales, Told for Children" mnamo mwaka 1838.
Miaka 42 iliyopita katika siku kama hii ya leo, vikosi vya jeshi la majini la Argentina vilivamia visiwa vya Falkland kwa jina jingine (Malvinas) na kuvidhibiti visiwa hivyo vya kiistratejia vilivyoko kusini mashariki mwa nchi hiyo.
Visiwa vya Falkland ambavyo kwa lugha ya Kiargentina vinatamkwa kama Malvinas, viligunduliwa katika karne ya 16 na kukaliwa kwa mabavu na Uingereza mwaka 1832.
Na siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, aliaga dunia Papa John Paul II aliyekuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani.
Papa John Paul II alizaliwa mwaka 1920 huko Poland na kufikia daraja ya uchungaji baada ya kuhitimu masomo ya dini. Mwaka 1964 Papa John Paul alikuwa askofu wa mji wa Kraku huko Poland na miaka mitatu baadaye akawa Kadinali. Hatimaye mwaka 1978 John Paul wa Pili aliteuliwa kushika wadhifa wa ngazi ya juu zaidi wa kanisa Katoliki, yaani Papa.
Papa John Paul wa Pili alikuwa mfuasi wa mazungumzo baina ya dini mbalimbali hususan kati ya Uislamu na Ukristo. Alikuwa akipinga vikali utoaji mimba na ndoa za watu wa jinsia moja na ufisadi wa kimaadili kwa ujumla uliotanda katika ulimwengu wa Magharibi. Aidha alikosoa vikali mashambulio ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iraq.