Apr 29, 2024 02:35 UTC
  • Jumatatu, tarehe 29 Aprili, 2024

Leo ni Jumatatu tarehe 20 Shawwal 1445 Hijria sawa na Aprili 29 mwaka 2024.

Tarehe 10 Ordebehesht kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani inafahamika kuwa Siku ya Taifa ya Ghuba ya Uajemi.

Siku hii jina hilo kutokana na baadhi ya pande zenye chuki dhidi ya Iran, kufanya njama za kutaka kupotosha historia, kwa kuipa majina mengine yasiyo na msingi. Jina la kihistoria la Ghuba ya Uajemi limetafsiriwa katika lugha mbalimbali kwa jina hilo au kwa jina la Bahari ya Pars. Inafaa kuashiria hapa kuwa, Ghuba ya Uajemi ni ya tatu kwa ukubwa duniani baada ya Ghuba ya Mexico na Ghuba ya Hudson.

Kutokana na kuwa na vyanzo vingi vya utajiri yakiwemo mafuta na gesi, Ghuba ya Uajemi na pwani yake inahesabika kimataifa kuwa sehemu yenye umuhimu mkubwa na ya kistratijia. Kwa kuzingatia utambulisho wa kiutamaduni na kihistoria wa taifa la Iran, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Utamaduni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, liliitangaza siku ya leo ambayo inakumbusha tukio la kuwaondoa Wareno kutoka lango la Hormuz, kuwa siku ya taifa ya Ghuba ya Uajemi.

Siku kama ya leo miaka 628 iliyopita mtaalamu wa lugha na mwandishi mashuhuri wa zama hizo Majduddin Abu Tahir Muhammad Yaaqub Firuzabadi aliaga dunia. 

Firuzabadi alikuwa pia hodari katika taaluma za Hadithi na tafsiri ya Qur'ani na ameandika vitabu kadhaa katika taaluma hizo. Hata hivyo kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni "al Qamus" ambacho ni miongoni mwa kamusi muhimu za lugha ya Kiarabu. Vitabu vingine mashuhuri vya mwanazuoni huyo wa Kiislamu ni "Sifrul Saada" na "Tanwirul Miqyas". 

Miaka 170 iliyopita siku kama leo Henri Poincare mtaalamu wa sayansi na hisabati wa Ufaransa alizaliwa katika mji wa Nancy nchini humo.

Poincare alikuwa mahiri katika somo la hisabati na alianza kufanya utafiti katika uwanja huo. Chunguzi mbalimbali zilizofanywa na mwanahisabati huyo wa Kifaransa kuhusiana na masuala ya uchanganuzi wa kimahesabu, mwangaza, umeme n.k zimetajwa kuwa muhimu na sahihi. 

Henri Poincare

Siku kama ya leo miaka 96 iliyopita sawa na tarehe 29 mwezi Aprili mwaka 1928, nchini Uturuki herufi za Kilatini zilitambuliwa rasmi na kuchukua nafasi ya zile za Kiarabu.

Hatua hiyo ilichukuliwa katika njama za kuipiga vita dini ya Uislamu na badala yake kuingizwa tamaduni za Kimagharibi katika jamii ya wananchi wa Uturuki. Mchakato huo ulianzishwa na Mustafa Kamal maarufu kwa jina la Ataturk kuanzia mwaka 1923. Mfumo wa Jamhuri ulishika hatamu za uongozi huko Uturuki chini ya Ataturk kuanzia mwezi Oktoba mwaka 1923 baada ya kuanguka kwa utawala wa Othmania uliodumu kwa miaka 623 nchini humo. ***

Miaka 79 iliyopita katika siku kama ya leo majeshi ya Muungano yalipata pigo kubwa mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia.

Vikosi vya nchi Waitifaki wa Ulaya vilifanya mashambulizi ya pande zote dhidi ya Italia baada ya kusambaratishwa safu ya ulinzi ya Ujerumani. Italia ilikuwa muitifaki wa Ujerumani chini ya uongozi wa Musolini. Baada ya ushindi huo askari karibu milioni moja wa Ujerumani waliokuwa nchini Italia walijisalimisha kwa majeshi ya Waitifaki.   ***

Na tarehe 10 Ordibehesht miaka 45 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikata uhusiano wake na Misri.

Amri ya kukatwa uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Misri ilitolewa na hayati Imam Ruhullah Khomeini baada ya Rais wa wakati huo wa Misri, Anwar Sadat kutia saini makubaliano ya aibu na fedheha ya Camp David na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusaliti malengo ya Wapalestina. Kutiwa saini makubaliano hayo ilikuwa hatua ya kuhalalisha uvamizi wa Wazayuni dhidi ya Palestina na kusaliti haki za Wapalestina waliokuwa wakipambana na utawala haramu wa Israel na vilevile kupuuza maslahi ya Umma wa Kiislamu. Baadaye kiongozi huyo wa Misri alitiwa adabu na shujaa, Khalid Islambuli aliyemmiminia risasi na kumuua kutokana na usaliti huo.

 

Tags