Apr 30, 2024 02:52 UTC
  • Jumanne, tarehe 30 Aprili, 2024

Leo ni Jumanne tarehe 21 Mfunguo Mosi Shawwal 1445 Hijria sawa na Aprili 30 mwaka 2024.

 Miaka 1353 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, ardhi ya Andalusia huko Uhispania ya leo ilidhibitiwa na jeshi la Kiislamu lililoongozwa na Tariq bin Ziyad. Tariq ambaye alikuwa na wapiganaji karibu ya elfu 12, alivuka kwa boti mlango bahari ulioko kati ya Morocco na Uhispania ambao umepewa jina lake Tariq bin Ziad au "Gibraltar". Tariq bin Ziyad aliamuru kochomwa moto boti zote zilizotumiwa na wapiganaji wake kuvukia lango bahari na Gibralta ili kuwahamasisha zaidi kupigana na maadui. Katika kipindi cha karne 8 za utawala wao huko Andalusia, Waislamu walianzisha vituo mbalimbali vya utamaduni na taasisi za kiuchumi na kwa kipindi kirefu ardhi hiyo ilikuwa kituo kikuu cha ustaarabu wa Kiislamu barani Ulaya.   

Tariq bin Ziyad

Katika siku kama hii ya leo miaka 1091 iliyopita, alifariki dunia Ibn Habban, mtaalamu wa hadithi, elimu ya fiq'hi na mwanahistoria mashuhuri wa karne ya 14 Hijiria.

Alipata elimu ya msingi kwa walimu mashuhuri wa zama zake na kisha akaelekea Neishabur kaskazini mwa mashariki mwa Iran, ambao katika kipindi hicho ulikuwa ni moja ya vituo muhimu vya kielimu. Ibn Habban anahesabika kuwa mtu mwenye nadharia muhimu katika elimu ya hadithi. Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyu mkubwa ni pamoja na kitabu cha"At-Thuqat" na Rawdhatul-Uqalaai wa Nazahatul-fudhalaai." 

Siku kama ya leo miaka 247 iliyopita, alizaliwa Carl Friedrich Gauss mwanahisabati na mnajimu mashuhuri wa Kijerumani.

Mama yake Gauss ndiye aliyemshawishi mno mwanawe ajikite zaidi katika somo la hisabati, na hatimaye mtoto huyo alitabahari kwenye fani hiyo. Msomi huyo wa hisabati na mnajimu mashuhuri wa Kijerumani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 78. 

Carl Friedrich Gauss

Tarehe 30 Aprili mwaka 1945 dikteta wa zamani wa Ujerumani, Adolf Hitler, alijiua akiwa mafichoni chini ya ardhi baada na kufeli ndoto yake ya kutawala dunia nzima.

Hitler alizaliwa mwaka 1889 nchini Austria na alipigana Vita vya Kwanza vya Dunia katika safu za kwanza za askari wa Ujerumani. Adolf Hitler alianzisha chama cha National Socialist German Workers baada ya kuchanganya itikadi za kisoshalisti na mitazamo mikali ya utaifa. Na ulipotimia mwaka 1939 alianzisha Vita vya Pili vya Dunia.   

Adolf Hitler

 

Tags