Tuujue Uislamu (11)
Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji tunapokutana katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu.
Katika kipindi chetu cha juma hili tutaendelea kubainisha ishara miongoni mwa ishara na alama za Tawhidi na uwepo wa Mwenyezi Mungu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki, hii ikiwa ni sehemu ya 11 ya mfululizo huu.
Bilal Habashi sahaba mtukufu na muadhini wa Mtume (saww) anasimulia kwamba: Katika usiku ambao Aya za 190 hadi 194 za Sura Al-Imran ziliteremshwa kwa Mtukufu Mtume wa Uislamu (SAW), mbora huyo wa viumbe alisimama akisali na kulia mpaka alfajiri. Kulipopambazuka, nilipoenda kwa ajili ya Sala ya asubuhi, niliona macho yake yenye machozi na nikashangaa sana. Nikamwaambia: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, kwa nini unalia, ilihali umejumuishwa katika neema maalumu za Mwenyezi Mungu? Katika kunijibu, Mtume alisema: Jana usiku, Mwenyezi Mungu aliniteremshia Aya za kutikisa moyo. Ewe Bilal, ole wake mwenye kuzisoma Aya hizi na asizitafakari. Kisha Mtume (SAW) akazisoma Aya hizo kwa sauti nzuri na ya kupendeza. Aya hizo zinasema:
Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara kwa wenye akili. Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima na wakikaa kitako na wakilala, na hufikiri kuumbwa mbingu na ardhi, wakisema: Mola wetu Mlezi! Hukuviumba hivi bure. Subhanaka, Umetakasika! Basi tukinge na adhabu ya Moto.
Katika Aya nyingi, Qur'ani Tukufu inawaita na kuwataka watu kusoma mfumo wa uumbaji ili kuelewa kuwepo kwa Muumba pekee wa ulimwengu kupitia kufikiri juu ya matukio. Mpangilio sahihi na wa kushangaza wa ulimwengu wa uumbaji unaelezea kuhusu lengo na tadibiri ya Mwenyezi Mungu. Ulimwenguni katika maisha ya wanyama na mimea, ardhini, angani, na mbinguni, katika chembechembe za atomu, na katika viumbe vyote kuanzia kile kidogo hadi kikubwa zaidi, inaweza kuonekana bayana na dhahiri hekima ya Mungu isiyo na kikomo, mipango na nguvu Zake.
Kwa hakika kusoma na kutwalii siri za kitabu cha uumbaji, ambacho kurasa zake zote zinashuhudia nafasi na mchango wa akili aali katika uumbaji wake, ni njia ya kumjua Mungu. Kila mtu, kwa kadiri ya kipaji chake na ufahamu wake, anaweza kufikiri na kutafakari katika mfumo wa ulimwengu na kuchunguza ishara za uratibu na mipango katika matukio ya uumbaji na kupata uthibitisho thabiti wa kuwepo kwa chimbuko la uwepo katika moyo wa kila chembe. Moja ya madhihirisho ya uwezo wa Mwenye Ezi Mungu ni kuwepo kwa uhai katika mgongo wa ardhi na ndani ya bahari. Bila shaka, kuweko kwa uhai katika mgongo wa ardhi kunategemea mambo mengi, ambapo kutokuwepo kwa mojawapo huzuia kupatikana uhai huo kwenye sayari hii. Wazo kwamba mambo yote muhimu kwa maisha yalipatikana kwa sadfa na hivi hivi tu ni dhana isiyo na busara na hekima. Mwenyezi Mungu amefanya maji kuwa chanzo cha uhai. Tumeona mvua mara nyingi ikinyesha na kupata uzoefu wa hisia ya furaha na nishati. Matone ya mvua ya rehema ambayo huanguka kwenye ardhi kavu na yenye kiu, huleta uhai na kijani kibichi duniani. Kwa sababu hiyo, maelfu ya mimea, miti na kijani kibichi huota katika ardhi na kuleta mandhari nzuri na ya kuvutia ambayo huwa ishara ya kuweko uhai. Kwa hakika mimea inahesabiwa kuwa dhihirisho la uhai. Aya za 26 na 27 za Surat Abasa zinasema: Tena tukaipasua pasua ardhi kwa nguvu. Kisha tukaotesha humo nafaka.

Swali la kujiuliza hapa ni kwamba, ardhi imepasuliwa kwa kutumia nini? Kwa mmea mdogo, laini na unaochipua na ambao umeweza kupasua ardhi ngumu, licha ya uzito wa ardhi na udongo wake. Mbegu ya mmea huo imejitutumua na kuota na kisha kupasua ardhi na kuelekea juu ili kupata mwanga wa jua na hewa. Ni nani anayeongoza na kusimamia uhai wa mbegu chini ya udongo na nje yake? Kwa hakika, mvua na jinsi mimea inavyokua kutoka ardhini humfanya kila mtu mwenye hekima afikiri na kutafakari juu ya hilo.
Moja ya maajabu ya mimea ni kwamba Mungu amelinda matunda na mazao ya kilimo kutokana na hatari ya uharibifu na kuangamia kwa njia tofauti. Amehifadhi nafaka kama vile kunde, maharagwe, mahindi na kadhalika kwenye vitu kama magunia na mashuke ya ngano, shayiri na mchele kwenye mashuke yaliyobana na kuweka kitu mfano wa mkuki kwenye kichwa cha kila punje ili ndege wasiweze kung'oa kwa urahisi. Ili kuipa mimea chakula, Mwenyezi Mungu ameweka mzizi wa kufyonza virutubisho vyenye manufaa kutoka kwenye udongo na kuvitoa kwenye majani na matunda. Dutu hizi hufikia matunda kutoka kwenye shina na majani. Kwa utaratibu huu, matunda yana virutubishi vingi kama vile chumvi, madini na vitamini zinazohitajika kwa wanadamu. Kwa upande mwingine, mizizi, kwa sababu imepenya ndani ya udongo, hufanya mimea kusimama na kubaki imesimama dhidi ya upepo mkali. Wakati huo huo, kokwa za matunda pia zina jukumu maalumu. Kokwa za matunda zimeumbwa ili kuzipanda na hivyo kuzaa maua na miti na kufanya miti na matunda kuongezeka. Jambo lingine ni kwamba, mimea ina matumizi ya chakula na tiba kwa binadamu. Kwa kuchunguza maajabu ya mimea, tunaelewa kwamba, muumba wake alikuwa anajua manufaa ya vitu aliumba mimea akiwa anafahamu mahitaji ya wanadamu na viumbe vingine hai.
Mimea ina maajabu mengi. Kwa uangalifu kidogo tu, tunaweza kutambua kwamba Muumba wake ni Muweza na ameweka mfumo fulani wa mageuzi kwa kila aina ya mimea, ambayo ni tofauti na nyingine kwa kiasi chake na kulingana na mahitaji.
Aya ya 19 ya Surat al-Hijr inasema:
Na ardhi tumeitandaza na humo tumeweka milima, na tumeotesha kila kitu kwa kiasi chake. Hivyo basi, miti na mimea hutufundisha somo la imani ya Mungu mmoja yaani tawhidi ili nyuma ya majani haya laini, macho yaweze kuona ukweli uliopo wa uweza wa milele wa Mungu.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati. Ninakuageni nikitaraji kukutana nanyi katika kipindi chetu kingine cha mfululizo huu wa Tuujue Uislamu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.