Jumanne, tarehe 14 Mei, 2024
Leo ni Jumanne tarehe 5 Dhulqaada 1445 Hijria sawa na tarehe 14 Mei 2024.
Tarehe 25 Ordibehesht ni siku ya kumbukumbu ya Abul-Qassim Firdowsi mwanafalsafa na malenga mashuhuri wa Iran.
Inasemekana kuwa Firdowsi alizaliwa mwaka 319 au 320 Hijria Shamsia katika mji wa Tus, kaskazini mashariki mwa Iran. Miongoni mwa athari muhimu za malenga huyo wa Kiirani ni kitabu alichokipa jina la "Shahnameh".
Kitabu hicho kilichosheheni historia ya jadi na utamaduni wa Iran kabla ya ujio wa Uislamu, kimefasiriwa kwa lugha mbalimbali.
Siku kama ya leo miaka 449 iliyopita, ardhi ya Angola ilikaliwa kwa mabavu na mkoloni Mreno.
Kabla ya Wareno kuwasili Angola, ardhi hiyo ilikuwa sehemu ya utawala wa Kiafrika wa Guinea. Baada ya Wareno kuidhibiti nchi hiyo walianzisha vituo vya biashara katika maeneo yake yote ya pwani. Baada ya kumalizika vita vya Pili vya Dunia, harakati kadhaa zilianzishwa nchini Angola kwa lengo la kupigania uhuru wa nchi hiyo.
Hatimaye mwaka 1975 harakati za wapigania uhuru zilizaa matunda baada ya nchi yao kupata uhuru.
Siku kama ya leo miaka 781 iliyopita, aliaga dunia Radhiyyuddin Ali ibn Musa mashuhuri kwa jina la Sayyid Ibn Tawus, fakihi, mpokezi wa Hadithi, mwanahistoria na mwanafasihi wa Kiislamu.
Alizaliwa katika mji wa Hillah nchini Iraq. Awali Ibn Taus alisoma kwa baba na kwa babu yake na baadaye akahudhuria darsa za wanazuoni mashuhuri wa mji wa Hillah. Sayyid Ibn Tawus mbali na kujulikana kama msomi na alimu mkubwa, vilevile alikuwa mashuhuri kwa sifa ya uchaji Mungu na kuipa mgongo dunia.
Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameandika vitabu kuhusiana na maudhui mbalimbali. Moja ya vitabu vyake mashuhuri ni kile kinachojulikana kwa jina la Al Luhoof kinachozungumzia tukio la Ashura.
Siku kama ya leo miaka 228 iliyopita, chanjo ya kwanza kabisa ya ugonjwa wa ndui ilitolewa nchini Uingereza.
Japokuwa hii leo ugonjwa huo umetoweka katika maeneo mengi ya dunia hususan katika nchi zilizoendelea, lakini hadi kufikia karne ya 18, maradhi hayo yalienea sana ndani ya mataifa mengi na kusababisha madhara makubwa.
Mwaka 1717 mwanamke mmoja wa Uingereza alianzisha utafiti na uchunguzi mkubwa katika suala hilo, ambapo juhudi zake zilipunguza sana idadi ya waathirika wa maradhi hayo.
Hatimaye tarehe 14 Mei mwaka 1796 Dakta Edward Jenner aliifanyia majaribio chanjo ya ndui kupitia mwili wa mtoto mdogo na kutoa majibu mazuri.
Siku kama ya leo miaka 213 iliyopita, nchi ya Paraguay ilijipata uhuru.
Paraguay iligunduliwa katika karne ya 16 Miladia na Muhispania mmoja na ikawa chini ya utawala wa Uhispania kwa zaidi ya karne mbili. Baada ya uhuru nchi hiyo ilitawaliwa na serikali ya kidikteta na kulishudiwa majaribio kadhaa ya mapinduzi na kila aliyeingia madarakani aliongoza kidikteta.
Uchaguzi wa kwanza huru wa rais ulifanyika nchini humo mwaka 1989. Kijiografia Jamhuri ya Paraguay inapatikana huko Amerika Kusini baina ya nchi za Brazil, Argentina na Bolivia.
Siku kama ya leo miaka 157 iliyopita alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 74, Joseph Reinaud, msomi na mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati wa Ufarasa.
Kutokana na kupendelea sana lugha za eneo la Mashariki ya Kati, alianza kujifunza lugha na fasihi ya Kiarabu. Baada ya muda mfupi, Joseph Reinaud alianza kufundisha lugha hiyo katika chuo kikuu nchini Ufaransa. Aliandika vitabu kuhusiana na historia ya Uislamu ambapo moja ya vitabu hivyo ni 'Fat'hul-Arab' na 'Al-Islamu Walmuslimin.
Katika siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, utawala bandia wa Israel ulitangaza uwepo wake baada ya kufanya mauaji makubwa ya umati dhidi ya Wapalestina.
Askari wa Uingereza waliikalia kwa mabavu Palestina kufuatia kushindwa utawala wa Othmania wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Miaka mitano baadaye Jumuiya ya Kimataifa iliikabidhi Palestina kwa Uingereza na kuiweka chini ya mamlaka ya mkoloni huyo.
Novemba mwaka 1947 Umoja wa Mataifa ulipasisha azimio lililotaka kuundwa madola mawili ya Kiarabu na Kiyahudi katika ardhi ya Palestina.
Na siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, mkataba wa kisiasa na kijeshi wa Warsaw ulitiwa saini baina ya nchi nane za kikomonisti barani Ulaya.
Makubaliano hayo yaliyojulikana kama The Warsaw Pact yalitiwa saini katika mji mkuu wa Poland, Warsaw, lengo lake lilikuwa ni kukabiliana na Mkataba wa Shirika la Kujihami la Nchi za Magharibi (NATO) uliotiwa saini na madola ya magharibi waitifaki wa Marekani.
Nchi zilizotia saini makubaliano hayo ziliahidi kutotumia nguvu na mabavu katika ushirikiano wao. Aidha zilikubaliana kwamba, kushambuliwa kijeshi mwanachama mmoja ni sawa na kuchokozwa nchi zote wanachama. Hatimaye baada ya miaka 36, mkataba huo ulifutwa mwaka 1991 baada ya nchi hizo kukutana huko Budapest mji mkuu wa Hungary.