Russia yaitahadharisha Ufaransa kuhusu kutuma makombora Ukraine
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ametahadharisha kuhusu Ufaransa kutuma makombora nchini Ukraine.
Akizungumza katika mahojiano na gazeti la Kifaransa la L'Journal Dudimanche", Sebastien Lecornu Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa ameeleza kuwa kumetolewa amri ili kulitumia jeshi la Ukraine makombora kumi ya masafa marefu ya aina ya Scallop kutoka Ufaransa na Uingereza.
Maria Zakharova Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameitahadharisha serikali ya Ufaransa kuhusu kutumia makombora hayo tajwa kushambulia ardhi ya Russia.
Harakati za nchi za Magharibi za kutuma silaha zao huko Ukraine zinajiri katika hali ambayo Rais Vladimir Putin wa Russia alishasisitiza mara kadhaa kuwa hatua ya nchi za Magharibi ya kutumia makombora yake ya masafa marefu kuishambulia Russia inamaanisha kuwa nchi wanachama wa NATO, Marekani na nchi za Ulaya zinapigana vita dhidi ya Russia.
Ikiwa imepita zaidi ya miaka miwili ya vita vya Ukraine; Marekani, Uingereza, Canada, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, Japan na pia taasisi za kimataifa zimeipatia ukraine zana za kijeshi, mafunzo na misaada ya kiuchumi yenye thamani ya mabilioni ya dola.