May 23, 2024 11:02 UTC
  • Tuujue Uislamu (19)

Ni matumaini kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji. Tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu

Katika kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 19 ya mfululizo huu tutazungumzia hoja nyingine miongoni mwa hoja za kumtabua Mwenyezi Mungu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Sababu mbalimbali zimetolewa kwa ajili ya kuthibitisha uwepo wa Mungu. Sababu nyingine ya kuthibitisha kuwepo kwa Mungu, ni hii ambayo inaitwa uthibitisho wa asili au kimaumbile.

Uthibitisho wa fitra au maumbile ni sababu dhahiri ya kuthibitisha uwepo wa Mungu. Hoja hii inasisitiza kwamba, fahamu ya ndani na mvuto wa ndani humpeleka mwanadamu kwa Mungu kiasi kwamba, mwanadamu, bila sababu yoyote au hoja, na bila ya ufahamu kwa kawaida ni mwenye kumtafuta Mungu. Kwa kuzingatia hayo, ni kana kwamba kuna wito wa ndani unatoka kwenye ujudi wa wanadamu wote na kuwataka waelekee kwenye asili ambayo ndiyo chimbuko la uumbaji na uhai.

Hisia ya kumtafuta Mungu ndani ya wanadamu pia inatajwa kuwa hisia ya kidini. Kuwepo kwa hisia hii kwa wanadamu kunathibitisha kwamba, mielekeo ya kidini ndani ya uwepo na ujudi wa mwanadamu ina mizizi na kumzingatia Mungu na masuala ya kimaumbile ni mambo ambayo chimbuko lake ni fitra na maumbile ya mwanadamu.

 

Wasomi na weledi wa masuala ya dini wanaamini kwamba, kumzingatia Mungu chimbukko lake ni moja ya hisia zenye kina za kidini ndani ya wanadamu na uwepo wa mwanadamu umechanganyika na hisia hii.

Hapa, inafaa kutaja mambo machache kuhusu masuala ya asili yaani ya kiifitra na kimaumbile na jinsi ya kutofautisha hayo kunako mambo yasiyo ya asili.

Inapasa kusema kwamba, fitra na maumbile ni mtaji wa pamoja wa wanadamu wote. Yaani mambo ya kifitra na kimaumbile ni ya pamoja kwa wanadamu wote, katika zama na sehemu zote.

Kama vile upendo na huba ya mama kwa mtoto wake au urafiki ni jambo zuri kwa mwanadamu. Akina mama wote katika sehemu zote za dunia wanapenda watoto wao tangu zamani, au wanadamu wote wanafurahia kuona mandhari za kupendeza kama vile maua ya rangi kwa rangi na mashamba ya kijani kibichi. Kwa kuwa masuala haya yanatokana na asili na maumbile ya mwanadamu, ni suala la kale na milele na halina mipaka ya kijiografia au kizazi fulani. Ni kwa sababu hii, mambo ya asili na ya kimaumbile ni ya ulimwengu wote na sio maalumu kwa jamii au eneo fulani.

 

Kwa upande wa mambo yasiyo ya kimaumbile hayako hivi na yanabadilika kulingana na mazingira. Mambo kama vile hali ya kijiografia, hali ya kiuchumi, maendeleo ya kisiasa na kijamii, au maadili ya kidini na kitamaduni, huathiri maisha ya binadamu wapende wasipende. Kwa mfano, watu wanaoishi katika maeneo ya ncha ya dunia wanapaswa kuvaa nguo nzito kutokana na hali ya hewa ya baridi, ilhali wanaoishi katika maeneo mengine huvaa nguo za kawaida ili ziendane na hali ya hewa ya maeneo wanauoishi.

Natija ya mazungumzo yetu haya ni kwamba, kuenea na kupanuka kwa imani ya kumtafuta Mwenyezi Mungu na imani ya kidini miongoni mwa mataifa mbalimbali jambo ambalo lilikuweko tangu karne zilizopita hadi sasa kunaonyesha hamu na shauku ya kumtafuta Mungu nan a hamu ya kutaka din. Kwa hakika hili ni jambo la kawaida miongoni mwa jamii zote za wanadamu.

Ayatullah Hossein Mazaheri, mwanafikra na mwanazuoni wa kidini, anasema kuhusiana na maudhui hi kwamba:

Maana na makusudio ya uthibitisho wa maumbile ni kwamba, ikiwa mtu ataacha hurafa na ushirikina, akapuuza sababu katika ulimwengu huu, na akajiweka mbali na mambo maovu na sifa mbaya basi, atampata Mungu. Hii ndio maana ya hoja ya kifitra na kimaumbile. Hali hii hutokea katika mikwamo kwa watu wote na kwa kila mtu, iwe ni wale wanaomkubali Mungu au wasiomkubali. Hata wale wanaotoa hoja za kutokuwepo kwa Mungu na wale ambao katika umri wao wote wamekanusha kila kitu kwa ukaidi, wanamkuta Mungu na kumhitajia katika mazingira ya mkwamo na mazonge.

Muda wa kipindi hiki kwa leo umefikia tamati, tukutane tena katika sehemunyingine ya mfululizo huu. Kwaherini.