Ureno pia kulitambua taifa la Palestina
Serikali ya Ureno pia imetangaza uamuzi wake wa kuitambua Palestina wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa mwezi ujao wa Septemba.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Ureno imetangaza kwamba, serikali yake itashauriana na Rais na Bunge (Ureno) kwa lengo la kutambua rasmi Palestina katika Umoja wa Mataifa wakati wa mkutano ujao wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi ujao wa Septemba. Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu wa Ureno imesema kuwa, Lisbon inakusudia kulitambua Taifa la Palestina ndani ya fremu ya hatua inayowezekana wakati wa kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Taarifa hiyo imesema uamuzi huo umechukuliwa baada ya kuwepo mawasiliano mengi na washirika wake, hasa kwa kuzingatia matukio yanayotia wasiwasi sana kuhusu mzozo wa Palestina, katika ngazi ya kibinadamu na marejeo ya mara kwa mara (ya utawala wa Kizayuni) ya kuziunganisha ardhi za Palestina kwa Israel (Palestina inayokaliwa kwa mabavu).
Rais wa Ureno pia, katika kuthibitisha uamuzi wa serikali, amesema kuwa serikali imechukua njia ya tahadhari, yenye malengo na iliyopangwa kwa kushauriana na washirika wa Ulaya na wengine. Hayo yanajiri katika hali ambayo, Markk Carney Waziri Mkuu wa Canada ametangaza kuwa nchi hiyo imepanga kuitambua rasmi nchi ya Palestina katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwaka huu.
Awali, Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer pia alisema Jumanne wiki hii kwamba atalitambua taifa la Palestina mwezi Septemba ikiwa utawala wa Israel hautakubali kusitishwa vita huko Gaza na kutumwa misaada ya kibinadamu katika ukanda huo.
Hivi karibuni pia Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alisema kuwa Paris itaitambua rasmi nchi ya Palestina na kwamba itatangaza rasmi uamuzi huu katika Mkutano wa Baraza Kuu la UN mwezi Septemba.