Mfumuko wa bei Kenya waongezeka kwa asilimia 4.1, wachambuzi waonya
Mfumuko wa bei nchini Kenya umeongezeka hadi asilimia 4.1 mwezi Julai, kiwango cha juu zaidi katika miezi mitatu, kutokana na kupanda kwa bei ya vyakula, vinywaji visivyolewesha, usafiri, makazi na huduma za matumizi ya nyumbani.
Takwimu za Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) zinaonyesha kuwa kiwango hiki cha Julai kinalingana na kile cha Aprili, kikionyesha ongezeko kutoka asilimia 3.8 miezi ya Mei na Juni.
“Ongezeko hilo la bei limechangiwa zaidi na kupanda kwa bei za bidhaa katika kundi la chakula na vinywaji visivyo na kileo (asilimia 6.8), usafiri (asilimia 4.1), na makazi, maji, umeme, gesi na kawi nyinginezo (asilimia 1.3) kwa kipindi cha mwaka mmoja,” KNBS ilisema.
Ingawa mfumuko wa bei wa asilimia 4.1 bado uko ndani ya lengo la serikali la kati ya asilimia 2.5 na 7.5, wachambuzi wameonya kuwa endapo ongezeko la bei ya mafuta litaendelea, huenda mfumuko wa bei ukaongezeka zaidi.
Mwezi uliopita serikali ilifichua kuwa hazina ya ruzuku ya kupunguza bei ya mafuta ilikuwa imeisha, hali iliyowaacha watumiaji katika hatari ya mabadiliko ya bei duniani ambayo yamesababisha gharama ya dizeli na petroli kupanda kwa angalau Sh 8.67 kwa lita.
Kwa miezi miwili mfululizo tangu Mei, serikali ya Kenya haijaweza kutumia ruzuku hiyo, hali ambayo imesababisha kupanda kwa gharama ya bidhaa nyingi kama vile usafiri, chakula na kawi.