…SB/Tuujue Uislamu (20)
Ni matumainii kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji. Tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu.
Tulisema katika kipindi kilichopita kwamba, uthibitisho wa fitra au maumbile ni sababu dhahiri ya kuthibitisha uwepo wa Mungu. Hili linasisitiza hoja kwamba, fahamu ya ndani na mvuto wa ndani humpeleka mwanadamu kwa Mungu kiasi kwamba, mwanadamu, bila sababu yoyote au hoja, na bila ya ufahamu kwa kawaida ni mwenye kumtafuta Mungu na kumtafuta Mungu. Kwa msingi huo, kile ambacho Manabii wa wa Allah walikuja nacho, kwa hakika ndicho mwanadamu anachotafuta kulingana na asili yake. Karibuni kutegea sikio sehemu ya 20 ya mfululizo huu.
Kabla ya kuendeleza maudhui ya teolojia na kumtafuta Mungu kama muelekeo wa kimaumbile wa wanadamu, ni muhimu kukumbusha nukta kadhaa kuhusu mielekeo ya kimaumbile. Asili na hali ya kimaumbile ya mwanadamu na mambo ambayo amepatiwa na Mwenyezi Mungu na hayapatikani kwa kuyatafuta na kuyapata. Kwa maana kwamba, hakuna sababu ya nje ambayo ina nafasi na mchango katika uwepo au kutokuwepo kwa hayo na wakati huo huo, mambo ya nje yana taathira katika kukua au kuzorota kwa hayo.
Jambo jingine ni kwamba, mielekeo ya kimaumbile imeenea na ni ya wote. Kwa maana kwamba wanadamu wote bila ubaguzi wana mielekeo hii na kimsingi mwanadamu ameumbwa na vitu hivi. Kwa hivyo, mambo haya hayana uhusiano na zama au sehemu maalumu.
Hata hivyo, baadhi ya watu wanaweza kuwa wameghafilika na mielekeo ya asili au hata kuikataa, lakini hii haimaanishi kwamba mielekeo hii haipo kwa wanadamu. Yumkini mtu akachagua njia ambayo asili yake safi ikazimwa chini ya kiburi na wingu la uongo, lakini asili ya mwanadamu haipotei kamwe na kujionyesha mara kwa mara na chini ya hali zinazofaa.
Sifa nyingine ya mielekeo ya asili na kimaumbile ni kwamba, jambo hili linaweza kupatikana kupitia tajiriba na uzoefu wa ndani. Kwa maana kwamba, endapo mwanadamu atatafakari kidogo atayaona hayo yakiwa katika uwepo wake. Kwa mfano, ili kufafanua suala hili, je, mtu kiasili anapenda uaminifu na kusema kweli au uongo? Njia moja ni kurejelea dhamiri na nafsi zetu. Kulingana na uzoefu wetu wa ndani, tunapata kwamba tuna mielekeo ya kuwa wakweli na waaminifu.
Mambo ya kimaumbile na kiasili yote ni kheri. Hivyo basi baina ya mambo ya kimaumbiile ya mwanadamu, hakuna shari na uovu na hakuna uovu wowote wenye mizizi na chimbuko la kimaumbile. Ingawa vitendo viovu na vya kikatili ni ni mambo yaliyoenea sana miongoni mwa wanadamu, lakini vitendo hivi kwa hakika havitokani na asili ya mwanadamu. Hata watu makatili na madhalimu kabisa wanapenda kuzungumzia haki na uadilifu wa kijamii na kutambuliwa mbele ya umma kuwa ni watu wema na wanaopigania uadilifu.
Hatua ya mwanadamu ya kushikamana mno na masuala ya kimaada na kukumbatia dunia sambamba na kufanya kila awezalo kutekeleta matakwa na matamanio ya mwili ni mambo ambayo humzuia kuchaua na kukua ile hali ya kifitra na kimaumbile. Ndio maana mtu ambaye ataachana na haya kwa hiari au bila hiari huwa rahisi kwake kumpata Mwenyezi Mungu.
Kwa maneno mengine ni kuwa, ikiwa mtu atajipata katika hali ambayo matumaini yake yamekatikiwa mbali na vitu vya kimaada na akajihisi kukata tamaa na kwamba hana kimbilio, vizuizi huondoka kwenye asili na maumbile yake na kujiona ana mawasiliano na chimbuko asili yaani Mwenyezi Mungu.
Qur'an inaashiria hilo katika Aya ya 65 ya Surat Ankabut kwa kusema:
Na wanapo panda katika marikebu, humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafia ut'iifu. Lakini anapo wavua wakafika nchi kavu, mara wanamshirikisha.
Imekuja katika riwaya ya kihistoria kwamba, siku moja mtu mmoja alikwenda kwa Imam Jafar Sadiq (a.s.) na kumwambia: Mijadala na mabishano kuhusu kuwepo Mwenyezi Mungu yamenishangaza na kunistaajabisha, nielekeze kwa Mwenyezi Mungu. Imam Swadiq akasema: Je, umewahi kupanda meli? Akajibu: Ndiyo. Imam akasema: Je, imewahi kutokea kwamba meli ikapigwa na tufani na ukawa huna njia ya kujiokoa katikati ya mawimbi? Akasema: Ndiyo. Imam Sadiq (a.s.) akamuuliza: Wakati ule ulipokuwa umepoteza matumaini kutoka kila mahali, je, hukutarajia mtu kukuokoa? Alisema: Ndiyo, moyo wangu ulikuwa safi na nilijua kwamba mwishowe, kuna nguvu itatuokoa. Imamu Sadiq (AS) akasema: Basi nguvu hiyo ndio Mwenyezi Mungu ambaye huokoa wakati hakuna mwokozi. Kwa leo tunakomea hapa tukutane tena wakati mwingine.