May 23, 2024 11:03 UTC
  • Tuujue Uislamu (21)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu.

Katika sehemu ya 21 ya mfululizo huu tutabainisha badhi ya sifa za Mwenyezi Mungu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Hakika ya kwanza na muhimu zaidi kuhusiana na Mwenyezi Mungu ni kwamba, Yeye ni Mungu Mmoja tu anayepaswa kupwekeshwa. Dini zote za mbinguni zinatilia mkazo juu ya Tawhidi yaani kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Katika dini ya Uislamu pia, Tawhidi ni msingi miongoni mwa mizizi mitano ya dini yaani (Usul Din). Maana ya Tawhidi ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika ibada, kumuabudu yeye peke yake, bila ya kumshirikisha na kitu chochote na kuamini kwamba, Mwenyezi Mungu hana mshirika wala mfano wake. Kwa mujibu wa wanazuoni na wasomi wa Kiislamu, Tawhidi (kumpwekesha Mwenyezi Mungu) ni mkabala wa shirki na kumshirikisha Mwenyezi Mungu ambako Qur'ani inasema kuwa, kufanya hivyo ni dhulma kubwa na ni dhambi isiyo na msamaha. Kukiri kwamba, Mungu ni mmoja na hana mshirika ni sharti la kwanza kwa mtu anayesilimu na kuingia katika dini ya Uislamu. Kwa maneno mengine ni kuwa, ibara isemayo: Laa Ilaha Illallah yaani Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu" ni maneno ya kwanza anayopaswa kutamka mtu anayetaka kusilimu na kuingia katika Uislamu. Hata hivyo, kutamka huku kwa ulimi kunapaswa kuambatana na kukiri kwa moyo. Nidhamu na mfumo wa kiitikadi na kiakhlaqi yaani kimaadili imesimama juu ya mzizi au msingi wa Tawhidi. Fauka ya hayo, sheria, adabu na mafundisho ya dini ya Kiislamu chimbuko lake ni moyo wa Tawhidi. Nara na kaulimbiu ya Tawhidi imekumbushwa katika kalibu ya ibara  nzuri tofauti katika Aya za Qur'ani Tukufu.

 

Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 18 ya Surat al-Imran

Mwenyezi Mungu, na Malaika, na wenye ilimu, wameshuhudia kuwa, hakika hapana Mungu ila Yeye, ndiye Mwenye kusimamisha uadilifu; hapana Mungu ila Yeye Mwenye nguvu na Mwenye hikima.

Mtume Muhammad (saw) pia kwa amri ya Mwenyezi Mungu alitangaza wazi na bayana kwamba, ajenda kuu ya risala na ujumbe wake ni kuwaita na kuwalingania watu Tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Aya ya 36 ya Surat al-Raad inasema:

Sema: Nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu, na wala nisimshirikishe. Ninalingania Kwake Yeye na marejeo ni Kwake.

Wapenzi wasikilizaji ili kuweka wazi maudhui hii, tunataja hoja kadhaa kuhusiana na Tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu.

Mosi, moja ya hoja za kuthibitisha Tawhidi ni suala la umoja na uratibu katika nidhamu na mpangilio wa uumbaji. Kuweko nidhamu madhubuti katika ulimwengu huu ni hoja ya kuthibitisha ukweli huu kwamba, viumbe vyote chimbuko lao ni moja. Nidhamu na mpangilio huu iwe ni kuchomoza na kuzama kwa jua, kuonekana, nyota, muonekano wa mbingu, ardhi, uhai wa mwanadamu na mpangilio wa viungo vyake na kila kimoja na kazi yake na kadhalika, ni jambo linalothibitisha juu ya kuweko Muumba mmoja tu, kwani kinyume na hivyo mambo yasingekuwa katika mpangilio huu. Aya ya 22 ya Surat al-Anbiyaa inaashiria hilo kwa kusema:

Lau wangeli kuwamo humo Miungu wengine isipo kuwa Mwenyezi Mungu, basi bila ya shaka hizo mbingu na ardhi zingelifisidika. Subahana 'Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu, Bwana wa A'rshi (Kiti cha Enzi), na hayo wanayoyazua.

 

Jambo jingine ni kuwa, kuna wakati fitra na maumbile ya mwanadamu ya kumtafuta na kumtaka Mungu humuelekeza upande wa Mungu mmoja. Kama ambavyo mwanadamu humpata Mungu kwa kutumia taa ya fitra na maumbile, vivyo hivyo katika suala la tahwidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, fitra na maumbile ya mwanadamu humsaidia katika hili.

Kwa mujibuuwa kanuni na msingi wa tauhidi katika Uislamu, Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye uwezo mkuu na mwenye taathira katika ulimwengu, kwa namna ambayo ni mkamilifu na yuko mbali na aina yoyote ile ya kasoro. Elimu na ujuzi wake unazunguka kila kitu na hakuna siri katika ulimwengu au tukio katika kona ya dunia ambalo linatokea na Yeye akawa halijui. Kwa maana kwamba, hakuna kinachofichika Kwake. Yeye ni Muumba Mwenye kusikia na Mwenye kuona. Anasikia kila mnong'ono na kuona kila kitu. Yeye si mhitaji. Hakuna ukomo wa rehema na fadhili Zake, na wema na uzuri Wake havina mpaka. Mwanadamu mwenye imani na itikadi thabiti kwa Mungu Mmoja wa pekee, akiwa katika dhiki na faraja na katika misukosuko yote ya maisha, humgeukia Muumba ambaye anachunga matendo yake, kwa hiyo anaomba msaada kutoka Kwake na kwa kumtaja na kumdhukuru Allah, mja huyu anapata amani na utulivu. 

Wapenzi wasikilizaji muda umenipa mkono, hivyo leo nakomea hapa. Kwaherini.