Jun 10, 2024 03:25 UTC
  • Jumatatu, 10 Juni, 2024

Leo ni Jumatatu tarehe 3 Mfunguo Tatu Dhul-Hijja 1445 Hijria sawa na tarehe 10 Juni 2024 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 234 iliyopita yaani tarehe 10 Juni 1790 vikosi vya jeshi la Uingereza viliivamia ardhi ya Malaya inayojulikana hii leo kama Malaysia. Wakati huo Uholanzi ilikuwa ikiikoloni Malaya na kupora utajiri mkubwa wa nchi hiyo wa madini ya bati. Uholanzi ilianza kuondoka katika ardhi ya Malaya baada ya jeshi la Uingereza kuingia nchini humo na mwaka 1824 ilikubali kuiachia Uingereza ardhi hiyo kwa sharti kwamba nayo iachiwe Indonesia ambayo ilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Uholanzi. Malaysia ilijipatia uhuru wake mwaka 1957 na Indonesia mwaka 1956. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 212 iliyopita, vilianza vita vya Marekani na Uingereza. Miongoni mwa matukio muhimu ya historia ya Marekani katika nusu ya kwanza ya karne ya 19 ni vita hivyo vilivyoendelea kwa miaka miwili. Sababu ya kuanza vita hivyo inasemekana ni kuzingirwa Ufaransa na Uingereza kutokea baharini na kuzuiwa safari za meli za Marekani katika maji yanayozunguka nchi za Ulaya. Lakini pamoja na hayo Marekani ilikuwa na sababu nyingine za kuanzisha vita hivyo, muhimu kati ya hizo ilikuwa ni madai ya uungaji mkono wa siri wa Uingereza kwa Wahindi Wekundi wa Marekani dhidi ya serikali kuu ya nchi hiyo. Kufuatia vita hivyo, tarehe 18 Juni 1812 wanajeshi wa Marekani walivamia vituo na mali za Uingereza huko Canada na kuuteketeza mji wa Toronto. Vita hivyo vilipamba moto kiasi kwamba mwezi Agosti 1814 Uingereza ilituma askari wake katika pwani ya mashariki ya Marekani na kuendesha vita hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Washington DC. Hatimaye mazungumzo ya amani baina ya nchi mbili hizo yalitiwa saini huko Ubelgiji na kupelekea kusimamishwa vita hivyo mwezi Disemba mwaka huhuo wa 1814. ***

 

Miaka 101 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 73 Pierre Loti, mwandishi mkubwa wa Ufaransa. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi na ya juu, alijiunga na kikosi cha majini katika jeshi la Ufaransa sambamba na kuhudumia nyadhifa kubwa jeshini. Ni wakati huo ndipo alipoanzisha shughuli zake za fasihi huku akieneza machapisho yake. Muda mfupi baadaye Pierre Loti alipata umshuhuri ambapo mwaka 1891 aliteuliwa kujiunga na kituo cha utamaduni nchini humo. Baada ya hapo alifanya safari mashariki ya mbali, safari za baharini na Mashariki ya Kati na kupata kuandika kuhusu mambo mbalimbali duniani. Aidha Loti alifika nchini Iran na kuandika kitabu kuhusiana na mambo ya kuvutia ya mjini Isfahani. Pierre Loti aliacha athari mbalimbali ambazo baadhi zipo hadi leo katika maktaba za nchini Ufaransa. ***

Pierre Loti

 

Miaka 24 Iiyopita siku kama ya leo, Hafidh Assad rais wa wakati huo wa Syria aliaga dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu. Alizaliwa mwaka 1930. Aliteuliwa kuwa kamanda wa kikosi cha anga cha Syria mwaka 1964 na kuwa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo miaka mitatu baadaye. Aliipindua serikali ya wakati huo ya Syria mwaka 1970 na kuchukua uongozi wa nchi hiyo na kisha kuteuliwa kuwa kiongozi wa chama cha Baath. Assad aliimarisha jeshi la nchi hiyo kiasi kwamba mwaka 1973 alifanikiwa kurejesha sehemu ya milima ya Golan iliyotekwa na kukaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel katika vita vya 1967. Siasa muhimu za Assad zilikuwa ni za kutofanya mapatano na utawala huo ghasibu. ***

Tags