Jun 20, 2024 02:49 UTC
  • Alkhamisi, Juni 20, 2024

Leo ni Akhamisi tarehe 13 Mfunguo Tatu Dhulhija 1445 Hijria sawa na tarehe 20 Juni 2024 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 149 iliyopita inayosadifiana na hii ya leo yaani tarehe 20 mwezi Juni mwaka 1875, kisiwa cha Okinawa kinachopatikana katika Bahari ya Pacific huko Japan kilidhibitiwa na jeshi la nchi hiyo.

Hata hivyo mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia kisiwa hicho cha kistratijia chenye ukubwa wa kilomita mraba 1250 kilikaliwa kwa mabavu na majeshi ya Marekani licha ya mapambano makali ya jeshi la Japan.

Jeshi la Marekani liliondoka Japan mwaka 1958 lakini kisiwa cha Okinawa kiliendelea kudhibitiwa na Wamarekani. Mwaka 1972 vikosi vya Marekani vilisitisha ukaliaji wa mabavu wa kisiwa hicho kufuatia mazungumzo marefu kati ya Washington na Tokyo.   

Okinawa

Miaka 112 iliyopita katika siku kama ya leo msomi wa Poland kwa jina la Casimir Funk kwa mara ya kwanza kabisa alifanikiwa kugundua vitamin au virutubisho.

Baada ya uhakiki mwingi Dakta Casimir Funk aligundua kwamba vyakula vinavyotumiwa na mwanadamu vina baadhi ya virutubisho (vitamins) ambavyo japokuwa ni vichache sana lakini vina udharura mkubwa katika ukuaji na usalama wa mwili na akaamua kuvipa jina la Vitamini.

Kuna aina mbalimbali za vitamin kama A, B, C, D na E, na kila moja ina sifa za kipekee na matumizi ya aina yake katika mwili.   

Dakta Casimir Funk

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu, Allamah Agha Bozorge Tehrani. Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu.

Allamah Agha Bozorge Tehrani alikweya kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa kidini. Allamah Tehrani alisafiri na kufanya uchunguzi katika maktaba nyingi za nchi kama Iran, Misri, Syria, Iraq, Hijaz, Palestina na kadhalika kwa ajili ya kutayarisha ensaiklopedia ya vitabu vya Kiislamu. Alifanikiwa kuandika tabu hilo kubwa lenye juzuu 26 ambalo alilipa jina la "Adhari'a ila Tasaanifish Shia". Kitabu kingine muhimu cha Allamah Agha Bozorge Tehrani ni "Tabaqatu Aalami Shia" chenye juzuu 8. 

Allamah Agha Bozorge Tehrani (katikakti)

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita inayosadifiana na tarehe 31 Khordad 1360 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 21 Juni mwaka 1981, aliuawa shahidi Dakta Mustafa Chamran, msomi na kamanda shujaa wa vikosi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran.

Dakta Chamran alifanikiwa kupata shahada katika fani ya elektroniki na kisha alielekea Marekani ambako alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu.

Kwa miaka kadhaa Dakta Chamran alikuwa nchini Lebanon kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo waliokuwa wakipambana na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Dakta Chamran alichaguliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na kisha akawa mbunge wa Tehran.

Dakta Mustafa Chamran

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, inayosadifiana na 31 Khordad 1369 Hijria Shamsia, mikoa ya Gilan na Zanjan iliyoko kaskazini na kaskazini magharibi mwa Iran ilikumbwa na mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na 7.3 kwa kipimo cha Rishta, na kusababisha maafa makubwa.

Zaidi ya watu elfu hamsini walifariki dunia na wengine zaidi ya elfu sitini kujeruhiwa, na laki tano kukosa makaazi. Mtetemeko huo licha ya maafa yake makubwa kwa binadamu, ulisababisha hasara kubwa ya kiuchumi kwa wananchi na serikali, hasa kwenye miundombinu.

Athari za mtetemko uliokumbwa mikoa ya mikoa ya Gilan na Zanjan ya nchini Iran miaka 34 iliyopita