Alkhamisi, Julai 4, 2024
Leo ni Alkhamisi tarehe 27 Mfunguo Tatu Dhulhija 1445 Hijria sawa na tarehe 4 Julai 2024 Milaadia.
Tarehe 14 Tir katika kalenda ya Iran imepewa jina la Siku ya Kalamu.
Kwa hakika kalamu huhifadhi elimu, maarifa na ni mlinzi wa fikra za wanazuoni na wasomi na hivyo ni kiunganishi cha kifikra na daraja la mawasiliano baina ya watu wa zamani na wa leo. Hata mawasiliano baina ya mbingu na ardhi yamepatikana kupitia kalamu.
Hivyo basi kalamu ni mtunza siri wa mwanadamu na hazina ya elimu na mkusanyaji wa tajiriba za karne nyingi. Na kama tunaona katika Qur’ani Mwenyezi Mungu ameapa kwa kalamu kwa kusema: "Nuun. Naapa kwa kalamu na yale wayaandikayo". Hilo linatokana na umuhimu wa kalamu, kwani kiapo mara nyingi hufanywa kwa jambo au kitu ambacho kina thamani na chenye hadhi na heshima kubwa.

Katika siku kama ya leo miaka 248 iliyopita, yaani tarehe 4 Julai mwaka 1776 wawakilishi wa majimbo 13 ya awali ya Marekani walisaini "Azimio la Uhuru" wa nchi hiyo katika mji wa Philadelphia.
Ardhi ya Marekani kwa maelfu ya miaka ilikuwa makazi ya Wahindi Wekundu. Mwishoni mwa karne ya 15 wavumbuzi wa Ulaya waliwasili Marekani na nchi mbalimbali za Ulaya zikavamia na kukalia kwa mabavu kila eneo la nchi hiyo.
Wazungu hao wa Ulaya waliandamana na mamilioni ya watumwa kutoka Afrika ambao walitumiwa katika kazi ngumu za mashambani na viwandani.

Miaka 78 iliyopita katika siku kama ya leo, visiwa vya Ufilipino vilijitangazia uhuru kutoka kwa Marekani.
Fernando Magellan mvumbuzi wa Kireno pamoja na wenzake ndio waliokuwa Wazungu wa kwanza kutoka Ulaya kuwasili katika ardhi ya Ufilipino na hiyo ilikuwa mwaka 1521. Katika kipindi cha nusu karne baadaye, Uhispania ikawa imeidhibiti ardhi yote ya nchi hiyo.
Mkoloni Muhispania alipora mali na utajiri wa Ufilipino kwa muda wa karne tatu.

Na katika siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, Ayatullah Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah mmoja wa maulama mashuhuri na marja taqlidi wa Kiislamu alifariki dunia.
Allama Fadhlullah alizaliwa mwaka 1935 katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq katika familia ya kidini yenye asili ya Lebanon. Sayyid Fadhlullah alianza kujifunza elimu ya dini katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Najaf, Iraq akiwa bado kijana mdogo. Alijishughulisha na uandishi wa makala na vitabu na alikuwa mshairi.
Ayatullah Fadhlullah alikuwa miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah, na jambo hilo liliikasirisha sana Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ambazo zilifanya majaribio kadhaa ya kutaka kumuua.
Ayatullah Muhammad Hussein Fadhlullah ameandika vitabu vingi vya thamani ikiwemo tafsiri ya Qur'ani ya "Min Wahyil Qur'an."
