Jumapili, Julai 17,2016
Leo ni Jumapili tarehe 12 Shawwal mwaka 1437 Hijria, inayosadifiana na tarehe 17 Julai 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1053 iliyopita, yaani sawa na tarehe 12 Shawwal mwaka 384 Hijiria, alifariki dunia Ibrahim Bin Hilal Sabi, mtaalamu wa fasihi na malenga maarufu wa karne ya nne Hijiria. Sabi alizaliwa mjini Baghdad, Iraq ambapo alitokea kuwa na uhodari maalumu katika fani ya mashairi na fasihi. Mwandishi huyo mashuhuri, alitabahari pia katika uga wa elimu za hisabati, nujumu na uhandisi. Kuna athari kadhaa kutoka kwa Ibrahim Bin Hilal Sabi, baadhi zikiwa ni 'Risala katika Elimu ya Pembe Tatu' na 'Risalah katika Elimu ya Nujumu.'
Siku kama ya leo miaka 407 iliyopita, alifariki dunia mjini Isfahan, Iran Bahaud-Din Muhammad Bin Hussein Amili, maarufu kwa jina la Sheikh Bahai, alimu maarufu wa Waislamu wa elimu ya sheria, mataalamu wa nyota na hisabati. Sheikh Bahai alizaliwa mjini Baalbek, Lebanon mwaka 952 Hijiria katika familia ya Kiirani. Baba yake alikuwa miongoni mwa viongozi na masheikh wakubwa wa zama hizo. Kwa kuwa na maandalizi ya kielimu msomi huyo aliweza ndani ya kipindi kifupi kufikia daraja la ualimu, huku akibobea pia katika elimu za fiqhi, tafsiri ya Qur'an, hadithi, hisabati, nyota, fasihi na historia. Kuna vitabu kadhaa vya thamani vinavyonasibishwa na msomi huyo ambavyo wataalamu wa historia wameviorodhesha na kufikia 100. Baadhi ya vitabu hivyo ni pamoja na 'Jamiu Abbasi' 'Kashkuul' 'Hablul-Matin' 'Tashriihul-Aflaak' na 'Khulaswatul-Hisaab.'
Siku kama ya leo miaka 226 iliyopita, alifariki dunia Adam Smith, mwanafalsafa na mtaalamu wa uchumi wa Scotland. Smith alizaliwa mwaka 1723 Miladia huko Scotland na baada ya kuhitimu masomo ya sekondari akajiunga na Chuo Kikuu cha Glasgow na kisha cha Oxford ambapo baadaye alichaguliwa kuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Glasgow. Sanjari na kufundisha falsafa chuoni hapo, Adam Smith alijishughulisha na utafiti katika masuala ya uchumi na kufanikiwa kuandika kitabu cha 'Utafiti juu ya aAsili na Chanzo cha Utajiri.' Ni kwa ajili hiyo ndio maana akaitwa jina la baba wa elimu ya uchumi wa sasa.
Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita Profesa Roger Garaudy, mwanafalsafa na mwanafikra wa Ufaransa alizaliwa huko katika mji wa Marseille. Garaudy alipata shahada ya udaktari katika taaluma tatu za masomo ya falsafa, fasihi na utamaduni. Roger Garaudy alifungwa jela katika kambi ya mateka wa kivita wa Ujerumani tangu mwaka 1940 hadi 1943 kutokana na mapambano yake dhidi ya ufashisti wa Adolph Hitler wakati Ufaransa ilipokaliwa kwa mabavu na Ujerumani. Profesa Garaudy alikuwa mwanachama wa chama cha Kikomonisti cha Ufaransa kwa miaka 36 na pia mwanachama wa kamati kuu ya chama hicho kwa miaka 25. Hata hivyo mitazamo ya kikomunisti na kiliberali haikuweza kukata kiu ya kutafuta ukweli ya msomi huyo wa Ufaransa na hatimaye alikubali dini ya tukufu ya Kiislamu baada ya kufanya utafiti mkubwa. Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwaka 1979 ulikuwa na taathira kubwa katika mitazamo ya Profesa Roger Garaudy.
Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, chama cha Baath cha Iraq kilichukua hatamu za uongozi kupitia mapinduzi yaliyoongozwa na Ahmad Hassan al Bakr na kumpindua Rais Abdulrahman Aarif. Baada ya kuchukua madaraka chama cha Baath, Saddam Hussein ambaye alikuwa kiongozi nambari mbili wa chama hicho alianza kuwaua wapinzani wake nchini Iraq na vikosi vya usalama na vya jeshi la nchi hiyo pia vikaanzisha hujuma kali dhidi ya Wakurdi wapinzani, wazalendo, wanaharakati wa Kiislamu na hata Wakomonisti.
Na siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikubali azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lilizitaka nchi mbili za Iran na Iraq kusimamisha vita. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ililikubali azimio hilo kutokana na sifa chanya za baadhi ya vipengee vyake hususan vifungu vilivyokuwa vikihusiana na suala la kuarifishwa nchi vamizi na udharura wa Iran kulipwa fidia. Hata hivyo utawala wa zamani wa Iraq ulilipinga azimio hilo ambapo uliendelea na mashambulizi yake dhidi ya Iran hadi pale usitishaji vita rasmi ulipotekelezwa yaani mwezi Mordad mwaka 1367 Hijria Shamsia sawa na mwezi Agosti mwaka 1988.