Jul 19, 2024 03:37 UTC
  • Ijumaa, tarehe 19 Julai, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 13 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 19 Julai 2024.

Siku kama ya leo miaka 1385 iliyopita, yaani sawa na tarehe 13 Muharram mwaka wa 61 Hijria Abdullah bin Afif aliuawa shahidi na gavana wa Yazid bin Muawiya, Ubaidullah bin Ziad.

Bin Afif alikuwa mtu wa kwanza kuanzisha malalamiko na upinzani wa waziwazi dhidi ya jinai za Ubaidullah bin Ziad za kumuua shahidi mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein (as) na wafuasi wake. Baada ya Ubaidullah bin Ziyad kuwashambulia kwa maneno makali na kuwavunjia heshima mateka wa Karbala waliokuwa wamepelekwa katika majlisi yake, Abdullah bin Afif ambaye alikuwa miongoni mwa wacha-Mungu wakubwa wa mji wa Kufa huko Iraq na wafuasi wa kweli wa Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as), alikerwa mno na mwenendo huo wa gavana wa Yazidi wa kuwavunjia heshima Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) na kumjibu mtawala huyo kwa hasira.

Ubaidullah ambaye hakutarajia kuona majibu kama hayo baada ya kuua watu wa Nyumba ya Mtume (saw) alitoa amri ya kukamatwa Afif na kupelekwa kwake. Hata hivyo watu wa kabila lake walizuia kitendo hicho. Askari wa utawala wa Bani Umayyah walivamia nyumba ya Abdullah bin Afif usiku na kumtoa nje kisha wakamuua shahidi kwa kumkatakata kwa mapanga.   

Miaka 131 iliyopita alizaliwa malenga wa Russia kwa jina la Vladimir Mayakovsky.

Mashairi ya Mayakovsky yalikuwa na nafasi kuu wakati wa mapinduzi ya Kikomonisti ya Urusi ya zamani mwaka 1917.

Vladimir Mayakovsky alikuwa akiamini kuwa fasihi inapasa kuwa lugha ya watu wengi na inayobainisha maisha yao ya kijamii.

Vladimir Mayakovsky

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, nchi ya Laos iliyopo katikati mwa Asia, ilipata uhuru kutoka kwa Ufaransa.

Nchi ya Laos yenye milima mingi, ipo baina ya Vietnam, Cambodia, Thailand, Myanmar na China huku ikiwa na jamii ya watu milioni tano. Kwa miaka mingi, nchi hiyo ilikuwa ikitawaliwa na uongozi wa kifalme. Mji mkuu wa nchi hiyo Vientiane una ukubwa wa kilometa 237 huku ukiwa kando ya mto maarufu wa Mekong.

Laos haipakani na bahari yoyote, na chanzo chake kikuu cha maji ni mto huo wa Mekong.   

Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, Kuwait ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza.

Katika kipindi cha utawala wa Achaemenid, Kuwait ilikuwa ikihesabiwa kuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Mwaka 1899 Miladia, Kuwait iliwekeana saini na Uingereza, suala lililoifungulia London mlango wa kuikoloni nchi hiyo. Mwenendo huo uliendelea hadi baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Kuwepo kwa visima vya mafuta kulipanua uingiliaji mkubwa wa mashirika mengi ya Uingereza na Marekani katika taifa hilo.

Hatimaye mwaka 1961 Kuwait na Uingereza zilitiliana saini makubaliano yaliyoifanya nchi hiyo kujipatia uhuru wake.

Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo mapinduzi ya wananchi wa Nicaragua yalipata ushindi dhidi ya dikteta Anastasio Somoza wa nchi hiyo na muitifaki wake mkubwa yaani Marekani.

Dikteta huyo kibaraka wa Marekani alichukua hatamu za uongozi wa Nicaragua mwaka 1967 na tangu wakati huo wimbi kubwa la upinzani lilianza kuenea nchini kote na katika America ya Kati dhidi ya kiongozi huyo. Mapambano ya silaha ya wapiganaji wa msituni ya Harakati ya Ukombozi wa Kitaifa ya Sandinista (FSLN) yaliyoanza mwaka 1963 yalipamba moto zaidi katikati ya muongo wa 1970 na kuungwa mkono na wananchi.

Hatimaye Somoza alilazimika kukimbia nchi baada ya jeshi la Sandinista kuingia Managua mji mkuu wa Nicaragua katika siku kama ya leo. Karibu watu elfu 40 waliuawa katika mapinduzi ya Nicaragua. 

Na siku kama hii ya leo miaka  37 iliyopita liliidhinishwa azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu haja ya kumalizwa vita vya Iran na Iraq.

Azimio hjilo lilijumuisha vifungu 10 ambavyo vilipasishwa kwa kauli moja na wanachama 15 wa Baraza la Usalama.

 

Tags