Jul 21, 2024 02:31 UTC
  • Jumapili, 21 Julai, 2024

Leo ni Jumapili tarehe 15 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria mwafaka na tarehe 21 Julai 2024 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1093 iliyopita, yaani tarehe 15 Muharram mwaka 353 Hijiria, alifariki dunia Ibn Sakan mwanazuoni na mpokezi mashuhuri wa hadithi wa karne ya nne Hijiria. Ibn Sakan alizaliwa mwaka 294 Hijiria huko mjini Baghdad, Iraq ambapo alisafiri katika nchi mbalimbali kwa ajili ya kutafuta elimu. Ibn Sakan alikusanya hadithi nyingi katika miji ya nchi kama Uzbekistan, Tajikistan, Kazakhstan Kyrgyzstan (Transoxiana), Khorasan, Iraq, Sham na Misri na mwishowe akaweka makazi yake nchini Misri. Mpokezi huyo wa hadithi ameacha athari nyingi na mojawapo ni kitabu cha historia kinachohusu maswahaba wa Mtume SAW, kinachoitwa Al Huruf fi Al -Swahaba. ***

 

Katika siku kama ya leo, miaka 857 iliyopita, sawa na tarehe 15 Muharram mwaka 589, alizaliwa Ali bin Mussa bin Ja'far maarufu kwa jina la Ibn Twaus, faqihi, mpokezi wa hadithi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika eneo la Hillah nchini Iraq. Ibn Twaus alipitisha kipindi cha utotoni katika mji huo na baadaye alihamia mjini Baghdad ambako aliishi kwa kipindi cha karibu miaka 15. Ibn Twaus alipata umashuhuri mkubwa katika elimu na ucha-Mungu na ameandika vitabu vingi ambavyo ni marejeo ya taaluma za Kiislamu. Kitabu mashuhuri zaidi cha msomi huyo ni "al Luhuuf" ambacho ndani yake alizungumzia kwa namna bora zaidi matukio ya Siku ya Ashura na harakati ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) katika medani ya vita vya Karbala. Kitabu kingine mashuhuri cha mwanazuoni huyo ni "Al Iqbal". Ibni Twaus alifariki dunia mwaka 664 akiwa na umri wa miaka 75. ***

 

Siku kama ya leo miaka 145 iliyopita John Boyd Dunlop raia wa Uingereza, alikuwa mvumbuzi wa kwanza wa gurudumu. Dunlop alifikia hatua ya kuvumbua gurudumu la magari baada ya utafiti wa miaka kadhaa. Alifariki dunia 1921.   ***

John Boyd Dunlop

 

Katika siku kama ya leo miaka 125 iliyopita, yaani sawa na tarehe 21 Julai mwaka 1899, alizaliwa mwandishi mtajika wa Kimarekani kwa jina la Ernest Hemingway. Kwa muda fulani Hemingway alikuwa mwandishi huko Uingereza na Ufaransa. Hemingway alianzisha mbinu ya kuandika riwaya na tungo fupi fupi na alikuwa akitumia lugha nyepesi na inayoeleweka kwa wepesi. Mwaka 1954 mwandishi Ernest Hemingway alitunukukiwa tuzo ya Nobel katika medani ya fasihi. Hemingway alipendelea sana kuwinda na alitumia muda mwingi katika shughuki hiyo. Alifariki dunia tarehe pili Julai 1961 baada ya kujipiga risasi na bunduki yake mwenyewe ya kuwindia, wakati akiisafisha. Hivyo, mkasa wa kifo cha baba yake ukawa umejirudia kwake baada ya kupita miaka 23. Miongoni mwa vitabu maarufu vya Hemingway ni pamoja na kitabu cha "The Old Man and The Sea", "A Farewell to Arms" na "For Whom The Bell Tolls". ***

Ernest Hemingway

 

Katika siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 21 Julai 1954 ulitiwa saini mkataba wa kuacha vita kati ya Ufaransa na Vietnam na kukomesha ukoloni wa Ufaransa huko India na China mwishoni mwa mkutano wa Geneva. Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya kuanguka ngome imara ya Wafaransa iliyojulikana kwa jina la Dien Bien Phu nchini Vietnam Mei mwaka 1954. Makubaliano ya mkutano wa kimataifa wa Geneva, yalihudhuriwa na wawakilishi wa ngazi za juu kutoka Ufaransa, Marekani, Uingereza, China, Vietnam na Urusi ya zamani. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, vikosi vya kigeni vilipaswa kuondoka Vietnam, lakini Marekani kinyume na makubaliano ya Geneva, ikaamua kutuma majeshi katika eneo hilo kwa lengo la kuzuia kuungana maeneo mawili ya Vietnam ya kaskazini na ya kusini.  ***

 

Tarehe 31 Tir mwaka 1331 Hijria Shamsia yaani miaka 72 iliyopita, Mahakama ya Kimataifa ya The Hague, Uholanzi, ilitoa hukumu ya kutupilia mbali mashtaka ya Uingereza dhidi ya Iran kuhusiana na kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran na kufanywa kuwa mali ya taifa. Bunge la Taifa la Iran tarehe 29 Isfand mwaka 1329 Hijria Shamsia lillikuwa limeitangaza sekta ya mafuta ya Iran kuwa mali ya taifa na kwa utaratibu huo, likawa limekata mikono ya serikali ya Uingereza iliyokuwa ikinufaika na mafuta ya Iran. Uingereza ambayo ilikuwa ikipata faida kubwa kutokana na kupora utajiri wa mafuta wa Iran iliamua kushtaki katika Mahakama ya The Hague. Hata hivyo katika siku kama ya leo, mahakama hiyo ilitupilia mbali mashataka hayo ya Uingereza. ***

Muhammad Musaddeq, Waziri Mkuu wa zamani wa Iran

 

Miaka 36 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, jeshi la mtawala wa wakati huo wa Iraq, dikteta Saddam Hussein lilianza kufanya mashambulio makubwa dhidi ya maeneo ya kusini ya Iran. Mashambulio hayo yalianza siku nne tu baada ya Iran kulikubali azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Azimio hilo lililokuwa limepasishwa takribani mwaka mmoja kabla, lilisisitiza juu ya usitishaji vita, liliuarifisha  utawala vamizi, likataka kulipwa fidia waathiriwa wa hujuma hiyo, kubadilishana mateka mataifa mawili ya Iran na Iraq na kurejea vikosi vya nchi mbili hizo katika mipaka ya kimataifa. Utawala vamizi wa Iraq hapo kabla ulikuwa umelikubali azimio hilo na ulikuwa ukiendesha propaganda dhidi ya Iran kutokana na kutolikubali azimio hilo. Lakini wakati Iran pia ilipotangaza kulikubali azimio hilo, jeshi la dikteta Saddam kwa mara nyingine tena likaishambulia ardhi ya Iran. ***

Azimio 598