Aug 16, 2024 02:26 UTC
  • Ijumaa, Agosti 16, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 11 Mfunguo Tano Safar 1446 Hijria sawa na Agosti 16 mwaka 2024 Milaadia.

Siku kama leo miaka 136 iliyopita, alizaliwa Thomas Edward Lawrence, jasusi mkubwa wa Uingereza aliyekuwa na mchango mkubwa katika kuzidhoofisha nchi za Kiarabu.

Kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia Lawrence, alikuwa amefanya safari katika nchi kadhaa za Kiarabu, ambapo sanjari na kujifunza lugha ya Kiarabu, alifahamu pia tamaduni na maisha ya Waarabu. Katika vita hivyo vya Kwanza vya Dunia vilivyojiri kati ya mwaka 1914 hadi 1918, na kwa msingi wa siasa za kikoloni za Uingereza, Lawrence alifanya njama kubwa kuyachochea makabila ya Kiarabu kwa kisingizio cha kutaka kujitawala, ili yaweze kujitenga mbali na utawala wa Othmania ambao katika vita hivyo ulikuwa ukikabiliana na Uingereza.

Aidha Thomas Edward Lawrence alikuwa na nafasi pi aya kuuingiza madarakani ukoo wa Aal-Saud nchini Saudia, suala ambalo lilipelekea kupata umashuhuri mkubwa nchini Saudia.   

Thomas Edward Lawrence

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, kisiwa cha Cyprus kilipata uhuru baada ya machafuko ya miaka kadhaa.

Kisiwa hicho ambacho hii leo kinaendeshwa chini ya mfumo wa jamhuri, kiko katika bahari ya Mediterraneanna kusini mwa Uturuki kikiwa na ukubwa wa zaidi ya kilomita mraba 9000. Kwa miaka kadhaa kisiwa cha Cyprus chenye historia kongwe na muhimu katika eneo kilikuwa chini ya falme za Iran, Ugiriki, Misri na utawala wa Othmania.

Lakini mwaka 1878, utawala wa  Othmania ulikabidhi usimamizi wa kisiwa hicho kwa Uingereza katika mkutano uliofanyika mjini Berlin Ujerumani na mwaka 1925 kisiwa cha Cyprus kikawa rasmi koloni la Uingereza.   

Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita, inayosadifiana na 16 Agosti 2003, alifariki dunia kiongozi wa zamani wa Uganda, Idi Amin Dada akiwa uhamishoni nchini Saudi Arabia.

Idi Amin alilazwa katika hospitali ya Mfalme Feisal mjini Jeddah kwa wiki kadhaa kabla ya kupatwa na umauti katika siku kama ya leo. Idi Amin alichukua madaraka ya Uganda mwaka 1971 baada ya kumpindua Milton Obote na aliongoza nchi hiyo hadi mwaka 1979, alipoondoshwa madarakani na majeshi ya Tanzania.

Idi Amin ambaye aliwahi kuwa bingwa wa masumbwi katika uzito wa juu nchini Uganda, aliwahi pia kuwa mkuu wa majeshi ya Uganda mwaka 1966 chini ya Rais Obote. Baada ya majeshi ya Uganda kupata kipigo mbele ya majeshi ya Tanzania, Amin alilazimika kuikimbia nchi hiyo na kukimbilia Libya, kisha Iraq na hatimaye Saudi Arabia.     

Idi Amin Dada

Tarehe 26 Murdad miaka 34 iliyopita kundi la kwanza mateka wa Kiirani waliokuwa wakishikiliwa katika magereza za kutisha za Saddam Hussein liliwasili katika ardhi ya Iran.

Kuachiwa huru mateka hao ilikuwa hatua muhimu ya kutekelezwa azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kati ya Iran na Iraq.

Saddam Hussein ambaye wakati huo alikuwa chini ya mashinikizo kutokana na kuivamia Kuwait alikubali kuwaachia huru mateka hao wa Iran na kurejea katika mipaka inayokubalika kimataifa ya nchi mbili baada ya kukubali mkataba wa mpaka wa Algeria.

Mateka wa vita wa Iran wakirejea nchini