Jul 25, 2026 03:17 UTC
  • Leo katika Historia
    Leo katika Historia

Leo ni Jumamosi 10 Mfunguo Tano Safar 1448 Hijria mwafaka na 25 Julai 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 132 iliyopita, vita kati ya Uchina na Japan vilianza kwa mashambulio yaliyofanywa na vikosi vya jeshi la Japan dhidi ya maeneo ya pwani ya Uchina. Vita hivyo vilitokea baada ya mashambulio yaliyofanywa na Japan kwa lengo la kuiteka ardhi kubwa ya Peninsula ya Korea na kaskazini mwa China. Japan ndiyo iliyoshinda katika vita hivyo kutokana na kujizatiti vyema kwa silaha za kisasa.

***

Katika siku kama ya leo miaka 88 iliyopita, Wapalestina 62 wasio na hatia waliuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa katika milipuko miwili ya mabomu iliyotokea kwa nyakati tofauti katika soko la kuuzia mboga za majani huko Palestina. Makundi ya kigaidi ya Wazayuni ndiyo yaliyotega mabomu hayo mawili na lengo lao lilikuwa kuzusha hali ya machafuko na ukosefu wa amani kwa Wapalestina.

***

Miaka 66 iliyopita katika siku kama ya leo, Ayatullah Sayyid Abdulhadi Shirazi, mmoja wa wanazuoni wakubwa na Marjaa mashuhuri wa Kiislamu, alifariki dunia. Akiwa bado mtoto mdogo, alifiwa na baba yake, hivyo akalelewa chini ya uangalizi wa Mirza Shirazi, ambaye alikuwa mmoja wa jamaa zake wa karibu. Kupitia malezi hayo, tangu utotoni alijifunza misingi ya dini tukufu ya Uislamu. Baadaye alijiunga na Hawza (Chuo KIkuu cha Kidini) ya Najaf, ambako alipata elimu kutoka kwa walimu mashuhuri kama vile Akhund Khorasani na Allama Yazdi. Kupitia juhudi zake katika kutafuta elimu, alifikia daraja za juu za kielimu na kiroho. Kwa muda mrefu, Ayatullah Sayyid Abdulhadi Shirazi alikuwa miongoni mwa walimu wakubwa wa Hawza ya Najaf, akitoa mchango mkubwa katika kuelimisha na kulea kizazi cha wanazuoni.

***

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita mnamo tarehe 3 mwezi Mordad mwaka 1361 Hijria Shamsiya, alifariki dunia Dakta Hamid Inayat, mwandishi na mtarjumi mahiri wa Kiirani. Dakta Hamid alielekea nchini Uingereza baada ya kupata shahada ya chuo kikuu nchini Iran na akiwa huko alihitimu shahada ya udaktari katika taaluma ya uchumi na sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha London. Dakta Hamid Inayat baadaye alirudi Iran na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Tehran. Dakta Inayat ameandika na kutarjumu vitabu vingi vya falsafa na fikra za kisiasa. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni Uislamu na Usoshalisti na Fikra za Kisiasa za Magharibi.

***

 Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilianzisha mashambulizi makubwa ya anga na baharini huko kusini mwa Lebanon. Mashambulizi hayo yalikuwa operesheni kali zaidi ya kijeshi kuwahi kufanywa na Wazayuni dhidi ya Lebanon baada ya mashambulio waliyoyafanya dhidi ya ardhi nzima ya Lebanon mwaka 1982.

***