Aug 17, 2024 22:54 UTC
  • Jumapili, 18 Agosti, 2024

Leo ni Jumapili 13 Mfunguo Tano Safar 1446 Hijria mwafaka na 18 Agosti 2024.

Siku kama ya leo miaka 1371 iliyopita, vilitokea vita vya Ajnadeen katika eneo la Ajnadeen huko Palestina kati ya Waislamu na Warumi. Katika vita hivyo ambavyo havikuwa na mlingano hasa kwa kuzingatia kuwa, askari wa Kirumi walikuwa wengi mara kadhaa kuliko Waislamu, jeshi la Waislamu liliibuka na ushindi mkubwa kutokana na wapiganaji wake kuwa na irada na imani thabiti. Baada ya Warumi kushindwa vibaya na Waislamu waliamua kurejea nyuma hadi katika mpaka wa Palestina na Syria sambamba na kupoteza maeneo mengi yaliyokuwa chini ya udhibiti wao. ***

 

Siku kama ya leo miaka 1143 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa hadithi wa Kiislamu Abu Abdulrahman Ahmad bin Shuaib Nasai, maarufu kwa jina la Sheikhul Islam. Nasai alizaliwa mwaka 220 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Khorasan huko kaskazini mwa Iran na akaelea nchini Misri akiwa kijana. Huko alipata elimu ya fiqhi na hadithi na akaanza kufunza taaluma hizo. Baadaye Sheikhul Islam Nasai aliekele Damascus, Syria ambako alibainisha sifa na maadili ya watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake) na kupigwa mara kadhaa na wapinzani wa Ahlul Bait. Hatimaye alielekea Hijaz na kuishi mjini Makka. Nasai ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha "Khasaisu Amirul Muuminina Ali" na kile cha "Sunanun Nasai" ambacho ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vya hadithi vya Kiislamu. ***

 

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, kulifanyika mapinduzi ya Kimarekani dhidi ya serikali ya Dakta Muhammad Musaddiq nchini Iran na baadaye kidogo Shah Reza Pahlavi akatwaa tena madaraka ya nchi. Mapinduzi hayo ambayo yalipangwa na shirika la ujasusi la Marekani CIA kwa ushirikiano wa Uingereza, yaliiondoa madarakani serikali ya Musaddiq kupitia njia ya kuzusha hitilafu na mifarakano kati ya wanaharakati wa kisiasa na wananchi na kueneza anga ya ghasia na machafuko nchini. Vilevile yalimrejesha Iran Shah Pahlavi ambaye siku tatu kabla alikuwa amekimbilia nchini Italia. Kabla ya tukio hilo la kusikitisha, wananchi Waislamu wa Iran walikuwa wamefanikiwa kukata mkono wa Uingereza hapa nchini na kutaifisha sekta ya mafuta iliyokuwa ikidhibitiwa na wakoloni hao. ***

Mapinduzi ya Mordad 28

 

Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 28 Mordad 1357, Hijria Shamsia, vibaraka wa utawala wa Shah walifanya maafa ya kutisha ya kuchoma moto jumba la sinema la Rex katika mji wa Abadan kusini mwa Iran. Katika tukio hilo la kinyama watu wasio na hatia 377 wakiwemo watoto na wanawake walipoteza maisha yao. Jinai hiyo ilifanywa na maajenti wa Shirika la Kiintelijensia na Usalama wa Taifa la Iran (SAVAK) na vibaraka wa utawala wa Shah. Watu karibu 700 waliokuwa wakitazama sinema katika jumba hilo walifungiwa ndani baada ya moto kuzuka na mamia miongoni mwao wakateketea. Tukio hilo lilizusha hasira kubwa baina ya wananchi. Utawala wa Shah ulifanya maafa hayo na kisha kuwatuhumu wanamapinduzi kuwa ndio waliotekeleza shambulizi hilo la kutisha kwa shabaha ya kuchafua sura la harakati za Mapinduzi ya Kiislamu mbele ya wananchi. Hata hivyo njama hizo za Shah zilifeli. ***

Kuungua moto jumba la sinema la Rex katika mji wa Abadan