Aug 18, 2024 22:47 UTC
  • Jumatatu, 19 Agosti, 2024

Leo ni Jumatatu tarehe 14 Mfunguo Tano Safar 1446 Hiijria sawa na tarehe 19 Agosti 2024.

Katika siku kama ya leo miaka 814 iliyopita sawa na tarehe 14 Safar mwaka 632 Hijria alifariki dunia Abul Mahasin Bahauddin mashuhuri kwa jina la Ibn Shidad, fakihi, kadhi na mwanahistoria wa Kiislamu.

Alizaliwa mwaka 539 huko Mosul, moja ya miji ya Iraq na alihifadhi Qur'ani akiwa bado mtoto na baadaye akajifunza hadithi, tafsiri na kusoma Qur'ani na kupata umahiri mkubwa katika taaluma hizo. Ibn Shidad alifanya safari katika nchi mbalimbali za Kiislamu kwa ajili ya kutafuta elimu.

Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni an Nawadir al Sultwaniya, Dalailul Ah-kam na al Aswaa kinachozungumzia maisha ya Nabii Musa A.S na mapambano yake dhidi ya Firauni. 

Miaka 439 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Mulla Muhsin Faidh Kashani, aliyekuwa faqihi, mpokezi wa hadithi, mwanafalsafa na arifu mkubwa wa Kiislamu nchini Iran.

Faidh Kashani alipata elimu za fiqhi, hadithi, tafsiri na falsafa kwa wanazuoni wakubwa wa zama zake kama Muhammad Taqi Majlisi, Sheikh Bahai na Mulla Sadra.

Msomi huyo mkubwa ameandika vitabu vingi, mashuhuri zaidi vikiwa ni tafsiri ya Qur'ani ya al Swafi, Mafatiihu Sharaai', al Wafi na al Mahajjatul Baidhaa.   

Mahali lilipo kaburi la Mulla Muhsin Faidh Kashani

Siku kama ya leo miaka 362 iliyopita, alifariki dunia Blaise Pascal, mwandishi, mwanahisabati na mvumbuzi wa calculator au kikokotoo wa Kifaransa.

Alizaliwa Juni mwaka 1623 na tangu utotoni Pascal alivutiwa mno na somo la hisabati. Vilevile urafiki wa baba yake Pascal na msomi mmoja maarufu wa zama hizo ulisaidia mno katika kuchanua kipawa na kugunduliwa uwezo wa kijana huyo katika taaluma ya hisabati.

Mwishoni mwa umri wake Blaise Pascal alijielekeza mno katika masuala ya dini na kuandika vitabu kadhaa katika uwanja huo.

Blaise Pascal

Katika siku kama hii ya leo miaka 205 iliyopita aliaga dunia mvumbuzi na mhandisi wa Kiingereza James Watt.

Msomi huyo alipendelea na kuvutiwa mno na utafiti kuhusu masuala ya kisayansi. Katika utafiti wake Watt alifanikiwa kuvumbua nishati ya mvuke na kuzusha mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda hususan usafirishaji wa nchi kavu na baharini.

James Watt

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Urusi ya zamani wakiongozwa na Gennady Ivanovich Yanayev walifanya mapinduzi dhidi ya rais wa mwisho wa Muungano wa Sovieti, Mikhail Gorbachev.

Wanajeshi hao walitaka kukomeshwa marekebisho ya Gorbachev na kuzuia mpango wa kugawanywa Urusi ya zamani. Wakati wa mapinduzi hayo Mikhail Gorbachev alikuwa katika Peninsula ya Crimea huko kaskazni mwa Bahari Nyeusi. Hata hivyo Boris Yeltsin ambaye wakati huo alikuwa kiongozi wa Federesheni ya Urusi na ambaye alikuwa akiungwa mkono na Magharibi, alizima mapinduzi hayo kwa msaada wa wananchi na baadhi ya watu wenye ushawishi serikalini.

Kushindwa kwa mapinduzi hayo kulizidisha uwezo na satua ya Boris Yeltsin na kuharakisha mwenendo wa kusambaratika Urusi ya zamani hapo mwaka 1991. ***

Katika siku kama ya leo miaka 36 iliyopita Marekani ilikiri kwamba ilifanya makosa kuishambulia ndege ya abiria ya Iran hapo tarehe 3 Julai mwaka 1988.

Siku hiyo ndege ya abiria aina ya Airbus ya shirika la ndege ya Iran iliyokuwa ikitoka Bandar Abbas kusini mwa Iran na kuelekea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, ilishambuliwa kwa makombora mawili kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi. Manowari ya kijeshi ya Marekani, USS Vincennes, ilifyatua makombora hayo na kuua shahidi watu 298 waliokuwemo.

Shambulio hilo lilionyesha wazi unyama wa serikali ya Marekani na ukatili wake hata kwa wanawake na watoto wadogo waliokuwemo ndani ya ndege hiyo.

Viongozi wa Marekani walizidisha ukatili wao pale walipomzawadia medali ya ushujaa nahodha wa meli hiyo kutokana na kitendo hicho kilichoonekana na serikali ya Washington kuwa eti ni cha kishujaa.

Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, aliaga dunia Muhammad Hussein Behjati, mshairi na mwanazuoni mahiri wa Kiirani.

Alizaliwa 1314 Hijria Shamsia. Muhammad Hussein Behjati alianza kujihusisha na masomo tangu akiwa na umri wa miaka 7. Mwaka 1331 alielekea katika mji wa Qum.

Msomi huyo aliposoma pamoja na Ayatullah Hashemi Rafsanjani, Mas'ud Khomeini na Ayatullah Khamenei. Alikuwa pia mmoja wa wanafunzi wa Imam Khomeini na Ayatullah Burujerdi.

Muhammad Hussein Behjati