Aug 21, 2024 23:59 UTC
  • Alkhamisi, Agosti 22, 2024

Leo Alkhamisi tarehe 17 Safar mwaka 1446 Hijria, sawa na Agosti 22 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 550 iliyopita, alizaliwa Muhammad Mustafa Imad, maarufu kwa jina la  Abus-Su’ud, faqihi na mfasiri wa Kiislamu katika kijiji cha Mudares karibu na mji wa Istanbul huko Uturuki.

Baada ya kuhitimu masomo yake, Abus-Su’ud alijishughulisha na ufundishaji na kufanya kazi ya ukadhi mjini Istanbul, kazi aliyoendelea nayo hadi mwisho wa uhai wake. Abus-Su’ud alikuwa hodari katika masuala mbalimbali ya kijamii na aliweza kuandaa sheria za kiidara kwa mujibu wa dini ya Kiislamu katika utawala wa Othmania.

Mbali na kuzungumza lugha ya Kituruki, alizungumza pia lugha za Kifarsi na Kiarabu. Msomi huyo wa Kiislamu ametunga mashairi kadhaa kwa lugha hizo. Miongoni mwa vitabu vya Abus-Su’ud ni pamoja na ‘Irshadul-Aqlis-Saliim’ ‘Dua Nameh’ ‘Qanun Nameh’ na ‘Mafrudhaat'.   ***

Katika siku kama ya leo miaka 397 iliyopita vilijiri vita vya mwisho vya La Rochelle kati ya Wakatoliki na Waprotestanti wa Ufaransa.

Vita hivyo vilianza baada ya Waprotestanti kuchochewa na Uingereza. Wakatoliki ambao walikuwa wakiungwa mkono na vikosi vya jeshi la serikali ya Ufaransa chini ya uongozi wa Richelieu, Kansela mashuhuri wa nchi hiyo, walipigana vita na Waprotestanti ambao walikuwa wakipigania maeneo yao katika bandari ya La Rochelle.

Vita hivyo vilimalizika baada ya mwaka mmoja kwa kupata ushindi Wakatoliki na kutekwa La Rochelle.  ***

Miaka 326 iliyopita katika siku kama ya leo, mkataba wa pande tatu wa Russia, Poland na Denmark ulitiwa saini dhidi ya Sweden.

Wafalme wa nchi hizo tatu walikuwa na lengo la kumuangusha Karl XII mfalme kijana wa Sweden ili kuikalia kwa mabavu nchi hiyo. Ni kwa msingi huo ndipo miaka miwili baadaye mnamo mwezi Aprili mwaka 1700 nchi wanachama wa mkataba huo wa pande tatu zikaamua kuishambulia Sweden, hata hivyo jeshi la mfalme Karl XII likakabiliana vilivyo na kutoa pigo kwa nchi vamizi.

Baada ya kufikia mapatano na Denmark, mwaka 1704 akaishambulia Poland na kuikalia kwa mabau. Hata hivyo mashambulio ya Sharel dhidi ya Russia hayakuzaa matunda.   ***

Katika siku kama ya leo miaka 191 iliyopita, alizaliwa Sheikh Abdul Rahim Sultanul-Qurrai Tabrizi, qaari mkubwa wa Qur’ani Tukufu na mmoja wa walimu mashuhuri wa taaluma ya qiraa, huko mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran.

Baada ya kujifunza taaluma hiyo kutoka kwa baba yake, Sultanul-Qurrai Tabrizi alifahamiana na Sheikh Shamil Daghestani na kushirikiana naye. Wakati Sheikh Shamil Daghestani alipoandaa jeshi kwa ajili ya kupambana na Warusi, Sultanul-Qurrai alifanya safari kuelekea Daghestani ili kushiriki katika harakati hiyo. Baadaye alirejea Tabriz na kuanzisha chuo cha kisomo cha Qur’ani na ni wakati huo ndipo alipopewa lakabu ya Sultanul-Qurrai.

Miongoni mwa athari zake ni pamoja na ‘Risala katika Elimu ya Tajwidi’. Sultanul-Qurrai alifariki dunia mwaka 1336 Hijiria mjini Tabriz.   ****

Siku kama ya leo miaka 164 iliyopita Paul Gottlieb Nipkow mmoja wa wavumbuzi wa televisheni alizaliwa huko Ujerumani.

Nipkow alikulia katika familia maskini, lakini juhudi na irada kubwa ilimuwezesha kuendeleza masomo yake ya fizikia hadi chuo kikuu. Paul Gottlieb Nipkow alifanya utafiti mkubwa na hatimaye alifanikiwa kuvumbua transimita ya televisheni.

Chombo hicho kilichobuniwa na Nipkow kiliweza kurusha mawimbi ya televisheni katika umbali wa mita 30 na baadaye transimita iliyotengenezwa na mvumbuzi huyo wa Kijerumani ilikamilishwa na wabunifu wengine.  ***

Na miaka 160 iliyopita katika siku kama hiii ya leo, mkataba wa kihistoria wa Geneva ulitiwa saini baina ya nchi kadhaa za Ulaya, Asia na Amerika.

Lengo la mkataba huo lilikuwa ni kuwasaidia majeruhi katika medani za vita.  Kwa mujibu wa mkataba huo, timu za madaktari, watoaji misaada na zana zao zinapaswa kutoegemea upande wowote na zisishambuliwe bali zibakie katika amani wakati wa vita. Mbunifu wa mkataba huo alikuwa Henry Dunant raia wa Uswisi.   ***

Miaka 26 iliyopita katika siku hii sawa na ya kwanza ya Shahrivar mwaka 1377 Hijria Shamsia:

Mwanamapinduzi na mmoja wa wanachama wakuu wa Chama  cha Muungano wa Kiislamu Sayyid Asadollah Lajevardi aliuawa shahidi na kundi la kigaidi la MKO.

Sayyid Asadollah Lajevardi alizaliwa mjini Tehran mwaka 1314 Hijria. Akiwa kijana, aliacha shule ya upili na kuanza kufanya kazi na baba yake. Baadaye, alijiunga na chuo cha kidini. Kuanzia mwanzo wa harakati ya Kiislamu ya wananchi wa Iran chini ya uongozi wa Imam Khomeini, Shahidi Lajevardi naye alijiunga na mwenendo huo na akawa na nafasi muhimu katika kuanzishwa  kwa jumuiya za muungano wa Kiislamu mwaka 1341.

Pamoja na mashahidi Beheshti na Motahari, aliamua kuunda muungano dhidi ya serikali na alifanya jitihada  kubwa katika uwanja huu. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Shahidi Sayyid Asadollah Lajevardi aliteuliwa katika Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mapinduzi ya Kiislamu. Uteuzui huo ulifanywa na Shahidi Dakta Beheshti aliyekuwa mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran wakati huo. Baada ya hapo akawa mkuu wa shirika la magereza nchini humo.

Kundi la kkigaidi la MKO lilijaribu kumuua mara nyingi hadi akauawa shahidi na mnafiki mamluki akiwa na umri wa miaka 63 mahali pake pa kazi katika soko la Tehran mnamo tarehe ya kwanza ya Shahrivar 1377.  ****

Na leo tarehe Mosi Shahrivar katika kalenda ya mwaka wa Kiirani inatambuliwa kuwa siku ya kumuenzi Hassan bin Abdullah maarufu kwa jina la Abu Ali bin Sina na Siku ya Daktari hapa nchini.

Ibn Sina

Abu Ali Sina mwanafalsafa na tabibu mashuhuri wa Kiislamu na Kiirani aliyejulikana pia kwa laqabu ya Sheikhul Rais, alizaliwa tarehe 3 Safar mwaka 370 Hijria Qamaria katika mji wa Balkh. Ibn Sina alihifadhi Qur'ani yote alipokuwa na umri wa miaka 10. Msomi na tatibu huyo mashuhuri wa Kiislamu alijifunza tiba baada ya kupata elimu za mantiki, hisabati, nujumu, falsafa pamoja na elimu nyinginezo. Alianza kuandika vitabu akiwa na umri wa miaka 21 na miongoni mwa vitabu vyake maarufu ni Qanun, Shifaa na Isharaat.