Jumanne, tarehe 27 Agosti, 2024
Leo ni Jumanne tarehe 22 Safar 1446 Hijria sawa na Agosti 27 mwaka 2024.
Siku kama ya leo miaka 389 iliyopita, alifariki dunia Lope de Vega, mwandishi mkubwa wa Uhispania.
Vega alizaliwa mwaka 1562 Miladia na akiwa kijana mdogo alionekana kuwa mwenye harakati nyingi na mwenye kipawa kikubwa cha akili huku akianza pia kusoma mashairi.
Akiwa na umri wa miaka 14 alijiunga na shule ya msingi na sekondari ya kidini ambapo baada ya kuhitimu masomo yake katika chuo kikuu, alijiunga na jeshi la kujitolea. Taratibu akaanza kuonyesha kipawa chake katika michezo ya kuigiza na masuala mengine na hivyo kuwavutia watu wengi.
Lope de Vega anajulikana kuwa mwanzilishi wa michezo ya kuigiza kitaifa nchini Uhispani.
Siku kama ya leo miaka 254 iliyopita, alizaliwa Georg Wilhelm Friedrich Hegel mwanafalsafa mkubwa wa Ujerumani.
Licha ya msomi huyo kufundisha katika vyuo mbalimbali na kuandika vitabu tofauti, lakini bado alikuwa masikini. Kufuatia uvamizi wa jeshi la Napoleon dhidi ya Ujerumani mwaka 1806, Hegel alivutiwa na shakhsia ya kamanda huyo Kifaransa. Alibainisha hatua za historia na kuamiani kuwa, muelekeo wa harakati ya kihistoria huainishwa na Mwenyezi Mungu na kwamba hata malengo ya historia ni hivyo.
Katika kubainisha itikadi yake, Georg Wilhelm Friedrich Hegel aliandika vitabu kadhaa katika uwanja huo. Hegel alifariki dunia mwaka 1831 Miladia.
Miaka 104 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi, msomi mkubwa na mwanamapambano wa Iran.
Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi ni mmoja wa maulama wakubwa wa Kishia na aliyepambika kwa elimu na uchaji-Mungu huko mjini Shirazi, moja ya miji ya Iran ya leo. Msomi huyo alipata umashuhuri kutokana na kuongoza mapinduzi ya Waislamu dhidi ya Uingereza.
Baada ya Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi kugundua kuwa Uingereza ilikuwa na lengo la kudhibiti nchi za Kiislamu kupitia pendekezo la kutaka kukubaliwa mwakilishi wa Londoni nchini Iraq kuwa rais wa nchi hiyo, alitoa fatwa mashuhuri iliyopewa jina la fatwa ya kujilinda ambayo ilihalalisha mapambano ya silaha ya wananchi wa Iraq dhidi ya mkoloni Mwingereza. Fatwa hiyo iliitia hofu Uingereza ambayo ililazimika kuachana na mpango huo wa kikoloni.

Tarehe 27 Agosti mwaka 1896, kulitokea vita vya muda mfupi zaidi duniani visiwani Zanzibar.
Jengo la Kihistoria mjini Unguja linalojulikana kwa jina la Beit al-Ajaib lililojengwa na Sultan Barghash bin Said huko Forodhani kisiwani Unguja, lilishambuliwa kwa mizinga ya manowari za Uingereza. Hatua hiyo ilikuja kufuatia ugomvi uliozuka baina ya wana wawili wa Sultani wa Zanzibar.
Watoto hao walijulikana kwa majina ya Said Barghash Khalid na Said Hamud bin Muhammed na ugomvi wao ulihusiana na utawala na nani anapaswa kurithi kiti cha ufalme. Vita hivyo vilidumu kwa dakika 45 tu na kuwa vita vifupi zaidi duniani. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, yaani tarehe 27 Agosti mwaka 1991, nchi ya Moldova iliyoko mashariki mwa Ulaya ilipata uhuru.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za historia nchi hiyo ilikaliwa kwa mabavu na tawala, kaumu na nchi mbalimbali zikiwemo, Ukraine, Russia, Romania na utawala wa Othmania. Baada ya mapinduzi ya kikomunisti nchini Russia, Moldova iliungana na Romania.
Mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, Moldova ilikaliwa kwa mabavu na Urusi. Hata hivyo baada ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti, nchi hiyo ikajikomboa na kupata uhuru.
