Jumatatu, tarehe Pili Septemba, 2024
Leo ni Jumatatu tarehe 28 Mfunguo Tano Safar 1446 Hijria mwafaka na tarehe Pili Septemba 2024.
Siku kama ya leo miaka 1435 iliyopita inayosadifiana na tarehe 28 Safar mwaka 11 Hijria, alifariki dunia Mtume Muhammad (saw) akiwa na umri wa miaka 63.
Kutokana na kuwa na tabia ya ukweli na uaminifu tangu alipokuwa na umri mdogo, Mtume Mtukufu (saw) alipata umashuhuri kwa jina la "Muhammad Mwaminifu". Akiwa na umri wa miaka 40 Mwenyezi Mungu SW alimteua kuwa Mtume Wake ili aweze kuwalingania watu ibada ya Mungu Mmoja na kuondoa ukabila, dhulma na ujinga.
Watu wa dini, madhehebu na mirengo tofauti na hata wale wasiokuwa na dini kabisa wamesema mengi kuhusu shakhsia adhimu ya Nabii Muhammad (saw). Mwandishi wa Ulaya, Stanley Lane Poole ameandika kwamba, Mtume Muhammad alipendwa na watu wote na kila aliyemuona, na kwamba hajawahi kuona wala hatamuona tena mtu mithili yake.

Siku kama ya leo miaka 1396 iliyopita, yaani sawa na tarehe 28 Safar mwaka 50 Hijiria, aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as), mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw).
Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia mjini Madina. Mtukufu huyo aliishi miaka saba ya mwanzo wa umri wake pamoja na babu yake Mtume Muhammad (saw) ambapo aliweza kunufaika na mafunzo na maarifa ya dini Tukufu ya Kiislamu. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ali (as). Baada ya kufariki dunia Imam Ali (as) Waislamu walimpa baia Imam Hassan kwa ajili ya kuwaongoza, ambapo hata hivyo baada tu ya kuteuliwa kwenye nafasi hiyo alikabiliwa na njama pamoja na ukwamishaji mambo wa Muawiyah bin Abi Sufiyan.
Hatimaye Imam Hassan aliandaa jeshi aliloachiwa na baba yake kwa ajili ya kumkabili Muawiya, ingawa muovu huyo (Muawiya) alitumia hila za kila namna kuwanunua wafuasi wa Imam Hassan ambao hatimaye walimkimbia na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume wa Allah.
Imam Hassan aliuawa shahidi siku kama ya leo kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufiyan.

Siku kama ya leo miaka 223 iliyopita, baada ya vita kadhaa baina ya vikosi vya utawala wa Othmania na jeshi la Uingereza kwa upande mmoja na vikosi vya Ufaransa kwa upande mwingine, hatimaye Wafaransa walishindwa katika vita na kulazimika kuondoka kikamilifu nchini Misri.
Ikumbukwe kuwa, baada ya Napoleone Bonaparte kuikalia kwa mabavu ardhi ya Misri, Uingereza ambayo katika zama hizo ilikuwa ikihesabiwa kuwa hasimu na mshindani mkuu wa Ufaransa katika masuala ya kiuchumi na kijeshi, ilihisi maslahi yake yakiwa hatarini.
Ni kwa sababu hiyo ndio maana Uingereza ikaungana na utawala wa Othmania kwa shabaha ya kwenda kuitoa Ufaransa huko Misri na kuzuia jeshi la Ufaransa lisisonge mbele.

Siku kama ya leo miaka 159 iliyopita, William Rowan Hamilton mwanahisabati na mtaalamu mahiri wa elimu ya fizikia wa Ireland alifariki dunia.
Alizaliwa mwaka 1805 na kuonyesha kuwa mwerevu na mwenye kipaji cha hali ya juu tangu akiwa mtoto mdogo. Hamilton alisoma kwa ami yake aliyekuwa kasisi. Alipofikisha umri wa miaka 13, mwanafizikia huyo mtajika wa Ireland alikuwa tayari anazifahamu lugha kadhaa za kimataifa. Hadi anafikisha umri wa miaka 22 alikuwa tayari ni mwalimu katika elimu ya nujumu.
Katika siku kama ya leo miaka 109 iliyopita aliuawa shahidi Rais Ali Delvari, kiongozi wa mapambano dhidi ya uvamizi wa Uingereza huko kusini mwa Iran.
Manzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia vikosi vya majeshi ya Urusi kutokea kaskazini na majeshi ya Uingereza kutokea kusini viliazimia kuikalia kwa mabavu ardhi ya Iran. Wakati huo Rais Ali Delvari alitoa wito kwa wananchi kukabiliana na wavamizi wa Uingereza kwa kutegemea fatua ya vita vya jihadi iliyokuwa imetolewa na maulama wa Kiislamu ya ulazima wa kulinda nchi mbele ya maadui.
Rais Ali Delvari na wapiganaji wenzake shupavu walikabiliana na mashambulizi ya mara kwa mara ya majeshi yaliyokuwa yamejizatiti kwa silaha na kuzuia kutekwa mji wa Busher. Mapambano ya wananchi wa Tengestan karibu na mji wa kuisni wma Iran wa Busher dhidi ya majeshi vamizi ya Uingereza yaliendelea kwa kipindi cha miaka 7.
Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, nchi ya Vietnam ilipata uhuru. Vietnam ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Ufaransa katikati mwa karne ya 19.
Mwaka 1940 nchi hiyo ikadhibitiwa na Japan baada ya Ufaransa kushindwa na Ujerumani wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Vietnam iliendelea kuwa chini ya utawala na udhibiti wa Japan hadi pale Japan iliposalimu amri mwishoni mwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Tarehe Pili Septemba mwaka 1945, Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vilifikia tamati baada ya Japan kusalimu amri bila ya masharti yoyote.
Baada ya Japan kushindwa mfululizo na majeshi ya waitifaki, ililazimika kusalimu amri katika vita hivyo, hasa baada ya miji yake miwili mashuhuri ya Hiroshima na Nagasaki kushambuliwa na Marekani kwa mabomu ya atomiki.
Baada ya tukio hilo lililotokea miezi minne tu baada ya kusalimu amri Ujerumani, nchi waitifaki ziliikalia kwa mabavu Japan kwa mujibu wa Mkataba wa Potsdam na Generali wa Kimarekani, Douglas MacArthur, akachaguliwa kuwa kamanda mkuu huko Japan.
Mwaka 1951, nchi 49 duniani zilitiliana saini mkataba wa amani na Japan, na mwaka mmoja baadaye nchi hiyo kwa mara nyingine tena ikaanza kujitawala na kujiamulia mambo yake yenyewe.

Na miaka 32 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, aliaga dunia Dkt. Mahmoud Hesabi mwanafizikia mashuhuri wa Iran anayejulikana kama baba wa fizika ya kisasa ya Iran. Alizaliwa mwaka 1281 katika mji wa Tehran. Profesa Mahmoud Hesabi alikuwa na bidii kubwa masomoni na daima kuanzia masomo yake ya msingi hadi ya juu alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani. Sambamba na masomo shuleni, Mahmoud Hesabi alikuwa akijihusisha pia na kujifunza na kusoma dafina na hazina ya maarifa ya Kiislamu na Kiirani. Hakutoshoka na taaluma moja tu, bali alifanya hima ya kusoma fani mbalimbali. Alipofikisha umri wa miaka 17, Mahmoud Hesabi alikuwa tayari amefikia daraja za juu za masomo. Mbali na kuwa mahiri katika taaluma kama za uhandisi wa barabara, majengo, madini, umeme, fizikia na kadhalika, msomi huyu alikuwa amebobea pia katika lugha za kigeni zilizoenea duniani kama Kiarabu, Kiingereza, Kijerumani na Kifaransa. Profesa Mahmoud Hesabi aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 90 baada ya kuishi maisha yaliyojaa hima na juhudi za kielimu.