Sep 03, 2024 23:07 UTC
  • Jumatano, 4 Septemba, 2024

Leo ni Jumatano tarehe 30 Mfunguo Tano Safar 1446 Hijria, sawa na tarehe 4 Septemba 2024.

Katika siku ya mwisho ya mwezi wa Safar miaka 1242 iliyopita, aliuawa shahidi Imam Ali bin Mussa al Ridha AS, mmoja kati ya wajukuu wa Mtume Mtukufu SAW.

Mtukufu huyo alizaliwa mwaka 148 Hijria katika mji wa Madina na alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, yaani Imam Mussa al Kadhim AS. Mnamo mwaka 200 Hijria, Maamun, Khalifa wa Bani Abbasi, alimtaka Imam Ridha AS aelekee kwenye makao ya Khalifa huyo yaliyokuwa katika mji wa Marwi, kusini mashariki mwa Turkemenistan ambayo ilikuwa sehemu ya Khorasan Kuu.

Ijapokuwa kidhahiri Maamun alimfanya Imam Ridha kuwa mrithi wake, lakini kwa njia hiyo alikusudia kuimarisha zaidi nguvu za utawala wake. Utukufu na daraja ya juu ya kielimu na kimaanawi aliyokuwa nayo Imam Ridha na ushawishi wake uliokuwa ukiongezeka siku hadi siku ndani ya fikra na nyoyo za watu, vilimtia woga na hofu Maamun, na hivyo akaamua kufanya njama za kumpa sumu na kumuua shahidi Imam Ridha katika siku kama leo.

Imam AS amesema:"Mja bora zaidi ni yule ambaye kila anapofanya jema hufurahia, na kila anapokosea huomba msamaha. Inapomfikia neema hushukuru, anapokumbana na masaibu husubiri, na wakati anapoghadhibika husamehe".

Haram ya Imam Ridha (as), Mash'had

Siku kama ya leo miaka 142 iliyopita, mota ya kwanza ya umeme ilitengenezwa.

Mvumbuzi na mtengenezaji wa mota hiyo alikuwa Thomas Edison mtaalamu na mtafiti wa Kimarekani. Kwa kutumia mota hiyo ya umeme, Edison alianzisha kiwanda cha umeme katika mji wa New York na wakati huo huo akawa amefanikiwa kudhamini sehemu ya mahitaji ya mwanga katika mji huo. Kumbukumbu za kihistoria zinaonyesha kwamba, mwaka 1879, Edison alifanikiwa kuvumbua balbu.   

Thomas Edison

Tarehe 4 Septemba miaka 116 iliyopita alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Marekani mwenye asili ya Afrika, Richard Wright.

Baada ya mashaka makubwa maishani, Richard Nathaniel Wright alianza kazi ya uandishi akiwa na umri wa miaka 30. Baadhi ya vitabu vyake vinaakisi sehemu ya maisha ya kifukara na ya kuchosha ya Wamarekani wenye asili ya Afrika.

Ameandika vitabu vingi kama Black Boy, Native Son, Uncle Tom's Children na The Outsider. 

Richard Wright

Siku kama ya leo miaka 96 iliyopita, tabibu Alexander Fleming alivumbua dawa ya penicillin.

Fleming ambaye alikuwa daktari maarufu wa nchini Uingereza, alizaliwa tarehe Sita Agosti mwaka 1881 Miladia katika familia ya wakulima mjini Lochfield farm, magharibi mwa Scotland.

Fleming alivumbua dawa hiyo baada ya kuona kuwa askari wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukumbwa na bakteria wa maambukizi kwenye majeraha, suala ambalo lilimtia wasiwasi mkubwa.   

Alexander Fleming

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita Ayatullah Ali Quddusi Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mapinduzi ya Kislamu nchini Iran aliuawa shahidi katika mlipuko wa bomu lililotegwa na kundi la kigaidi la MKO.

Shahidi Quddusi alipata elimu yake kutoka kwa wasomi na wanavyuoni kama Ayatullah Burujerdi, Allama Tabatabai na Imam Ruhullah Khomeini MA na kufikia daraja ya Ijtihad. Shahidi Quddusi alishiriki vilivyo katika masuala ya kidini na mfano wa wazi wa mchango wake ni kuasisi skuli ya mafunzo ya kidini ya Haqqani. Mwaka 1341 Hijria Shamsia alisimama kupambana na utawala dhalimu wa Shah na akatiwa jela kwa kipindi fulani.

Ayatullah Quddusi alisabilia miaka ya mwishoni mwa umri wake katika juhudi za kuimarisha mfumo mchanga wakati huo wa Kiislamu hapa nchini na hatimaye aliuawa shahidi na magaidi wa kundi la MKO katika siku kama hii ya leo.

Ayatullah Ali Quddusi