Ijumaa, tarehe 6 Septemba, 2024
Leo ni Ijumaa tarehe Pili Rabiul Awwal 1446 Hijria sawa na tarehe 6 Septemba 2024.
Siku kama ya leo miaka 816 iliyopita, aliaga dunia Ibn Athir Jazari, mwanahistoria, mtaalamu wa fasihi na mpokezi mkubwa wa Hadithi.
Ibn Athir alizaliwa mwaka 555 Hijria huko Iraq na kujifunza taaluma mbalimbali. Alipata umashuhuri katika masuala ya lugha na fasihi ya Kiarabu.
Kitabu maarufu zaidi cha Ibn Athir ni al Kamil fi al Tarikh. Kitabu kingine cha mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ni Usdul Ghabah Fi Ma'rifatis Sahabah ambacho kinaeleza wasifu wa masahaba 7,500 wa Mtume Muhammad (saw).

Siku kama ya leo miaka 258 iliyopita, alizaliwa John Dalton, msomi na mtaalamu wa fizikia wa Kingereza katika familia ya watu wa kijijini.
Kutokana na Dalton kupendelea sana elimu na licha ya kukabiliwa na matatizo mengi, alifanikiwa kwenda shuleni na kujifunza mambo mbalimbali. Ni wakati huo ndipo alipoanza kufanya uchunguzi na utafiti katika masuala mbalimbali ya kielimu.
Dalton alibuni na kuvumbua mambo mengi katika uwanja wa fizikia, kemia na sayansi asilia baada ya utafiti mkubwa.
Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, jeshi la India lilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Pakistan kufuatia machafuko ya zaidi ya mwezi mmoja katika mipaka ya nchi mbili hizo.
Hivyo vilikuwa vita vya pili vikubwa kuwahi kutokea kati ya nchi mbili hizo jirani kuhusiana na eneo la Kashmir. Vita hivyo viliendelea kwa takribani wiki tatu.
Pakistan na India zilikubaliana kusimamisha mapigano kufuatia upatanishi wa Urusi ya zamani. Viongozi wa nchi mbili hizo hatimaye waliafikiana kuanza mazungumzo tarehe 10 mwezi Juni mwaka 1966 huko Tashkent mji mkuu wa Uzbekistan nchini ya upatanishi wa Waziri Mkuu wa Urusi ya zamani.
Japokuwa azimio la Tashkent lilibainisha njia za kumaliza mgogoro wa eneo la Kashmir na namna ya kuboresha uhusiano kati ya New Delhi na Islamabad na pia kukaribishwa na nchi mbalimbali duniani, lakini lilishindwa kumaliza hitilafu kati ya India na Pakistan kuhusu umiliki wa eneo la Kashmir.

Katika siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Eswatini (Swaziland zamani) ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza na kila inapowadia siku kama ya leo husherekewa nchini humo kwa anwani ya siku ya taifa.
Kuimarika ukoloni wa Ulaya huko kusini mwa Afrika kulisababisha pia Eswatini kukaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Ulaya.
Hatimaye katika siku kama ya leo nchi hiyo ndogo ya kusini mwa Afrika ilipata uhuru. Eswatini ina ukubwa wa kilomita mraba 17364 na kijiografia iko kusini mwa bara la Afrika ikiwa inapakana na nchi za Msumbiji na Afrika Kusini.
