Ijumaa, tarehe 13 Septemba, 2024
Leo ni Ijumaa tarehe 09 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1446 Hijria sawa na 13 Septemba 2024.
Siku kama ya leo miaka 1397 iliyopita, vilimalizika vita vya miaka 24 baina ya mfalme wa Iran na Roma.
Khosrow Parvēz, mfalme wa Kisasani kwa kutekeleza mashambulizi mtawalia, aliweza kudhibiti maeneo ya Mesopotamia, Syria, Palestina, Misri na Asia Ndogo, na hivyo akawa ameweza kupanua wigo wa ushindi wake hadi kufikia Istanbul ya leo. Mwaka 591 Miladia, hatimaye amani ilifikiwa kufuatia kutiwa saini makubaliano baina ya mfalme Khosrow Parvēz na mfalme wa Roma. Hata hivyo tarehe Tano Juni mwaka 603 Miladia, kuliibuka tena vita vilivyoendelea kwa muda wa miaka 24 baina ya nchi hizo mbili.
Katika vita hivyo, jeshi la Iran lilipata ushindi mtawalia katika ardhi ya Roma kiasi cha kudhibiti karibu eneo zima la Roma ya Mashariki. Baadaye jeshi la mfalme Khosrow lilidhoofika na kumfanya mfalme huyo kukimbilia eneo la Ctesiphon, moja ya tawala za Sasania, huku akikataa pendekezo la usuluhishi.
Aidha kutokana na Mfalme Khosrow Parvēz kuchana barua ya Mtukufu Mtume Muhammad (saw) na kulaaniwa na mtukufu huyo, utawala wa mfalame huyo ulidhoofika na hatimaye kushindwa na Waroma. Baadaye raia wa Iran, kwa kushirikiana na jeshi la taifa, walimuengua Khosrow kwenye utawala na kumfunga jela kabla ya kuuawa kwake.

Siku kama ya leo miaka 1186 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, baada ya kuuawa shahidi Imam Hassan Askari (AS), kilianza rasmi kipindi cha uongozi wa Imam wa Zama, Imam Mahdi (AF).
Imam Mahdi ni mwana wa Imam Hassan al Askari (AS) na miongoni mwa wajukuu wa Bwana wetu Muhammad (saw). Imam Mahdi yuko ghaiba kwa amri ya Mwenyezi Mungu (SW) na hadi mwaka 328 Hijria alikuwa akiwasiliana na watu kupitia wawakilishi wake maalumu. Kipindi hicho kilipewa jina la "Ghaiba Ndogo".
Baada ya hapo kilianza kipindi cha Ghaiba Kubwa ambapo Imam wa Zama hakuainisha mwakilishi makhsusi, na mafaqihi wenye ujuzi wa dini ya Kiislamu, wachamungu na watambuzi wa masuala ya zama ndio wawakilishi wa mtukufu huyo katika Umma.
Kwa mujibu wa Hadithi tukufu za Mtume Muhammad (saw), Imam Mahdi (AF) atadhihiri tena katikka aheri zamani kwa ajili ya kueneza haki na uadilifu.

Siku kama ya leo miaka 774 iliyopita, vilianza vita vya Mansuriyya katika silsila ya Vita vya Msalaba kati ya Wakristo na Waislamu.
Vita hivyo vya kihistoria vilianzishwa katika eneo lililojulikana kwa jina hilo huko Misri na mfalme Saint Louis wa Ufaransa ambaye alikuwa na lengo la kuidhibiti Misri.
Katika vita vya Mansuriyya Jeshi la Msalaba lilipigwa vibaya na wapiganaji wa Kiislamu wa Misri waliokuwa wakiongozwa na Salahuddin Ayyubi.
Hatimaye Saint Louis alikamatwa mateka na Waislamu na kufungwa jela katika ikulu ya Loken ambayo hii leo inatumika kama jumba la makumbusho.

Miaka 244 iliyopita lifti au elevator kwa kimombo ilivumbuliwa.
Mvumbuzi wa lifti hiyo ya kwanza alikuwa raia wa Marekani aliyejulikana kwa jina la John Bikbart.
Lifti hiyo ilifanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza huko katika mji wa Chicago. Katika majaribio hayo, watu kadhaa waliingia ndani ya lifti hiyo na kwenda juu na chini katika masafa marefu.
Lifti ya kwanza ya umeme ilitengenezwa mwaka 1889 na ile ya otomatiki mwaka 1915. ***
Siku kama ya leo miaka 139 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 13 Septemba 1885, alizaliwa Aquilino Ribeiro mwandishi na mwanamapinduzi wa Ureno.
Baada ya kumaliza masomo yake, Ribeiro alitumbukia kwenye uwanja wa kisiasa na kufungwa jela kwa miaka kadhaa. Mnamo mwaka 1961, Aquilino Ribeiro alifanikiwa kupokea tuzo ya Nobel katika taaluma ya fasihi, na miaka miwili baadaye yaani mwaka 1963 akafariki dunia.
Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita yaani tarehe 23 Shahrivar mwaka 1357 Hijria Shamsia kulifanyika maandamano makubwa hapa nchini kuwaenzi mashahidi waliokuwa wameuawa na vibaraka wa Shah siku kadhaa kabla yake.
Siku hiyo umati mkubwa wa watu ulimiminika katika makaburi ya Behest Zahraa mjini Tehran kuwaenzi mashahidi hao.
Askari wa utawala wa Shah walikuwa na nia ya kuzuia maandamano hayo lakini umati mkubwa wa wananchi walioshiriki maandamano ulidumisha malalamiko yao dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah huku wakipiga nara za: “Iran ni nchi yetu na Khomeini na kiongozi wetu.”
Na Siku kama hii ya leo miaka 31 iliyopita, mwafaka na tarehe 13 Septemba 1993 Yasir Arafat, kiongozi wa zamani wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na Yitzhak Rabin waziri mkuu wa wakati huo wa utawala haramu wa Israel walisaini mkataba wa mapatano kwa jina la "Makubaliano ya Ghaza-Jericho" huko Washington, Marekani.
Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na utawala wa Kizayuni zilitambuana rasmi katika makubaliano hayo yaliyosainiwa miaka miwili baada ya kuanza mazungumzo eti ya amani kati ya Waarabu na utawala wa Kizayuni.