Jumapili, 15 Septemba, 2024
Leo ni Jumapili 11 Mfuunguo Sita Rabiuul Awwal 1446 Hijria sawa na 15 Septemba 2024 Miladia.
Miaka 203 iliyopita yaani tarehe 15 Septemba 1821, nchi za Nicaragua, Honduras, el-Salvador, Guatemala na Costa Rica zilijitangazia uhuru kutoka kwa Uhispania. Baada ya Napoleone Bonaparte mtawala wa Kifaransa kuikalia kwa mabavu Uhispania na kudhoofika serikali ya kijeshi ya Madrid, nchi kadhaa za Latin America zikiwemo Nicaragua, Honduras, el-Salvador, Guatemala na Costa Rica zilijitangazia uhuru. Baada ya nchi hizo tano kujitangazia uhuru ziliunda Muungano wa Amerika ya Kati. Baada ya muungano huo kuvunjika mwaka 1838, nchi wanachama kila moja ilianza kujitawala na kujiendeshea mambo yake yenyewe.

Siku kama ya leo miaka 153 iliyopita alizaliwa kulingana na kalenda yay Hijria mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Allamah Agha Bozorge Tehrani. Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Allamah Agha Bozorge Tehrani alikweya kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa kidini. Allamah Tehrani alisafiri na kufanya uchunguzi katika maktaba nyingi za nchi kama Iran, Misri, Syria, Iraq, Hijaz, Palestina na kadhalika kwa ajili ya kutayarisha ensaiklopedia ya vitabu vya Kiislamu. Alifanikiwa kuandika tabu hilo kubwa lenye juzuu 26 ambalo alilipa jina la "Adhari'a ila Tasaanifish Shia". Kitabu kingine muhimu cha Allamah Agha Bozorge Tehrani ni "Tabaqatu Aalami Shia" chenye juzuu 8. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia katika mji mtakatifu wa Najaf na kuzikwa katika maktaba yake kama alivyokuwa ameusia.
Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita utawala wa kidikteta wa Reza Khan nchini Iran uliangushwa na kukaanza kipindi cha utawala wa mwanawe yaani Muhammad Reza Pahlavi. Baada ya mashambulio ya Jeshi Jekundu la Umoja wa Kisovieti upande wa kaskazini na jeshi la Uingereza upande wa magharibi na kusini mwa Iran na kukaliwa kijeshi Iran wakati wa kujiri Vita vya Pili vya Dunia, Reza Khan alilazimika kujiuzulu katika siku kama ya leo baada ya kutawala kidikteta nchini Iran kwa muda wa miaka 15. Baada ya kubaidishwa Reza Khan, mwanawe yaani Muhammad Reza Pahlavi aliingia madarakani kwa ushirikiano na Waingereza. Baada ya kubaidishwa kwa muda katika kisiwa cha Mauritius hatimaye alipelekwa Johannesburg Afrika Kusini. Aliishi huko hadi alipofariki dunia tarehe 26 Julai 1944.
Katika siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, zilzala iliyokuwa na ukubwa wa 7.7 kwa kipimo cha rishta ililitikisa eneo la kaskazini mashariki mwa Iran na kuuharibu mji wa Tabas na vijiji vya kando kando yake. Watu zaidi ya elfu 25 waliuawa na makumi ya maelfu kujeruhiwa katika mtetemeko huo mkubwa wa ardhi. Zilzala ya Tabas ilitokea sambamba na kupamba moto mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah.