Sep 16, 2024 02:27 UTC
  • Jumatatu, 16 Septemba 2024

Leo ni Jumatatu tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1446 Hijria sawa na Septemba 16, 2024.

Siku kama ya leo miaka 1499 inayosadifiana na tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal miaka 53 kabla ya Hijria, kwa kauli ya baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu akiwemo Mas'udi, alizaliwa Mtume Muhammad SAW.

Wanachuoni wengine wa Kiislamu wanaamini kwamba, Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huohuo. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani.

Wiki ya umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu.     

Tarehe 12 Rabiul Awwal mwaka wa kwanza Hijria, Mtume Muhammad (saw) aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa msikiti wa kwanza kabisa katika Uislamu katika kijiji cha Quba kilichoko pambizoni mwa Madina.

Mtume (saw) aliweka jiwe la msingi la msikiti huo wa kihistoria wakati aliposimama kwa siku chache katika eneo la Quba akiwa njiani kutoka Makka akielekea Madina. Mtukufu huyo alisimama kwa muda katika kijiji cha Quba akimsubiri Ali bin Abi Twalib na jamaa wa familia ya Mtume.   

Msikiti wa Quba

Siku kama ya leo miaka 1205 iliyopita, inayosadifiana na 12 Rabiul Awwal 241 Hijria, alifariki dunia Imam Ahmad bin Hanbal, mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu katika mji wa Baghdad, Iraq ya leo.

Ahmad bin Hanbal alizaliwa mwaka 124 Hijria, katika mji wa Baghdad na kupata elimu ya kidini katika mji huo kutoka kwa maulamaa wakubwa akiwemo Imam Shafii. Imam Hanbal alisafiri katika miji kadhaa kama vile Kufa, Basra, Makka, Madina, Sham na Yemen kwa minajili ya kukusanya Hadithi za Bwana Mtume SAW.

Ahmad bin Hanbal ni mwasisi wa madhehebu ya Kisuni ya Hanbal na ameacha kitabu mashuhuri cha Hadithi, kiitwacho al Musnad.   

Miaka 288 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Daniel Gabriel Fahrenheit mwanahesabati na mwanafizikia wa Kijerumani aliyevumbua kipimajoto yaani thermometer, akiwa na umri wa miaka 50.

Fahrenheit alikuwa na fikra ya kubuni kifaa ambacho kingekuwa na uwezo wa kupima kiwango cha joto na mwaka 1724 mwanafizikia huyo Mjerumani akafanikiwa kutengeneza kipimajoto hicho. Kifaa hicho ambacho kimepewa jina la msomi huyo mwenyewe yaani Fahreinheit, bado kinatumika hadi leo.

Daniel Gabriel Fahrenheit

Siku kama ya leo miaka 203 iliyopita, Mexico ilijipatia uhuru.

Mexico ilipata uhuru baada ya miaka 300 ya kukoloniwa na Uhispania. Siku hii inatambulika kuwa siku ya kitaifa ya nchi hiyo. Nchi ya Mexico yenye kilomita za mraba 1,958,201 iko Amerika ya Kati na inapakana na Marekani na Guatemala. Akthari ya watu wa Mexico ni Wakatoliki.

Mji mkuu wa nchi hii ni Mexico City na sarafu yake ni peso. Wengi wa watu wa Mexico wana rangi mchanganyiko na wanazungumza Kihispania. 

Miaka 93 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, aliuawa Omar al Mukhtar kiongozi wa taifa la Libya katika mapambano ya ukombozi dhidi ya wakoloni wa Italia.

Omar Mukhtar aliyekuwa kiongozi wa kidini alizaliwa mwaka 1859. Mwaka 1895 alielekea Sudan na kushiriki katika harakati za kupambana na ukoloni wa Uingereza. Baada ya kushindwa kwa harakati hizo, Omar Mukhtar alirejea nchini Libya.

Mwaka 1911 Wataliano waliivamia Libya kwa lengo la kuitawala nchi hiyo. Kiongozi huyo wa kidini aliwahimiza wapiganaji wa makabila ya Libya kusimama kidete na kupambana dhidi ya wavamizi wa Kitaliano na kuwasababishia hasara kubwa. Hata hivyo, kwa kutumia askari wengi zaidi na silaha za kisasa, wavamizi hao walimzingira Omar Mukhtar na wenzake na kumkamata na kisha wakamnyonga katika siku kama ya leo.

Omar Mukhtar

Siku kama ya leo miaka 92 iliyopita Sir Ronald Ross daktari mashuhuri wa Kiingereza na mvumbuzi wa chanzo cha ugonjwa wa Malaria alifariki dunia. 

Alizaliwa Mei 13 mwaka 1857 katika mji wa Almora huko India. Alielekea Uingereza akiwa mdogo na kusoka akiwa huko ambapo alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu PhD katika taaluma ya tiba.

Uvumbuzi wake wa chanzo cha Malaria ulikuwa na nafasi muhimu sana kwani uliandaa uwanja wa namna ya kukabiliana na maradhi hayo.

Mwaka 1902 Dakta Ronald Ross alitunukiwa tuzo ya Nobel. Hatimaye Daktari Ronald Ross aliaga dunia katika siku kama ya leo baada ya kuishi kwa muda wa miaka 75.

Sir Ronald Ross

Tarehe 16 Septemba miaka 85 iliyopita Warsaw mji mkuu wa Poland ulizingirwa na Wajerumani, katika mwezi wa kwanza wa Vita vya Pili vya Dunia.

Mashambulio ya wanajeshi wa Kinazi wa Ujerumani huko Poland yalianza siku 15 kabla ya kuanza vita hivyo.

Na leo tarehe 16 Septemba ni Siku ya Kimataifa ya Kulindwa Tabaka la Ozoni.

Siku hii haina historia ndefu ikilinganishwa na matukio mengine ya kimataifa. Siku hii iliainishwa mwaka 1994 wakati nchi wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa zilipokubaliana kutenga siku maalumu ya kulindwa tabaka la Ozoni. Tangu wakati huo nchi zote ziliahidi kuanza kuzalisha na kutumia nyenzo na vitu ambavyo havina madhara kwa tabaka hilo.

Lengo la maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Ozoni ni kuhamasisha kulindwa tabaka hilo muhimu sana linalowalinda viumbe hai ardhini wasiathiriwe na mionzi hatari ya Kikiuka Urujuani (Ultraviolet).