Sep 17, 2024 02:27 UTC
  • Jumanne, tarehe 17 Septemba, 2024

Leo ni Jumanne tarehe 13 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1446 Hijria sawa na Septemba 17 mwaka 2024.

iKatika siku kama ya leo miaka 1156 alizaliwa Qadhi Jorjani maarufu kwa lakabu ya Abulhassan, faqihi, mwandishi na malenga wa Kiislamu.

Jorjani alifunzwa masomo hayo ya kidini na Qadhi Mkuu wa mji wa Rei ulioko karibu na Tehran ya leo.

Qadhi Jorjani ameandika vitabu vingi na miongoni mwake ni "Tafsirul Qur'an" na "Tahdhib al Tarikh". Qadhi Jorjani alifariki dunia mwaka 366 Hijria huko Neishabur na akazikwa huko Jorjan au Gorgan ya leo kaskazini mashariki mwa Iran.   

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, aliaga dunia Emil Ludwig mwandishi wa wasifu wa Kijerumani.

Alizaliwa 1881 katika mji wa Breslau nchini Ujerumani ambao leo hii ni sehemu ya ardhi ya Poland. Alipata umashuhuri katika nusu ya pili ya karne ya 19 baada ya kuandika wasifu wa Otto Van Bismarck Kansela wa wakati huo wa Ujerumani, kiongozi wa zamani wa Russia Joseph Stalin, Beethoven na rais wa zamani wa Marekani Franklin Roosevelt.

Wakati wa Vita vya Pili vya Dunia Ludwig alikuwa mwandishi wa habari aliyepata nafasi ya kufanya mahojiano na watawala waliokuwa na satua na ushawishi mkubwa katika kipindi hicho kama Franklin Delano Roosevelt, Winston Churchil na Joseph Stalin. 

Emil Ludwig

Tarehe 17 Septemba miaka 63 iliyopita aliuawa waziri mkuu wa zamani wa Uturuki, Adnan Menderes.

Alizaliwa mwaka 1899 na kupata elimu katika taaluma ya sheria. Alijiunga na harakati za kisiasa akiwa bado kijana na alishika hatamu za uongozi nchini Uturuki kama waziri mkuu mwaka 1950. Menderes ambaye alikuwa akifuata siasa za sera za kimarekani, alituma vikosi vya jeshi kushambulia Wakurdi wa nchi hiyo, suala ambalo liliwakasirisha sana wasomi na wanafikra wengi nchini Uturuki.

Mwaka 1957 alichaguliwa tena kuwa Waziri Mkuu wa Uturuki na kukandamiza maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu waliokuwa wakipinga utawala wake na kudai marekebisho ya kisiasa.

Mwaka 1960 Adnan Menderes aliondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi na kufikishwa mahakamani ambapo alihukumiwa kifo kwa kupatikana na hatia ya kuua wanafunzi wa vyuo vikuu, kukiuka katiba ya nchi na kuwa na mahusiano haramu.

Usiku wa kutekelezwa hukumu ya kifo, Menderes alifanya jaribio la kujiua lakini madaktari waliwahi kuokoa maisha yake. Hatimaye tarehe 17 Septemba, Adnan Menderes alinyongwa akiwa na umri wa miaka 62.

Adnan Menderes

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita sawa na tarehe 17 Septemba 1982, wanamgambo wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa kundi la Mafalanja, wakipata himaya ya askari wa utawala haramu wa Israel, walifanya mauaji makubwa katika kambi za wakimbizi wa Kipalestina huko Sabra na Shatila nchini Lebanon.

Ilikuwa Juni mwaka 1982 wakati askari 150,000 wa utawala haramu wa Israel walipoishambulia Lebanon na kuukalia kwa mabavu baada ya kuwalazimisha wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO kuondoka Beirut.

Kwa amri ya Menachem Begin Waziri Mkuu wa wakati huo wa Israel na Ariel Sharon Waziri wa Vita wa utawala huo, tarehe kama ya leo askari wa Israel waliizingira kambi za Sabra na Shatila kisha mafalanja wa Lebanon wakaanza kufanya mauaji ya kinyama dhidi ya wakimbizi wa Kipalestina waliokuwamo katika katika kambi hizo. Wapalestina wasiokuwa na hatia 3,300 waliuawa shahidi katika mashambulio hayo.  ***