Sep 23, 2024 02:41 UTC
  • Jumatatu, 23 Septemba, 2024

Leo ni Jumatatu tarehe 19 Rabiul Awwal 1446 Hijria imayosadifiana na tarehe 23 Septemba 2024.

Miaka 349 iliyopita katika siku kama ya leo, Valentin Conrart mwandishi na mwanafasihi wa Kifaransa aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 72.

Alizaliwa mwaka 1603 katika familia iliyokuwa na mapenzi makubwa na fasihi ya lugha na kwa msingi huo ndio maana alipokuwa katika rika la ujana, Valentin Conrart akawa na mapenzi na taaluma ya fasihi ya lugha na taratibu akaanza kujihusisha na fani ya uandishi.

Valentin Conrart

Siku kama ya leo miaka 92 iliyopita sawa na Septemba 23 mwaka 1932, Saudi Arabia iliasisiwa, na Abdulaziz bin Saud akawa mfalme wa nchi hiyo.

Bara Arabu au Hijaz ni mahali alipotokea Mtume wa Uislamu Muhammad S.A.W. Saudi Arabia ilijitoa chini ya udhibiti wa utawala wa Abassiya mwanzoni mwa karne ya tatu Hijria na hadi karne kadhaa badaye, nchi hiyo iliendelea kuwa na ukosefu wa amani.

Jitihada za al Saud za kutaka kuiongoza Saudia zilianza katikati mwa karne ya 18 na kushika kasi zaidi mwanzoni mwa karne ya 20.

Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, aliaga dunia Sigmund Freud daktari wa magonjwa ya akili raia wa Austria.

Sigmund alizaliwa mwaka 1856. Daktari huyo alifanya utafiti na kuchunguza matatizo mbalimbali ya kiakili yanayomkumba binadamu na kutoa maoni na nadharia mpya kuhusu chanzo cha magonjwa ya akili.

Kwa sababu hiyo anahesabiwa kuwa mwasisi wa elimu ya uchunguzi wa kisaikolojia au Psychoanalysis.

Sigmund Freud

Miaka 46 iliyopita katika siku kama hii ya leo, askari usalama wa utawala wa Baath nchini Iraq wakishirikiana na utawala wa Shah waliizingira nyumba ya Imam Khomeini, Mwenyezi Mungu amrehemu, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu huko Najaf.

Kwa kuzingatia uhusiano wake mzuri na utawala wa Shah, utawala wa zamani wa Iraq ulimtaka Imam Khomeini asifanye mahojiano na waandishi wa habari, kutoa taarifa, kuhutubia wala kuzungumzia hali ya mambo ya Iran dhidi ya utawala wa Shah.

Imam Khomeini aliwajibu kwa kusema kuwa: "Nitatekeleza wajibu wangu wa kisheria popote pale nitakapokuwa." Baada ya hapo, serikali ya wakati huo ya Iraq, ilimlazimisha Imam Khomeini kuondoka Iraq na hatua hiyo ikaandaa uwanja wa hijra ya kihistoria ya Imam Khomeini ya kuelekea Paris, Ufaransa na kupamba moto harakati za Mapinduzi ya Kiislamu.

Imam Khomeini akiwa Najaf, Iraq